1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki kulipiza kisasi kikubwa kwa kuuwawa wanajeshi wake 24

19 Oktoba 2011

Uturuki leo imefanya mashambulizi ya anga na ardhini dhidi ya wanamgambo wa Kikurdi nchini Iraq na kuahidi kulipiza kisasi kikubwa baada ya wanajeshi 24 wa Uturuki kuuwawa na wanamgambo hao wa Kikurdi.

https://p.dw.com/p/RrpA
Rais Abdullah Gul wa UturukiPicha: dapd

Maafisa wa usalama wanasema takriban wanajeshi 100 kutoka chama cha PKK au chama cha Wafanyakazi wa Kurdistan walifanya mashambulizi kwa wakati mmoja katika vituo saba vya kijeshi vilioko mbali vya wilaya za Cukurca na Yuksekova kwenye jimbo la milima kusini magharibi mwa mpaka na Iraq.

Chama cha PKK ambacho kina kambi zake katika jimbo lenye utawala wa ndani la Kurdistan nchini Iraq kimedai kuhusika na shambulio hilo. Lakini mapigano ambayo Uturuki inasema imewauwa wanamgambo 15 wa Kikurdi baada ya shambulio la awali yanatishia ukosefu mkubwa wa utulivu katika kipindi ambapo kuna machafuko katika nchi jirani ya Syria na kwa vikosi vya Marekani vilioko nchini Iraq.

Duru za usalama za Uturuki zimesema makomandoo wameingia hadi kilomita nane ndani ya Iraq kuwasaka wapiganaji wa Kikurdi na kwamba ndege za kivita zimeshambulia maeneo karibu na kambi ya wapiganaji hao kwenye mto Zap katika jimbo lenye utawala wa ndani la Kurdistan nchini Iraq.

NO FLASH Türkische Armee dringt bei Einsatz gegen PKK in den Irak ein
Jeshi la Uturuki likiwa katika mojawapo ya operesheni zake za kuwasaka wapiganaji wa PKK nchini Iraq mwaka 2007Picha: picture-alliance/dpa

Rais Abdullah Gul wa Uturuki alizungumza na waandishi wa habari mjini Istanbul kuhusu kadhia hiyo amesema yule anayeamini kwamba mashambulio

hayo yataitikisa nchi yao anajidanganya na kwamba atajionea mwenyewe jinsi kisasi chao kitakavyokuwa kikubwa.

Maafisa wa usalama katika eneo hilo wameliambia shirika la habari la Uingereza Reuters kwamba vikosi vya Uturuki vimeuwa wanamgambo 15 wa Kikurdi katika mapambano. Helikopta aina ya Cobra za mashambulizi ya mizinga zimeshambulia baadhi ya maeneo na kwamba kuna wanajeshi 500 wa Uturuki ndani ya ardhi ya Iraq baadhi yao walipelekwa huko kwa ndege.

Shambulio hilo la wapiganaji wa Kikurdi na hatua iliochukuliwa na Uturuki kujibu mapigo vinaweza kuzidisha ukosefu wa utulivu kwenye eneo hilo katika kipindi ambapo vikosi vya Marekani nchini Iraq vikitarajiwa kuondoka ifikapo mwishoni mwa mwaka huu na huku machafuko ya umwagaji damu yakiongezeka nchini Syria ambako Rais Bashar al- Assad ameanzisha ukandamizaji kwa waandamanji wanaoupinga utawala wake.

Hali ya mvutano kati ya Uturuki na Iran pia imekuwa ikiongezeka kutokana na uamuzi wa Uturuki kuweka rada ya kujikinga dhidi ya mashambulizi ya makombora.

Watu wa kabila la Wakurdi wanaishi katika eneo lililosambaa kwenye mipaka ya Iran,Iraq, Syria na Uturuki.

Rais Abdullah Gul wa Uturuki pia ametowa onyo kali kwa wale wanaowapa hifadhi wanamgambo wa Kikurdi.

Uturuki ambayo mara kwa mara imekuwa ikiishutumu Iraq kwa kutochukuwa hatua za kutosha kuvunja makambi ya wapiganaji wa PKK huko nyuma imefanya mashambulizi ya anga na ardhini mara kadhaa upande wa pili wa mpaka.

Shambulio kuu la mwisho lilifanyika mwaka 2008 wakati ilipowapeleka wanajeshi 10,000 ndani ya Iraq wakisaidiwa na ndege za kivita.

Waasi wa Kikurdi wanaopigania kuwa na taifa lao huru walianza kubeba silaha dhidi ya taifa la Uturuki hapo mwaka 1984 na zaidi ya watu 40,000 waliuwawa katika mzozo huo.

Waziri Mkuu wa Uturuki Tayyip Erdogan amefuta ziara yake nchi za nje na ameitisha mkutano wa dharura na mawaziri wa mambo ya ndani na ulinzi pamoja na wakuu wa ujasusi na magenerali waandamizi.

Mwandishi: Mohamed Dahman/ RTRE

Mhariri: Yusuf Saumu