1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Utawala wa Burkina Faso wasitisha matangazo ya VoA

8 Oktoba 2024

Utawala wa kijeshi wa Burkina Faso umesitisha kwa muda wa miezi mitatu matangazo ya shirika la utangazaji la Sauti ya Amerika, VoA, kufuatia taarifa walioitoa kuhusu uasi wa makundi ya itikadi kali katika eneo la Sahel.

https://p.dw.com/p/4lXdh
Jenerali wa jeshi wa Burkina Faso
Kiongozi wa mapinduzi ya Burkina Faso Kepten Ibrahim Traore akishiriki katika sherehe huko Ouagadougou, Oktoba 15, 2022.Picha: Kilaye Bationo/AP/picture alliance

Baraza kuu la mawasiliano nchini humo (CSC) limeishutumu VoA kuwakatisha tamaa wanajeshi wa Burkina Faso na wale wa nchi jirani ya Mali katika majadiliano ya Septemba 19 ambayo pia yalikuwa yakipeperushwa na kituo cha redio cha kibinafsi. Serikali mjini Ouagadougou imepiga pia marufuku kwa muda kadhaa vyombo vyote vya habari vya ndani kutumia ripoti zozote za vyombo vya habari vya kimataifa. Viongozi wa kijeshi wa Burkina Faso walionyakua mamlaka katika mapinduzi ya Septemba mwaka 2022, wamekuwa wakidhihirisha kutovumilia hatua za kukosolewa huku kukiripotiwa hali mbaya ya ukosefu wa usalama katika kanda ya Sahel licha ya ahadi za kutokomeza uasi wa makundi ya itikadi kali za Kiislamu.