1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki na China wapanua uhusiano licha ya tofauti zao

Amina Mjahid Yusuf Saumu
2 Julai 2019

Uturuki na China zimepanua ushirikiano wao lakini uhusiano baina ya nchi hizo bado unakabiliwa na hali ya kutoaminiana pamoja na ushindani.

https://p.dw.com/p/3LSGs
China G20-Gipfel Xi Jinping mit Recep Tayyip Erdogan
Picha: picture-alliance/AA/Turkish Presidency/Y. Bulbul

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan  ameanza ziara yake mjini Beijing hii leo Jumanne kukutana na mwenzake wa China Xi Jinping.

Mataifa hayo mawili yana nia ya kukuza ushirikiano wao kiuchumi na kisiasa wakati wakipitia kipindi kigumu katika mahusiano yao na Marekani.

Uhusiano wa Uturuki na Marekani pamoja na washirika wake wa Mataifa ya Magharibi umezidi kuingia doa kufuatia tofauti zao katika mgogoro wa Syria, mpango wa Uturuki wa kununua mfumo wa makombora ya Urusi aina ya S-400, na kurejea nyuma kidemokrasia baada ya jaribio la mapinduzi yaliyoshindwa  mwezi Juni mwaka 2016.

Kuharibika kwa uhusiano huo kumezua hisia kutoka kwa baadhi ya waangalizi kuwa Uturuki, ambaye ni mwanachama wa Jumuiya ya kujihami NATO huenda ikawa inapanga mikakati ya kuuelekeza uhusiano  wake  kutoka Magharibi kuelekea Mashariki, kutokana na tamko la Rais Erdogan, kwamba Uturuki inaweza kujiunga na shirika la ushirikiano la Shanghai ambalo ni bodi ya usalama inayoyajumuisha mataifa ya China, Urusi na mataifa manne ya Asia ya kati.

Wataalamu wasema uhusiano wa Uturuki na China ni wa kiuchumi zaidi

Türkei Wahlen Wahlkampf Recep Tayyip Erdogan
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan Picha: Reuters/M. Sezer

Hata hivyo wataalamu wa mambo wanasema mkutano huu wa nane na rais XI tangu mwaka 2012, unahusu zaidi uchumi na kupanua uhusiano wao lakini sio sehemu ya mpango wa kimkakati wa kuegemea  upande wa Mashariki.

"Uhusiano wa Uturuki na China hauwezi ukachukua nafasi ya ushirikiano wa taifa hilo na Marekani au na Umoja wa Ulaya, Uturuki ina uhusiano mkubwa na ulio na faida na mataifa ya Magharibi," alisema Altay Atli, mhadhiri katika chuo kikuu cha Koc mjini Istanbul aliyebobea katika masuala ya uhusiano kati ya Uturuki na mataifa ya Asia.

Atli ameongeza kuwa sera za kigeni za Uturuki zinalenga kuifanya nchi hiyo kuwa na ushawishi kimataifa na kupanua uhusiano wake na mataifa yote, tofauti na hali ilivyokuwa katika vita baridi ikiwa imejisogeza zaidi upande wa Magharibi.

Tofauti kubwa kati ya mataifa haya mawili ni siasa na athari ya siasa hizo katika kanda yake.  Kati ya mambo China na Uturuki wanayotofautiana baina yao ni mgogoro wa wenyewe kwa wenyewe wa Syria, ambapo Uturuki inaunga mkono upinzani na China imekuwa ikiiunga mkono serikali ya Assad  kiuchumi na kisiasa pamoja na uingiliaji wa kijeshi nchini humo unaofanywa na Urusi.

Chanzo: DW Page