1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Utulivu wa kisiasa Guinea Bissau unahitaji marekebisho katika jeshi la taifa

26 Novemba 2008

Ndiyo njia pekee ya kuimarisha demokrasia changa ya nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/G2Y4

Jaribu la kutaka kutwaa madaraka kwa nguvu hivi karibuni katika taifa dogo la Afrika magharibi-Guinea Bissau, limezusha haja ya kufanywa mabadiliko makubwa katika jeshi la nchi hiyo, wakati nchi hiyo ikiandamwa na shutuma za maafisa wa ngazi ya juu jeshini na serikali kuhusika katika biashara ya madawa ya kulevya. Wazo la mageuzi makubwa katika jeshi linaungwa mkono na Rais Abdoulaye Wade wa nchi jirani ya Senegal akisema hilo litasaidia kuimarisha demokrasia inayolega lega nchini Guinea Bissau.

Mwishoni mwa juma lililopita wanajeshi walioasi waliishambulia Ikulu ya Rais Joao Bernado Vieira anayejulikana pia kwa jina la "Nino" na kumuuwa mlinzi mmoja na mwengine kujeruhiwa. Hawakufanikiwa kumuuwa kiongozi wa taifa.

Kitendo hicho kilitokea wiki moja baada ya uchaguzi wa bunge uliogharimiwa na wafadhili ukiwa na lengo la kuimarisha demokrasia baada ya taifa hilo kuandamwa na uazi ana mapinduzi tangu uhuru kutoka kwa Ureno 1974. Majeshi ya usalama yalikua yakimsaka afisa mmoja wa jeshi la majini mwenye cheo cha Sajenti. Wanajeshi wengine watano walikua tayari wameshatiwa nguvuni.

Muakilishi wa kanda wa ofisi ya umoja wa mataifa ya kupambana na biashara ya madawa ya kulevya Antonio Mazziteli alisema vitega uchumi na maendeleo ni mambo yaliotekwa nyara na hali mbaya ya usalama.

Tangu miaka kadhaa iliopita, Shirika la umoja wa mataifa la kupambana na biashara ya madawa ya kulevya UNODC limekaua likionya juu ya kitisho cha Guinea Bissau kugeuka kituo kikuu cha kupitishia biashara ya madawa hayo kutoka kwa wahalifu wa Colombia kama sehemu ya bidhaa zao zinazoelezwa Ulaya na Marekani kupitia Afrika.

Rais Wade wa Senegal amedokeza kwamba Guinea Bissau yenye wakaazi milioni 1.6 imeingia na ilioingia katika mgogoro wa kisiasa ukiandamana ana mapigano yaliotishia vita vya wenyewe kwa wenyewe 1998-1999, inahitaji msaada wa haraka wa jamii ya kimataifa kwa kusaka mfumo imara wa kupambana na biashara ya madawa ya kulevya.

Jenerali mmoja wa Kihisapania tayari alishaongoza ujumbe wa umoja wa ulaya ukiwa na lengo la kulisaidia kuwepo mafunzo ya nidhamu katika jeshi la Guinea Bissau. Jeshi hilo linalotokana na wapiganaji wakati wa vita vya kuwania uhuru, na katika uasi mmoja wapo kamanda wake mkuu Ansumane Mane aliuwawa 2004.

Uchunguzi mmoja uliogharimiwa na Umoja wa mataifa uligundua kuweko kwa maafisa zaidi ya 3000 katika jeshi la jumla ya askari 4.500 huku baadhi ya wanajeshi wakiwa na umri wa zaidi ya miaka 60. Wengi miongoni mwa wanajeshi wazee wakiwa na nyadhifa za juu jeshini wanapinga kustaafu katika wakati nchi hiyo inaandamwa na umasikini. Wachambuzi wanasema kasi ya wakongwe hao jeshini kustaafu inahitajika, kama sehemu ya marekebisho katika jeshi hilo, na kuleta hali ya utulivu wa kudumu katika taifa hilo, ambayo ndiyo njia pekee ya kusaidia kuimarisha demokrasia.