Uturuki yaikabidhi Ujerumani ′orodha ya magaidi′ | Matukio ya Kisiasa | DW | 20.07.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Uturuki yaikabidhi Ujerumani 'orodha ya magaidi'

Serikali ya Uturuki imeikabidhi Ujerumani orodha ya kampuni kadhaa za Kijerumani na watu binafsi ambao inadai wana uhusiano na mhubiri wa Kiislamu wa Uturuki anayeishi nchini Marekani, Fethullah Gulen.

Orodha hiyo ya kampuni 68 za Ujerumani pamoja na watu binafsi imekabidhiwa kwa jeshi la polisi la Ujerumani. Hayo ni kwa mujibu wa gazeti la kila wiki la Die Zeit lililochapishwa jana Jumatano. Orodha hiyo inaijumuisha kampuni kubwa ya kutengeneza magari Daimler pamoja na kampuni ya madawa ya BASF. Hata hivyo, duru za polisi zimeiita orodha hiyo ''ya kipuuzi'' na isiyo na maana.

Uturuki inamshutumu Gulen pamoja na wafuasi wake kwa kuhusika na jaribio la mapinduzi lililoshindikana mwaka mmoja uliopita, ambapo zaidi ya raia 250 walipoteza maisha yao katika ghasia. Kundi la Gulen ambaye ni adui wa Rais Recep Tayyip Erdogan limepigwa marufuku na limeorodheshwa na Uturuki kama kundi la kigaidi.

Orodha hiyo iliwasilishwa kwa mamlaka za Ujerumani wiki kadhaa zilizopita na imezitaja kampuni hizo kama zinazounga mkono ugaidi. Orodha hiyo pia inaujumuisha mkahawa wa chakula wa Kituruki pamoja na duka moja linalouza chakula hadi usiku wa manane.

Fethullah Gülen (picture alliance/dpa/M.Smith)

Fethullah Gulen

Mapema mwezi huu, Rais Erdogan aliliambia gazeti la Die Zeit kwamba maafisa wake walituma nchini Ujerumani mafaili 4,500 ya watu wanaofungamana na Gulen na kuitaka nchi hiyo iwakabidhi kwa Uturuki.

Uturuki yataka ikabidhiwe magaidi

Erdogan alisema Ujerumani inapaswa kuwakabidhi magaidi hao kwa Uturuki na iwapo hilo halitofanyika, basi Uturuki itaichukulia Ujerumani kama nchi inayowalinda magaidi. Kwa mujibu wa gazeti la Die Zeit, Idara ya Upelelezi ya Shirikisho la Ujerumani, BKA imeomba kupatiwa maelezo zaidi kutoka kwa maafisa wenzao wa Uturuki, lakini haijapata majibu hadi sasa.

Hayo yanajiri wakati mvutano kati ya mataifa hayo mawili ukizidi kushamiri. Kwa muda mrefu Ujerumani imekuwa katika mvutano wa kidiplomasia na Uturuki, huku Ujerumani ikiukosoa utawala wa Rais Erdogan kwa kutumia nguvu kuwanyamazisha wapinzani wake wa kisiasa. Mapema jana, Ujerumani ilimuita balozi wa Uturuki mjini Berlin ikiwa ni katika kupinga hatua ya kukamatwa kwa wanaharakati kadhaa wa haki za binaadamu, akiwemo raia wa Ujerumani Peter Steudtner. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje, Martin Schaefer amesema jambo hilo halikubaliki.

Porträt Peter Steudtner (privat)

Mwanaharakati Peter Steudtner

''Balozi wa Uturuki alielezwa wazi kwamba hatua ya kukamatwa Peter Steudtner na wanaharakati wengine wa haki za binadamu haikubaliki. Serikali ya Ujerumani inataka kuachiwa haraka Peter Steudtner,'' alisema Schaefer.

Hata hivyo, Uturuki leo imeupuuza ukosoaji huo wa Ujerumani. Aidha, Ujerumani imesema itaangalia upya uhusiano wake na Uturuki. Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Sigmar Gabriel, amesema serikali ya Ujerumani imewaonya raia wake wanaosafiri kwenda Uturuki, kwamba wako katika hatari ya kukamatwa.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP, AP, DPA, http://bit.ly/2gMHk8I
Mhariri: Daniel Gakuba

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com