1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Historia

Usman dan Fodio: Mwanzilishi wa Ukhalifa wa Sokoto

Yusra Buwayhid
11 Februari 2020

Alikuwa mwalimu wa dini na baadae kuwa kiongozi wa mapinduzi: Usman dan Fodio, alikosoa kundi la watu wa tabaka la juu na kubadilisha mfumo wa kisiasa katika Nigeria ya leo ya kaskazini.

https://p.dw.com/p/3WAZ6
DW African Roots | Sheikh Usman dan Fodio

Usman dan Fodio: Mwanzilishi wa Ukhalifa wa Sokoto

Je! ni lipi chimbuko la Usman dan Fodio?

Usman dan Fodio alizaliwa mnamo Desemba 15, 1754 katika kijiji cha Maratta, jimbo la Gobir lenye wazungumzaji wa lugha ya Hausa, eneo linajulikana sasa kama Nigeria Kaskazini. Alisomea sheria, theolojia na falsafa huko Agadez (ambayo sasa ni Jamhuri ya Niger) chini ya msomi wa Kiislam Jibril Ibn Umar. Kwa sababu ya elimu aliyokuwa nayo na uelewa mzuri wa dini ya Kiislam, baadae alikuja kutajwa kwa heshima kama Shekhe Usman.

Kwanini Usman akaupinga mfumo wa uongozi ulikuwapo wakati huo?

Baada ya kumaliza masomo yake, alirudi Gobir na kuanza kuhubiri dini ya Kiislam kwa watu wa eneo hilo, ambao walikuwa ni mchanganyiko wa Waislam na Wapagani. Umaarufu wake uliongezeka hadi Mfalme wa Gobir, Rimfa, akaanza kumuona Usman dan Fodio kama kitisho kwa uongozi wake na kujaribu kumuua. Usman alikimbia na kuanza kuhama hama na kuhubiri katika jamii mbalimbali za watu wa vijijini, huku akifundisha watu kusoma na kuandika.

Usman dan Fodio: Mwanzilishi wa Ukhalifa wa Sokoto

Mnamo mwaka 1803, Shekhe Usman na mamia ya wafuasi wake walihamia Gudu ambako aliendelea kueneza dini ya Kiislam. Wakati akiwa Gudu, Usman dan Fodio alitangaza vita vya kidini (vita vya jihadi) dhidi ya Mfalme Yunfa wa Gobir (mtoto wa Rimfa na mrithi wake) pamoja na watu wake, kwa sababu aliona mwenendo wao wa maisha ukienda kinyume na mafundisho ya Kiislam.

Vipi Usman dan Fodio alianzisha Ukhalifa wa Sokoto?

Tangazo la vita hivyo vya kidini lilisambaa kote katika eneo linalozungumza lugha ya Hausa, na wengi walijitolea kujiunga na jeshi lake. Mnamo mwaka 1804, alitangaza rasmi vita vya kidini dhidi ya eneo zima la Hausa. Mwaka 1808, Usman na wafuasi wake walifanikiwa kudhibiti majimbo ya Gobir, Kano na mengine yanayozungumza Hausa. Alistaafu katika harakati za vita mnamo mwaka 1811 na kurudi tena kuwa mwalimu wa kufundisha watu kusoma na kuandika. Lakini majeshi yake yaliendeleza vita hadi 1815.

DW African Roots | Sheikh Usman dan Fodio
Asili ya Afrika| Shekhe Usman dan Fodio

Mapinduzi hayo ya kidini yaliyaunganisha majimbo ya wanaozungumza lugha ya Hausa chini ya uongozi unaotumia sheria za Kiislam, na mwaka 1812, ilianzishwa himaya iliyojulikana kama Ukhalifa ya Sokoto ambayo ilikuwa na majimbo tofauti yanayolingana na yale ya awali ya watu wa Hausa. Ukhalifa wa Sokoto ulipata mafanikio makubwa ya kisiasa na kiuchumi. Ulikuwa ni mfumo wa uongozi uliokuwa na nguvu kubwa katika eneo zima la kaskazini mwa Nigeria wakati wa karne ya 19, na ulichangia sana kulifanya eneo hilo kuwa na idadi kubwa ya Waislam.

DW African Roots | Sheikh Usman dan Fodio
Asili ya Afrika | Shekhe Usman dan Fodio

Ukhalifa ulioanzishwa na Usman dan Fodio ulikuwa na umuhimu wa kiasi gani?

Ufalme wake ulioongozwa kwa sheria za Kiislam ulijumuisha sehemu nyingi zinazopatikana sasa kaskazini mwa Nigeria, na baadhi ya maeneo ya Niger pamoja na kaskazini mwa Cameroon. Vita hivyo vya kidini vilihamasisha kufanyika mfululizo wa vita vengine vya kidini kote Afrika Magharibi nyakati hizo, na dini ya Kiislam ikawa ndiyo inayoongoza miongoni mwa watu wa Afrika Magharibi.

Mwaka 1837, Ukhalifa wa Sokoto, uliokuwa na idadi ya watu wanaopindukia milioni 20, ulikuwa ufalme maarufu Afrika Magharibi.

Shekhe Usman dan Fodio alifariki dunia mnamo Aprili 20, 1817 huko Sokoto.

Ushauri wa kisayansi kuhusu makala hii umetolewa na wanahistoria Profesa Doulaye Konaté, Lily Mafela, Ph.D., na Profesa Christopher Ogbogbo. Mfululizo wa makala za Asili ya Afrika umefadhiliwa na taasisi ya Gerda Henkel.