1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yapinga ripoti ya UN

28 Oktoba 2016

Urusi imekanusha ripoti ya uchunguzi iliyotolewa na Umoja wa Mataifa ikionyesha kwamba Serikali ya Syria imefanya mashambulizi matatu yaliyohusisha silaha za kemikali, ikiita ripoti isiyo mashiko.

https://p.dw.com/p/2RpCc
USA UN Sicherheitsrat Sitzung zu Ukraine in New York Witali Tschurkin
Picha: Reuters

Uchunguzi huo ulihusisha wataalamu wa uchunguzi wa Umoja huo na Shirika la Kuzuia Matumizi ya Silaha za Kemikali Duniani. 

Balozi wa Urusi kwenye Umoja wa Mataifa, Vitaly Churkin, amesema Urusi ilipitia ripoti hiyo kwa uangalifu mkubwa, na imegundua kuwa ina mapungufu makubwa ya kitaalamu na imekosa ushahidi muhimu. Kwa mujibu wa Balozi huyo, wachunguzi hawakuwasilisha ushahidi wa vifaa na ripoti hiyo ina taarifa zenye mgongano:

Wakosoaji wa Urusi kwenye Baraza la Usalama wanasema kauli ya Balozi Churkin inaonesha wazi kwamba Urusi haipo tayari kutoa ushirikiano katika kuunga mkono mkataba unaotaka uwajibikaji kwa waliotumia silaha hizo za kemikali wanaotajwa kwenye ripoti hiyo. 

Ufaransa, Uingereza na Marekani zimeonesha nia yao ya kupitishwa kwa vikwazo dhidi ya serikali ya Syria kutokana na uhusika wake wa kutumia silaha za aina hiyo. Balozi wa Uingereza kwenye Umoja wa Mataifa, Matthew Rycroft, amenukuliwa akisema kuwa "ni lazima kuwepo kwa uwajibikaji kwa kila mmoja anayetuhumiwa katika aina yoyote ya matumizi ya silaha za kemikali nchini Syria."

Virginia Gamba aliyeongoza timu ya uchunguzi chini ya mwamvuli wa wachunguzi kutoka Umoja wa Mataifa na Shirika la Kuzuia Matumizi ya Silaha za Kemikali Duniani, ameukingia kifua utaalamu wa wachunguzi wa ripoti hiyo, akisema "watasimama imara kuitetea ripoti yao." 

Irak IS-Angriff mit Senfgas Chemiewaffen
Maeneo yaliyoathirika na silaha za kemikali yakipuliziwa dawa ya kuyasafisha ili kuepusha athari. Picha: Getty Images/AFP/M. Ibrahim

Na huko Jijini Moscow, waziri wa mambo ya nje wa Urusi, Sergey Lavrov ametaka kuongezwa kwa rasilimali za kivita katika mapambano dhidi ya makundi ya kigaidi katika ukanda wa Mashariki ya Kati, wakati ambapo amekutana na washirika wake wa Sria na iran mjini Moscow.

Amesema, anatarajia kuboresha hatua za kukabiliana na mzozo wa Syrian kwenye mazungumzo ya utatu yatakayomuhusisha Walid al-Muallem wa Syria na Mohammad Javad Zarif wa Iran, limesema shirika la habari la serikali TASS. Balozi wa Syria nchini Urusi, Riyad Haddad amesema mapema wiki hii kwamba mazungumzo hayo yatazingatia zaidi hali ilivyo katika mji wa Aleppo.

Generali wa Urusi igor Konashenkov, ambaye ni msemaji wa wizara ya ulinzi ya Urusi amesema Urusi na syria hazijafanya mashambulizi yoyote ya anga katika mji wa Aleppo kwa siku tisa sasa.

Kwingineko nchini Syria, afisa wa kundi la waasi na makundi yanayofuatilia mzozo huo wamesema hivi leo waasi wamefyatua roketi kuelekea kambi ya jeshi la anga ya Nairab mjini Aleppo, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mashambulizi mapya yanayolenga kuvunja mzingiro wa majeshi ya serikali dhidi maeneo yanayoshikiliwa na waasi.    

Shirika la Uchunguzi wa Haki za Binaadamu la Syria lenye makao yake nchini Uingereza limesema mashambulizi hayo ya roketi yameharibu kambi hiyo ya ndege za kivita na maeneo yanayozunguka kambi ya Hmeimim, iliyopo karibu na Latakia.

Mwandishi: Lilian Mtono/AP/Reuters/dpa/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef