Vifo vya mahujaji vyarejesha upya uhasama wa Iran, Saudia | Matukio ya Kisiasa | DW | 27.09.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Vifo vya mahujaji vyarejesha upya uhasama wa Iran, Saudia

Idadi ya mahujaji waliokufa kutokana na mkanyagano nchini Saudi Arabia imefikia 769, huku Iran ikitangaza azma yake ya kuchukuwa hatua za kisheria dhidi ya utawala wa Saudia kwa maafa hayo.

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Rais Hassan Rouhani wa Iran aliitumia hotuba yake mbele ya Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York siku ya Jumamosi (26 Septemba) kutaka ufanyike uchunguzi juu ya ajali hiyo kwenye ibada ya kila mwaka ya Hijja, ambayo hadi sasa miongoni mwa waliothibitishwa kupoteza maisha ni raia 136 wa Iran.

Ukweli kwamba Rouhani alitumia mkutano wa kilele wa Umoja wa Mataifa kuhusu malengo endelevu ya milenia kurejelea hasira za nchi yake juu ya mkasa huo wa Hijja unaonesha kwamba serikali yake haiko tayari kuacha ukosoaji wake dhidi ya hasimu wake mkuu kwenye eneo la Ghuba, Saudi Arabia. Mataifa hayo mawili yanajiona ndiyo viongozi wa umma wa Waislamu duniani.

Kwenye hotuba yake hiyo mbele ya mataifa 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa, Rouhani alitilia mkazo haja ya kufanyika uchunguzi juu ya "sababu za ajali hiyo na matukio mengine kama hayo kwenye Hijja ya mwaka huu", huku akiielezea ajali hiyo kuwa inachoma nyoyo.

Rouhani alisema huenda mkasa huo ulisababishwa na uamuzi wa Saudi Arabia kuwaondoa wanajeshi wake wenye uzoefu na kuwapeleka vitani nchini Yemen kupambana na waasi wa Kihouthi, wanaoshukiwa kuungwa mkono na Iran, hatua ambayo daima imekuwa ikipingwa na serikali ya Iran.

Wiki moja kabla ya mkasa huu, winji ilianguka katika Msikiti Mtakatifu wa Makka na kuwauwa watu 110 na kuwajeruhi wengine kadhaa, wengi wao wakiwa mahujaji wa kigeni.

Saudi Arabia yajibu

Wafanyakazi wa huduma ya uokozi wa Saudi Arabia wakiwahudumia majeruhi wa ajali ya Mina, Makka.

Wafanyakazi wa huduma ya uokozi wa Saudi Arabia wakiwahudumia majeruhi wa ajali ya Mina, Makka.

Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia, Adel al-Jubeir, aliwaambia waandishi wa habari jijini New York kwamba Iran haipaswi kuingiza siasa kwenye msiba huu mkubwa kwa umma wa Kiislamu uliowakumba watu ambao walikuwa wakitelekeza nguzo muhimu ya dini yao, yaani Hijja.

Al-Jubeir aliwahakikishia waandishi akiwa mbele ya mwenzake wa Marekani, John Kerry, kwamba serikali yake itafanya uchunguzi wa kina. "Tutausema ukweli wote kama unavyojitokeza, na hatutaficha kitu. Ikiwa makosa yalifanyika, aliyeyafanya atawajibika. Na tutahakikisha kuwa tunajifunza kwa hili na kamwe halitarejea."

Siku ya Ijumaa, Saudi Arabia ilisema mahujaji waliokuwa wamedharau kanuni za udhibiti wa mkusanyiko ndio wa kulaumiwa kwa tukio hilo. Mfalme Salman aliamuru kupitiwa upya kwa mipango ya hija, huku waziri wake wa afya, Khalid al-Falih, akisema uchunguzi ungelifanyika.

Kwa mujibu wa mashahidi, watu walikufa aidha kwa kukosa hewa au kukanyagwa siku ya Alhamisi pale makundi mawili ya mahujaji yalipojikuta yakibanana kwenye ujia mmoja mwembamba, katika kile kinachoelezewa kuwa ni ajali mbaya kabisa kuwahi kutokea kwenye ibada hiyo ndani ya robo karne nzima.

Iran inadai Saudi Arabia ina usimamizi mbovu sana wa Hijja, tukio linalowakusanya zaidi ya waumini milioni 2 wa Kiislamu kila mwaka kutoka mataifa 180 duniani.

Mashitaka mbele ya mahakama za kimataifa

Wafanyakazi wa huduma ya uokozi wa Saudi Arabia wakiwahudumia majeruhi wa ajali ya Mina, Makka.

Wafanyakazi wa huduma ya uokozi wa Saudi Arabia wakiwahudumia majeruhi wa ajali ya Mina, Makka.

Hadi sasa, Iran ndiyo yenye watu wengi zaidi waliokwishatambuliwa kupoteza maisha kwenye mkasa huo. Televisheni ya taifa ya nchi hiyo inasema mabalozi wa zamani wa Iran nchini Lebanon na Slovenia, waandishi wawili wa televisheni hiyo na mchambuzi mmoja mashuhuri wa masuala ya kisiasa ni miongoni mwa waliokufa.

Mapema, mwendesha mashitaka wa serikali, Ebrahim Raisi, aliiambia televisheni hiyo kwamba kwa mujibu wa sheria za kimataifa, tukio hilo linapaswa kuchunguzwa, na utawala wa al-Saud lazima ujibu. Aliongeza kuwa mamlaka nchini Saudi Arabia ziliifunga barabara inayotumiwa na mahujaji na kuruhusu msafara wa kifalme kupita, na hivyo kusababisha msongomano mkubwa mjini Mina, nje kidogo ya mji wa Makka.

"Wanapaswa kujuwa kwamba tutaanzisha kesi dhidi ya al-Saud kwa uhalifu walioufanya dhidi ya mahujaji kupitia mahakama na jumuiya za kimataifa," alisema mwendesha mashitaka huyo.

Hata hivyo, si Iran wala Saudi Arabia iliyo mwanachama wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), na ni mwendesha mashitaka wa mahakama hiyo tu ndiye anayeweza kufungua mashitaka kama hayo. Iran ingeliweza kufungua kesi kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Haki, ambayo huamua migogoro kati ya mataifa, lakini mahakama hiyo haihusiki na kesi za uhalifu.

Bado Saudi Arabia haijasema kitu kuhusu tuhuma za msafara wa ukoo wa kifalme, lakini msemaji wa wizara ya mambo ya ndani ya nchi huyo, Meja Jenerali Mansour al-Turki, aliliambia shirika la habari la Associated Press kwamba msafara uliokwenda Mina siku ya Alhamisi haukuhusika kabisa na ajali, kwani ulipita kwenye upande tafauti wa mji.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/AP
Mhariri: Isaac Gamba

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com