Vettel aukamilisha msimu wa Formula One kwa kishindo | Michezo | DW | 25.11.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Vettel aukamilisha msimu wa Formula One kwa kishindo

Sebastian Vettel ameukamilisha msimu wa mashindano ya mbio za magari ya Formula One nchini Brazil kwa kupata ushindi wake wa tisa mfululizo na kuifikia rekodi iliyowekwa na dereva Michael Schumacher

Sebastian Vettel akisheherekea ushindi wake katika mkondo wa Grand Prix

Sebastian Vettel akisheherekea ushindi wake katika mkondo wa Grand Prix

Sebastian Vettel hakuwa na zawadi yoyote ya kumwambia kwaheri dereva mwenzake wa timu ya Red Bull Mark Webber katika mashindano ya jana nchini Brazil, lakini anafahamu kuwa ni bora kufurahia ushindi wake wa karibuni kwa namna anavyoweza kabla ya mchezo wa Formula One kufanywa mabadiliko makubwa msimu ujao.

Bingwa huyo mara nne wa ulimwengu alimaliza wa kwanza katika mkondo wa Brazil mbele ya Mark Webber, na kuifikia rekodi iliyowekwa na Michael Schumacher ya kushinda mikondo 13 katika msimu mmoja pamoja na ile ya Alberto Ascari ambaye alishinda mikondo tisa mfululizo katika mwaka wa 1952 na 1953.

Vettel mwenye umri wa miaka 26 anaweza kuboresha rekodi hiyo na kufikisha 10 wakati msimu wa 2014 utakapong'oa nanga nchini Australia mnamo Machi 16. lakini magari yatakayotumiwa mwaka huo yatakuwa tofauti sana na muundo wa yale ya mwaka huu na hiyo huenda ikawa changamoto kwa madereva kupata uzoefu.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alikuwa miongoni mwa waliotuma ujumbe wa kumpongeza dereva huyo kutokana na mafanikio hayo. Nasi hapa pia tunamtumia pongezi zetu. Na kufikia hapo ndipo natia kikomo michezo kwa leo, mimi ni Bruce Amani kutoka Bonn.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/Reuters

Mhariri: Yusuf Saumu