1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Usalama kupewa kipaumbele Misri

13 Februari 2011

Kuhifadhi usalama na kurejesha maisha ya kawaida ndio vipaumbele vya muda mfupi kwa serikali ya mpito nchini Misri.

https://p.dw.com/p/10GQl
Sherehe kuu katika mji mkuu Cairo.Picha: AP

Waziri Mkuu Ahmed Shafiq alitamka hayo kwenye televisheni baada ya kukutana na mkuu wa baraza la kijeshi Mohammed Hussein Tantawi. Alisema kuwa serikali ya mpito itatoa kipaumbele kurejesha utulivu. Vile vile alitoa mwito wa kuwepo umoja kati ya umma na serikali. Serikali ya mpito imeahidi kuanzisha mageuzi ya kidemokrasia na kuheshimu makubaliano ya kimataifa, ukiwemo mkataba wa amani uliotiwa saini pamoja na Israel tangu muda mrefu.

Ägypten Proteste Demonstranten und Panzer in Kairo
Picha: AP

Kwa mujibu wa shirika la habari la serikali MENA, waziri mkuu wa zamani Ahmed Nasif na waziri wa habari wa hivi sasa Anas el Fekki wamepigwa marufuku kusafiri nje. Hata mali ya waziri wa zamani wa ndani Habib el Adli na familia yake imezuiliwa. Sababu ni tuhuma kuwa kampuni moja ya ujenzi imelipa kiasi ya Euro 500,000 katika akaunti ya Adli binafsi.

Hosni Mubarak
Picha: picture-alliance/dpa

Rais Hosni Mubarak alijiuzulu kufuatia maandamano ya siku 18 na Wamisri wamesherehekea kuondoka kwake, huku wengine hiyo jana, wakijitolea kuusafisha uwanja wa Tahrir, kitovu cha vuguvugu la upinzani dhidi ya serikali.

Mwandishi: Prema Martin/afpe,rtre,dpae
Mhariri:Maryam Abdalla