1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki yasifu hatua ya Özil

Lilian Mtono
23 Julai 2018

Mawaziri wa Uturuki hii leo wamesifu maamuzi ya mchezaji wa Ujerumani mwenye asili ya Uturuki, Mesut Özil, ya kutangaza kuachana na timu ya taifa ya soka ya Ujerumani kwa misingi ya ubaguzi wa rangi.

https://p.dw.com/p/31uhS
WM 2018 Deutschland Südkorea Mesut Özil
Picha: picture-alliance/Photoshot/L. Ga

Waziri wa mambo ya ndani nchini humo ameitaja hatua hiyo kuwa "goli dhidi ya virusi vya Ufashisti”.

Özil aliyezaliwa nchini Ujerumani katika familia yenye asili ya Kituruki, hivi karibuni amekabiliwa na ukosoaji mkubwa tangu alipopiga picha na rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan mnamo mwezi Mei na kuibua utata mkubwa, uliogubikwa na maswali kuhusu uaminifu wake kwenye kikosi cha Ujerumani, kilipokuwa kikijiandaa na mashindano ya kombe ya dunia mwezi Juni, nchini Urusi.

Baada ya wiki kadhaa za ukimya, Özil alichapisha waraka, uliosambaa kupitia mitandao ya kijamii akisema, "kwa moyo mzito na baada ya kufikria sana kufuatia matukio ya hivi karibuni, sitaendelea kuwa sehemu ya kikosi cha timu ya taifa ya Ujerumani, wakati nikiwa na hisia ya kubaguliwa na kutoheshimiwa".

Mchezaji huyo kiungo wa timu inayocheza ligi kuu ya Uingereza ya Arsenal, amekosolewa pakubwa na uongozi wa shirikisho la soka la Ujerumani, DFB, kutokana na picha hiyo, lakini pia akilaumiwa na baadhi ya Wajerumani baada ya timu hiyo kufanya vibaya kwenye kombe la dunia nchini Urusi, baada ya kuondolewa kwenye hatua ya makundi ya michuano ya kombe la dunia.

Chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha Mbadala wa Ujerumani, AfD, kilikuwa cha kwanza kumlaumu Özil kwa kushindwa kwa timu ya taifa ya Ujerumani katika hatua hizo za mwanzo. Mbunge wa chama hicho, Jens Amier kwenye ukurasa wa twitter aliandika "bila ya Özil, tungeshinda!"

Berlin Mesut Özil Kabine Merkel
Mesut Özil akipeana mkono na Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: picture-alliance/dpa/Bundesregierung/G. Bergmann

Özil alisisitiza kwamba alikuwa mwaminifu kwa asili zake zote mbili, na hakunuia chochote ambacho kingeibua matamko ya kisiasa, baada ya picha hiyo na rais Erdogan. Mchezaji mwenzake wa kimataifa Ilkay Gundogan anayechezea Manchester City ya Uingereza pia alikuwepo, walipokutana na rais Erdogan, alipokuwa ziarani Uingereza, pamoja na mshambuliaji Cenk Tosun anayechezea Everton, aliyezaliwa Ujerumani, lakini akiiwakilisha Uturuki.

Mawaziri wa Uturuki wamsifu Özil.

Waziri wa sheria wa Uturuki, Abdulhamit Gul aliandika kwenye ukurasa wake wa twitter akimpongeza Özil, akisema hatua ya kuachana na timu hiyo ni kama goli muhimu dhidi ya virusi vya siasa za Kifashisti.

Waziri wa michezo Mehmet Kasapoglu, naye aliweka picha ya Özil akiwa anatabasamu, aliyopiga na Erdogan, na kuandika "tunaunga mkono hatua hii muhimu ambayo ndugu yetu ameichukua.”

Özil mwenye miaka 29, aliandika kwenye waraka wake huo mrefu na mkali kupitia ukurasa wake wa twitter, akimzungumzia  rais wa DFB Reinhard Grindel akisema hataendelea kuchukuliwa kama kisingizio cha Grindel aliyeshindwa kufanya kazi yake vizuri. Aliongeza kuwa na hapa namnukuu, "mbele ya macho ya Grindel na wafuasi wake, mimi ni Mjerumani tukishinda, lakini tukishindwa mimi ni mhamiaji.” Mwisho wa kumnukuu. 

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel kupitia msemaji wa serikali amesema anamthamini Özil, na ni mchezaji mzuri, aliyefanya mengi akiwa na timu ya taifa.

Mwandishi: Lilian Mtono/AFPE/DW.

Mhariri: Iddi Ssessanga