Urusi yasitisha ujumbe wake kwenye Jumuiya ya NATO | Matukio ya Kisiasa | DW | 19.10.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Urusi yasitisha ujumbe wake kwenye Jumuiya ya NATO

Urusi imeamuru kufungwa ofisi ya jumuiya ya NATO mjini Moscow katika kile kinachoelezwa kuwa ni hatua ya kulipiza kisasi baada ya NATO kuwafurusha wanadiplomasia wake.

Mapema mwezi huu, NATO iliwaondolea idhini wanadiplomasia wanane wa Urusi katika makao makuu ya jumuiya hiyo mjini Brussels, kwa kusema inaamini wanafanya kazi kwa siri kama maafisa wa kijasusi wa Urusi. Lakini pia umoja huo umepunguza idadi ya maafisa wa Urusi katika makao makuu yake kutoka watu 20 hadi 10.

Urusi imeyatupilia mbali madai hayo kwa kusema hayana msingi wowote. Na Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergey Lavrov jana Jumatatu akatangaza kusitisha shughuli za Urusi katika jumuiya ya NATO na pamoja na ofisi ya mawasiliano ya mjini Moscow.

Lavrov alidai kwamba hatua ya muungano huo imethibitisha kwamba NATO haipendi aina yoyote ya mazungumzo sawa au ushirikiano, akiongeza kuwa Urusi haioni haja yoyote ya kuendelea kudhani kuna mabadiliko yoyote ya dhati katika siku zijazo. Lavrov ameongeza kuwa mawasiliano kati ya NATO na Urusi, sasa yanaweza kufanyika kupitia ubalozi wa Urusi huko Ubelgiji.

Soma pia: Chama cha Putin chaelekea ushindi uchaguzi wa bunge

''Hakuna na uhusiano wowoote kati ya Urusi na NATO''

Urusi yasema hakuna mabadiliko mazuri katika uhusiano wake na NATO

Urusi yasema hakuna mabadiliko mazuri katika uhusiano wake na NATO

Msemaji wa Rais Putin, Dmitri Peskov, amesema leo kwamba hatua ya kusimamisha ujumbe wa Urusi kwenye Jumuiya ya NATO kunamaanisha ukosefu wa uhusiano.

''Hakukuwa na uhusiano wowote kati ya Urusi na na Jumuiya ya NATO. Hakukuwa na mazungumzo. Kinyume chake, NATO ilitangaza nia yake ya kuishikilia Urusi kwa njia yoyote ile, iliunga mkono maneno haya kwa vitendo fulani.",alisema Peskov.

Kwa upande wake, msemaji wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO, Oana Lungescu, amesema wamesikitishwa na hatua zilizofikiwa na Urusi. Akiongeza kuwa sera ya Jumuiya ya NATO kuelekea Urusi bado ni thabiti.

Lungescu amesema NATO imeimarisha uwezo wake wa kujihami ilikubaliana na vitendo vya uvamizi vya Urusi, lakini wakati huo huo nchi za Jumuiya ya NATO ziko wazi kwa mazungumzo ya pamoja kupitia Baraza la Uhusiano baina na NATO na Urusi.

Soma pia: Putin, Assad wakutana Moscow

Umuhimu wa mazungumzo baina ya pande mbili

Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Heiko Maas, amesema nchini Luxembourg kwamba uamuzi uliochukuliwa na Moscow, utazidisha hali ngumu ambayo imekuwepo na kutia doa zaidi katika mahusiano ya pande hizo. NATO ilisitisha ushirikiano wa kivitendo na Urusi mnamo mwaka 2014 baada ya serikali ya Rais Vladimir Putin kuitwaa Rasi ya Crimea kutoka mamlaka ya Ukraine.