1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Utafiti: Vita vya Marekani Afghanistan, Iraq vyaua 225,000

1 Julai 2011

Kwa mujibu wa utafiti wa Chuo Kikuu cha Brown cha Marekani, vita vya Marekani katika mataifa ya Iraq, Pakistan na Afghanistan kufuatia mashambulizi ya Septemba 11, vimeshauwa watu 225,000 na kugharimu dola trilioni nne.

https://p.dw.com/p/11nZA
Majeshi ya Marekani nchini Iraq
Majeshi ya Marekani nchini IraqPicha: AP

"Gharama za vita hazimalizikii pale tu vita vinapomalizika", anasema Profesa wa Anthropolojia, Catherine Lutz, ambaye ni mratibu wa mradi wa utafiti katika Taasisi ya Watson ya Chuo Kikuu cha Brown.

Hadi sasa hakuna hisabu kamili ya gharama za vita ambavyo Marekani imekuwa ikipigana tangu ishambuliwe hapo Septemba 11, 2011, wala gharama ambayo jamii nzima ya Marekani imekuwa ikilipa kwa vita hivi.

Kundi hili linalokusanya wataalamu 20 wa mambo ya uchumi, wanasheria na wataalamu wa siasa kutoka chuo kikuu cha Brown cha jimbo la Rhode Island, linakisia kuwa baina ya dola trilioni 3.2 hadi trilioni 4 zimeshatumiwa na serikali ya Marekani tangu vita hivi vianze.

Hisabu hii inajumuisha pia huduma za maveterani wa kivita na za kimatibabu wanazopata wanajeshi wanaoumia kwenye vita hivyo. Vile vile inajumuisha msaada wa kijeshi ambao Marekani inautoa kwa Pakistan kila mwaka.

Majeshi ya Ujerumani nchini Afghanistan
Majeshi ya Ujerumani nchini AfghanistanPicha: dapd

"Lengo la kufanya utafiti huu lilikuwa ni kuziweka taarifa zaidi za vita hivi, hasa hapa Marekani, ambapo takwimu wanazopewa watu mara nyingi huwa si sahihi, bali huwa zi kibajeti, za kifedha tu." Anasema Profesa Lutz.

Kwa kiasi gani Marekani itabeba deni la vita hivi, ambalo hadi sasa limeshafikia dola bilioni 185 za Kimarekani, bado haijawa wazi. Hadi kufikia mwaka 2020, riba ya deni lenyewe itakuwa imeshavuka dola bilioni moja, na hili ni hata baada ya majeshi ya Marekani kuanza kujiondoa nchini Afghanistan.

Takwimu za Umoja wa Mataifa juu ya wahanga wa vita hivi zinaelezwa kuwa za juu sana. Kwa takwimu hizo, watu waliouawa hadi sasa ni 137,000 kwa Iraq na Afghanistan, huku wanajeshi 31,000 wa Kimarekani wakipoteza maisha, na vita hivi vikizalisha wakimbizi milioni 7.8 kwa ujumla wake.

Siasa za ndani nchini Marekani zinalifanya suala la gharama za vita hivi kuwa tete sana kutajwa, ndiyo maana hivi sasa Marekani inafanya hima ya kujiondoa Afghanistan. Ikulu ya Marekani inataka hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu iwe imeshapunguza wanajeshi wake kwenye ardhi ya Afghanistan kwa wastani wa thuluthi tatu. Huko Iraq, inataka ijiondoshe kabisa kufikia mwishoni mwa mwaka 2012.

Kuhusu kuzilinganisha hali za Afghanistan na Iraq, Profesa Lutz anasema kwamba vita vyote viwili vina msingi mmoja, na hivyo matokeo na gharama zake ni moja pia.

"Kwa sababu hivyo, ndivyo ambavyo vita hivi vimekuwa vikielezewa kwa umma wa Marekani. Utawala wa Bush ulikwenda vitani Iraq na mawazo kwamba kwa kufanya hivyo tutainusuru Marekani na mashambulizi ya kigaidi ya siku za baadaye. Kwa hivyo, nadhani vita hivi vinafanana sio tu kwa utawala, bali hata kwa raia." Anasema Profesa Lutz.

Mradi wa Utafiti wa Eisenhower wa Chuo Kikuu cha Brown unafadhili utafiti huu. Rais Eisenhower ndiye aliyekuwa kiongozi wa Marekani katika Vita vya Pili vya Dunia.

Katika hatuba yake ya kuaga hapo mwaka 1961, aliikosoa vikali sekta va viwanda vya silaha nchini mwake kwa ushawishi wake kwenye vita ulimwenguni.

Nukta hii pia ni sehemu muhimu ya utafiti huu wa kuangalia gharama za vita vinavyopiganwa na Marekani hivi sasa duniani.

Mwandishi: Daniel Scheschkewitz
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Othman Miraji