Venezuela: Umoja wa Ulaya wapanga kumtambua Juan Guaido | Matukio ya Kisiasa | DW | 03.02.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Venezuela

Venezuela: Umoja wa Ulaya wapanga kumtambua Juan Guaido

Viongozi wa nchi saba za Umoja wa Ulaya wamesema watamtambua kiongozi wa upinzani nchini Venezuela Juan Guaido huku muda waliompa Maduro wa kuitisha uchaguzi mpya nchini Venezuela unakaribia kumalizika.

Kiongozi wa upinzani nchini Venezuela Juan Guaido (picture-alliance/dpa/sincepto/R. Hernandez)

Kiongozi wa upinzani nchini Venezuela Juan Guaido

Ufaransa, Ujerumani, Uingereza, Ureno, Uholanzi, Ubelgiji pamoja na nchi zingine kadhaa zimesema zitamtambua rasmi Juan Guaido kama Rais iwapo Nicolas Maduro hatokuwa ametangaza kufanyika uchaguzi mpya kabla ya kipindi cha siku nane kumalizika siku ya Jumapili tarehe 03.02.2019.

Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini amesema mawaziri wa nchi za Ulaya na wenzao wa nchi za Amerika ya Kusini watakutana siku ya Alhamisi kwenye mkutano wao wa kwanza katika mji wa Montevideo, Uruguay. Kwenye mkutano huo mawaziri hao wanatarajiwa kutafuta mikakati ya kuumaliza mgogoro wa kisiasa wa nchini Venezuela.  

Rais wa Marekani Donald Trump amesema kuwapeleka wanajeshi nchini Venezuela ni hatua mojawapo inayoweza kuchukuliwa na nchi yake. Mnamo siku ya Jumamosi kundi linalomuunga mkono Rais Maduro na wafuasi wa kiongozi wa upinzani Juan Guaido walifanya maandamano makubwa mjini Caracas.

Federica Mogherini (picture-alliance/Photoshot/S. Di Nolfi)

Federica Mogherini, Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya

Kwenye maandamano hayo Rais Maduro alipendekeza juu ya uwezekano wa kuitisha uchaguzi wa bunge huku Guaido akiwaambia wafuasi wake juu ya mikakati ya kuingizwa misaada katika nchi hiyo iliyowekewa vikwazo na Marekani kupitia Colombia na Brazil. Rais Maduro amekuwa anapinga kuingizwa misaada hiyo kwa madai kwamba Marekani itapata fursa ya kuivamia nchi hiyo kijeshi.

Jeshi la nchini Venezuela linamuunga mkono Rais Maduro lakini mkuu wa kikosi cha wanaanga Jenerali Francisco Yanez wiki iliyopita aliungana na upande wa upinzani. Juan Guaido, alijitangaza mwishoni mwa mwezi Januari kuwa Rais wa mpito wa Venezuela na anataka uchaguzi mpya wa Rais ufanyike.

Mwandishi: Zainab Aziz/p.dw.com/p/3CdTF/APE/RTRE

Mhariri: John Juma

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com