Uswisi yailaza Spain ,mabingwa wa ulaya bao 1:0 | Michezo | DW | 16.06.2010
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Uswisi yailaza Spain ,mabingwa wa ulaya bao 1:0

Na je, Bafana bafana watatamba usiku huu ?

default

Uswisi yaitoa Spain 1:0

Baada ya kuwaona mabingwa wakubwa uwanjani tangu kuanza kombe hili la dunia 2010 nchini Afrika Kusini: Ujerumani,Itali,Argentina,Ufaransa,Uingereza na Brazil, Spain imechezeshwa kindumbwe-ndumbwe na Uswisi huko Durban, ilipozabwa bao 1:0.Matokeo hayo ni ya kwanza ya kusisimua tangu kuanza Kombe hili la dunia Juni 11. Timu hizo mbili ziliachana sare 0:0 baada ya kipindi cha kwanza .

Mabingwa wa ulaya ambao wanapigiwa upatu ndio timu inayoweza kutoroka na Kombe, wana ila moja:

Kama Holland, Spain, hawatimizi matarajio katika Kombe la dunia; na hivyo ndivyo hali ilivyokua zaidi ya miaka 40 iliopita. Je, leo Waspain, watatoa salamu kwa Ujerumani,waliowalaza katika Finali ya Kombe la Ulaya 2008 au Waswisi wakiongozwa na kocha wa zamani wa Bayern Munich, Ottmar Hitzfeld, watazima vishindo vya mastadi wa Barcelona na Real Madrid chini ya usukani wa kocha Del Bosco.?

Kocha wa Spain Vicente Del Bosque na mastadi wake akina Iniesta,David Villa,David Silva,Sergio Ramos,alianza bila ya Farbrigas na gombe-dume hatari Torres.Ingawa Spian, inapigiwa upatu ndio itakayotawazwa mabingwa wapya wa dunia, imekumbushwa na Uswisi leo, darasa waliopewa huko huko Afrika kusini wakati wa Kombe la mashirikisho-Confederations Cup,Kombe lililofungua pazia la Kombe hili la dunia, Juni mwaka jana. Spain, ililazwa na Marekani na ikabidi kuridhia nafasi ya tatu nyuma ya Brazil na Marekani.

Wakijikuta kundi moja mara hii na Uswisi,Chile na Hondurus, waspain wamewaachia Waswisi pointi zote 3 jioni hii na baaada ya ushindi Chile wa bao 1:0. dhidi ya hondurus, Spain wana kibarua kigumu kukata tiketi ya duru ijayo.

Ikitamba langoni na kipa Iker Casillas,stadi wa kiungo Xavi na David villa,Spain imekuwa hatari sana katika lango la Waswisi wanaocheza kwa hadhari. hodi hodi zao hadika dakika ya 95 ya mchezo, hazikufua dafu kuvunja tumbuu ya lango la waswisi.

Chile, hapo kabla, imekomesha subira ya miaka 48 kunyakua ushindi katika Kombe la dunia,shukurani kwa bao la kipindi cha kwanza alilotia Jean Beausejour baada ya pasi maridadi kutoka Mauricio Isla huko Nelspruit.

Usiku wa leo, Bafana Bafana wanarudi uwanjani mjini Pretoria, kwa mpambano wao wapili tangu kufungua dimba ijumaa iliopita na Mexico. Ushindi dhidi ya mabingwa wa kwanza kabisa wa dunia-Uruguay, ni lazima ili mazumari ya Vuvuzela, yasikome kuihanikiza uwanjani .

Wakiwa hawakupewa nafasi mwezi uliopita wa kubaki hayi zaidi ya duru ya kwanza, wenyeji Bafana Bafana ,walitoka suluhu na Mexico bao 1:1 kufuatia mapambano 12 bila kushindwa.Lakini, mla, ni mla leo, mla jana kala nini: Bafana bafana siku ya ukumbusho wa machafuko ya Soweto, lazima ishinde leo usiku na kukata tiketi yake ya duru ijayo kabla haikupambana na makamo-bingwa wa dunia-Ufaransa duru ijayo.

Mwandishi: Ramadhan Ali/AFPE

Uhariri: Josephat Charo