1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki kupewa euro bilioni 3 kuwasaidia wakimbizi

30 Novemba 2015

Umoja wa Ulaya unataka Uturuki isaidie kuzuia wimbi la wakimbizi kutoka Syria na wahamiaji wengine kuingia Ulaya. Wakati huo huo, Uturuki inadhamiria kupewa uanachama wa Umoja wa Ulaya.

https://p.dw.com/p/1HEUa
EU Türkei Gipfel in Brüssel
Picha: Reuters/E. Vidal

Uturuki itasaidia kuzuia wimbi la wakimbizi wanaoingia Ulaya ili ipatiwe fedha, viza na mazungumzo ya kujiunga na umoja wa Ulaya kuanzishwa tena, katika makubaliano yaliyoafikiwa jana. Viongozi wa mataifa 28 wanachama wa umoja huo walikutana jana jioni na waziri mkuu wa Uturuki Ahmet Davutoglu mjini Brussels, kuidhinisha makubaliano yaliyoandaliwa na wanadiplomasia katika wiki chache zilizopita.

Kipengele muhimu cha makubaliano hayo ni kitita cha euro bilioni tatu kama msaada wa Umoja wa Ulaya kwa wakimbizi milioni 2.2 kutoka Syria wanaoishi nchini Uturuki, zikilenga kuimarisha hali ya maisha na kuwashawishi wabakie nchini humo badala ya kujaribu kukimbilia visiwa vya Ugiriki na mataifa ya Umoja wa Ulaya.

Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Jean Claude Juncker alisema, "Tuko tayari kutoa euro bilioni tatu; kiwango hiki hakitolewi bure bila mafungamano. Pesa hizi ni kwa ajili ya matumizi katika hali itakayoamuliwa kwa pamoja na utawala wa Uturuki."

Makubaliano hayo yamethibitishwa na Rais wa baraza kuu la Umoja wa Ulaya Donald Tusk kufuatia mkutano wa kilele uliodumu muda wa masaa manne na kusema juhudi za Uturuki kutaka kujiunga na Umoja wa Ulaya zitaanzishwa tena kwa ushirikiano wake katika kuwazuia wakimbizi wa Syria inayowahudumia wasikimbilie Ulaya. Tusk ambaye alikuwa mwenyekiti wa mkutano huo, alisema mazungumzo hayo yaliashiria mwanzo mpya wa mahusiano na Uturuki.

EU Türkei Gipfel in Brüssel
Waziri mkuu wa Uturuki Ahmet Davutoglu (kulia) na Rais wa baraza kuu la Umoja wa Ulaya Donald TuskPicha: Reuters/T. Monasse

"Acha niseme wazi kwamba hatukubali mtu yeyote ailinde mipaka yetu. Kazi hiyo inaweza na inatakiwa kufanywa na wakazi wa Ulaya. Lakini tunatarajia hatua kubwa kuelekea kuzibadili sheria likija suala la kupunguza wimbi la wakimbizi wanaoingia Umoja wa Ulaya kupitia Uturuki."

Pande zote mbili zimeamua kutumia mkakati wa pamoja ulioafikiwa Oktoba 15 mwaka huu kusimamia vyema wimbi la wakimbizi. Chini ya mpango huo Uturuki na Umoja wa Ulaya zitashirikiana kuwalinda watu wanaokimbia vita huku zikiwazuia wahamiaji wengine au kuhakikisha wale wanaoingia Umoja wa Ulaya na Uturuki wanarejeshwa haraka nchi walikotokea.

Mazungumzo ya uanachama wa Uturuki kufufuliwa

Suala lengine muhimu katika makubaliano hayo ni mchakato wa Uturuki kutaka kujiunga na Umoja wa Ulaya kupigwa jeki, ingawa ni viongozi wachache tu katika pande zote mbili wenye matumaini kwamba Uturuki itajiunga na umoja huo hivi karibuni. Mazungumzo kuhusu ibara ya 17 ya mchakato huo inayohusu uchumi na sera ya fedha, yataanza tarehe 14 mwezi huu.

Akizungumza baada ya mkutano wa mjini Brussels, waziri mkuu wa Uturuki Ahmet Davutoglu alisema ilikuwa ni siku ya kihistoria na kuahidi kwamba nchi yake itatimiza ahadi zake, licha ya baadhi ya mataifa 28 wanachama wa umoja huo kuonyesha wasiwasi.

"Tumeupiga jeki mchakato wetu wa kutaka kujiunga na Umoja wa Ulaya. Tumekubaliana kuwa na mkakati wa pamoja dhidi ya migogoro yote katika maeneo jirani na Ulaya, na pia kufanya kazi pamoja kuutafutia ufumbuzi mzozo wa wakimbizi."

Umoja wa Ulaya umeridhishwa na jinsi Uturuki inavyoharakisha juhudi za kutimiza masharti ya Umoja wa Ulaya kuifanya rahisi kwa Waturuki kupata visa za mataifa wanachama. Katika makubaliano ya Brussels, Waturuki wengi huenda wakanufaika na safari bila visa katika eneo la Schengen barani Ulaya kufikia Oktoba 2016, ikiwa Uturuki itatimiza masharti ya kuimarisha ulinzi katika mipaka yake ya mashariki kuwafungia wahamiaji kutoka Asia na kuimarisha sheria kupunguza idadi ya wanaohamia Ulaya.

Mwandishi: Josephat Charo/AFPE/RTRE/

Mhariri: Daniel Gakuba