Uturuki kutumia njia zozote kupambana na PKK | Matukio ya Kisiasa | DW | 22.10.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Uturuki kutumia njia zozote kupambana na PKK

Uturuki inatangaza kuwa iko tayari kuchukua hatua zozote zile ili kuwamaliza wapiganaji wa Kikurdi wa PKK baada ya wanajeshi 12 na waasi 32 kuuawa katika mapigano kwenye eneo linalopakana na Iraq.Tangazo hilo linatolewa baada ya kikao cha dharura kufanyika kati ya viongozi wa Uturuki wa kiraia na kijeshi .Kikao hicho kiliongozwa na rais wa Uturuki Abdula Gul.Zaidi ya watu alfu 37 wameuawa tangu mwaka 1984 pale wapiganaji wa PKK walipoanzisha mashambulizi ya kutaka kujitenga kwenye eneo la kusini mashariki mwa Uturuki

Wapiganaji wa PKK

Wapiganaji wa PKK

Mapigano hayo yanafanyika siku nne baada ya bunge la Uuturuki kuidhinisha hatua ya kupeleka vikosi katika eneo la kaskazini mwa Iraq ili kushambuliwa waasi 3500 wa PKK wanaojificha kwenye eneo hilo.

Waziri Mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan anasema kuwa serikali yake iko tayari kutumia uwezo wake wa kupeleka vikosi nchini Iraq ili kwashambulia waasi hao wa PKK ila anaongeza kuwa ni katika mazingira yanayokubalika.Kwa mujibu wa taarifa ya kiongozi huyo Uturuki haitavumilia ugaidi japo inaheshimu uongozi wa Iraq ila haitachelea kulinda haki zake na raia wake.

''Uturuki haitashirikiana na nchi yoyote ambayo haiku tayari kukubali kuwa kundi la waasi la PKK ni kundi la kigaidi.''

Kiongozi huyo aliyasema hayo alipofanya mkutano na waandishi wa habari mjini Ankara baada ya kikao hicho cha dharura.Kulingana na Waziri wa Ulinzi wa Uturuki Vecdi Gonul,nchi yake haina mipango ya dharura ya kuvuka mpaka ili kufanya mashambulizi.Bwana Gonul aliyasema hayo alipokutana na mwenzake wa Marekani Robert Gates.Waziri Mkuu Erdogan anaongeza kuwa anaishawishi Marekani kushambulia kambi za waasi wa PKK alipozungumza na Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bi Condoleeza Rice aliyetoa wito wa kupewa muda zaidi.Marekani kwa upande wake inapinga vikali hatua ya Uturuki kufanya mashambulizi yoyote kwenye eneo la kaskazini mwa Iraq jambo ambalo huenda likahatarisha amani katika eneo hilo la utulivu.Rais Bush anatilia mkazo zaidi ushirikiano kati ya Uturuki na waasi wa PKK na kutoa wito kwa Iraq kutafuta suluhu bila kuvuka mipaka.Robert Gates ni Waziri wa Ulinzi wa Marekani

''Mashambulizi kwenye eneo la mpakani kati ya pande hizo mbili hayatanufaisha Uturuki…. Sisi Marekani …..aidha Iraq''

Kwa upande mwingine Waziri Mkuu wa Iraq Nuri al Maliki alishtumu hadharani kundi la waasi wa PKK saa chache baada ya bunge la Iraq kuidhinisha mswada unaolaani tishio la Uturuki la kufanya mashambulizi kwenye eneo la Wakurdi wengi la kaskazini mwa Iraq.Viongozi wa kiKurdi wa eneo hilo wanasema kuwa watahakirisha shambulio lolote katika eneo lao.

Mapigano yalizuka katika eneo la milima mingi lililo katika mkoa wa kusini mashariki wa Hakkari baada ya waasi wa PKK waliotokea eneo la kaskazini mwa Iraq kuwashambulia wanajeshi walioshika doria jumamosi usiku.Uturuki inakabiliwa na ongezeko la ghasia jambo inaloifanya kufikiria sana kuchukua hatua za kijeshi.Kulingana na nchi hiyo Marekani wala Iraq hazijatia bidii ya kutosha ili kutafuta suluhu ya tatizo hilo la uasi. Wakati huohuo serikali ya Ujerumani inashtumu mashambulizi hayo ya mwishoni mwa juma ila inatoa wito kwa Uturuki kujizuia ili kudumisha usalama katika eneo hilo la mpakani lililo tulivu.Yapata watu alfu 3 waliobeba bendera ya Uturuki wameandamana hii leo kwenye eneo la Kadikoy ili kupinga vitendo vya mauaji vya waasi wa PKK.Maandamano hayo yanaingia siku yake ya pili.

 • Tarehe 22.10.2007
 • Mwandishi Thelma Mwadzaya
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/C7gg
 • Tarehe 22.10.2007
 • Mwandishi Thelma Mwadzaya
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/C7gg

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com