1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yaondoa maafisa wake wa kijeshi Kherson

Iddi Ssessanga
23 Oktoba 2022

Uongozi wa jeshi la Urusi umeondoa maafisa wake katika mji ulionyakuliwa na Urusi wa Kherson katika matarajio ya kusonga mbele kwa vikosi vya Ukraine.

https://p.dw.com/p/4IZhX
Russland -Ukraine Krieg
Picha: Andrew Kravchenko/AP/picture alliance

Uhamishaji huo wa vikosi umekuja wakati jeshi la Ukraine likisema vikosi vyake vinaendeleza mashambulizi yao katika mikoa ya Kherson na Zaporizhzhia.

Siku ya Jumamosi, viongozi waliowekwa na Urusi nchini Ukraine waliwambia wakaazi wote wa Kherson kuondoka mara moja kabla ya hatua hiyo inayotarajiwa ya vikosi vya Ukraine kuuchukuwa tena mji huo.

Kirill Stremousov, naibu mkuu wa utawala wa mkoa unaoungwa mkono na Urus mkoani Kherson, alisema Jumapili kwamba zaidi ya raia 20,000 walikuwa wameondoka kuelekea ukingo wa mto Dnieper.

Alisema wakati vikosi vya Ukraine vilikuwa vinajaribu kusukuma mashambulizi yao kwenye ukingo wa kulia, safu ya ulinzi ya Urusi "imeimarishwa na hali imeendelea kuwa tulivu."

Mji wa Kherson umekuwa mikononi mwa Urusi tangu siku za mwanzo za vita vya miezi minane nchini Ukraine. Mji huo ndiyo mji mkuu wa mkoa wenye jina sawa, mmoja ya minne ambayo rais wa Urusi Vladmir Putin iliinyakuwa kinyume cha sheria mwezi uliopita na kuiweka chini ya sheria ya kijeshi ya Urusi siku ya Alhamisi.

Mnamo siku ya Ijumaa, vikosi vya Ukraine vilizishambulia ngome za Urusi kwa mabomu kote katika mkoa huo, vikilenga njia za ugavi kwa vikosi vinavyoegemea Kremlin kwenye mto na kujiandaa kwa mashambulizi ya mwisho kuurejesha mji huo.

Urusi yalenga kuvunja ari ya Ukraine kupigana

Shirika la utafiti wa kivita la ISW pia lilisema siku ya Ijumaa kwamba mkakati wa karibuni wa kivita wa Urusi, wa kulenga mitambo ya umeme katika siku za karibuni, unaonekana kulenga kupunguza nia ya Ukraine ya kupigana na kuilaazimisha serikali ya Ukraine kutumia rasilimali zaidi kulinda raia na miundombinu ya nishati.

Ukraine-Krieg | Kernkraftwerk  Saporischschja
Kinu cha nyuklia cha ZaporizhzhiaPicha: AA/picture alliance

Lilisema juhudi hiyo haina uwezekano wa kuharibu ari ya Ukraine lakini itakuwa na athari kubwa ya kiuchumi.

Mashambulizi ya Urusi dhidi ya miundombinu ya ugavi wa umeme yalilaazimu kusitisha kwa uzalishaji wa mbolea katika kiwanda kikubwa cha kemikali cha Rivneazot, kilichoko kaskazini-magharibi mwa Ukraine. Kampuni hiyo ilisema Jumapili kwamba usitishaji huo hautowi kitisho chochote cha kimazingira.

Meya wa Enerhodar, nyumbani kwa mtambo wa nyuklia wa Zaporizhzhia, aliripoti shambulio dhidi ya hoteli inayotumiwa na vikosi vya ukaliaji vya Urusi na wale wanaoshirikiana nao. Haikuwa wazi iwapo hakuna alieumizwa.

Urusi yazidi kulenga miundombinu ya nishati

Jeshi la Ukraine lilisema siku ya Jumapili kwamba vikosi vya Urusi hivi sasa vinafanya kazi ya kujilinda zaidi, lakini vinaendeleza mashambulizi dhidi ya miundombinu ya nishati ya Ukraine na dhidi ya miji kadhaa katika eneo la mashariki la Donbas.

Mikoa tisa kote nchini Ukraine, kuanzia Odesa kusini-magharibi hadi Kharkiv katika upande wa kaskazini-mashariki, ilishuhudia tena mashambulizi yanayolenga miundombinu ya nishati na mingine muhimu katika siku iliyopita, ilisema kamandi kuu ya jeshi la Ukraine. Imeripoti jumla ya mashambulizi 25 ya angani ya Urusi na zaidi ya makombora 100 na maroketi kote nchini Ukraine.

Wakati huo huo vikosi vya mashambulizi ya kujibu vya Ukraine katika mikoa ya Kherson na Zaporizhzhia, vililenga maeneo yanayoshikiliwa na Urusi, hasa mji wa Vova Kakhovka, na kufanya mashambulizi 17 ya angani katika kampeni jumla, kwa mujibu wa kamandi kuu ya jeshi la Ukraine.

Katika posti ya Telegram siku ya Jumapili, jeshi la Ukraine lilidai kuharibu droni 14 za Urusi zilizotengenezwa na Iran katika muda wa siku moja iliyopita.

Mashambulizi ya makombora ya Urusi aina ya S-300 usiku yalilenga kiunga cha makaazi katika mji wa Mykolaiv, na kujeruhi watu watatu, kwa mujibu wa jeshi la Ukraine, kamandi ya kusini.

Majengo mawili ya makaazi, uwanja wa michezo na ghala viliharibiwa, ilisema katika post ya Facebook.

Picha zilizochapishwa na vyombo vya habari vya ndani na maafisa zilionesha jengo la makaazi likiwa na upande mmoja ulioporomoka, na lundo la vifusi katikati mwa madimbwi kwenye eneo mkabala.

Mikoa ya Urusi inayopakana na Ukraine yajenga safu za ulinzi

Ukraine Russische Raketenangriffe in Saporischschja
Mashambulizi ya Urusi dhidi ya majengo, ZaporizhzhiaPicha: Sergiy Chalyi/REUTERS

Magavana wa mikoa mwili ya Urusi inayopakana na kaskazini-mashariki mwa Ukraine, walisema safu za ulinzi zinajengwa, yumkini katika matarajio ya mashambulizi ya kuvuka mipaka wakati vikosi vya Ukraine vikisonga mbele.

Gavana wa Kursk Roman Starovoit, alisema Jumapili kwamba safu mbili za ulinzi katika mkoa huo tayari zimejengwa na ya tatu itakamilishwa kufikia Novemba 5.

Naye gavana wa Belgorod Vyacheslav Gladkov, alisema safu za ulinzi zilikuwa zimejengwa pia katika mkoa wake.

Siku ya Jumamosi, alichapisha picha za tofali za zege zenye muundo wa piramidi zilizowekwa ili kuzuwia usafiri wa magari ya kivita.

Rais wa kiwanda cha injini za ndege Ukraine akamatwa kwa kushirikiana na adui

Kwingineko, idara ya usalama ya Ukraine ilisema siku ya Jumapili kwamba imemkamata mkuu wa muda mrefu wa kiwanda cha injini za ndege, ikimtuhumu kushirikiana na Urusi kwa kutoa vifa vya kijeshi kwa matumizi katika ndege za mashambulizi za Urusi.

Viacheslav Bohuslaiev, rais wa kiwanda cha Motor Sich mkoani Zaporizhzhia na afisa mwingine wa juu wa kiwanda hicho, walishtakiwa kwa kushirikiana na "kulisadia taifa la uvamizi."

Idara ya usalama ya Ukraine SBU, ilisema katika taarifa kwamba wawili hao wanashtumiwa kwa kula njama na mtengenezaji wa silaha wa Urusi, alie karibu na Kremlin, kutoa injini zilizotengenezwa Ukraine na vipuli kwa vikosi vya Urusi.

SBU ilielezea mfumo mgumu wa kutumia watu wa kati katika mataifa matatu ili kuepuka vikwazo dhidi ya Urusi.

Motor Sich ni mmoja ya viwanda vikubwa zaidi nchini Ukraine, na imekuwa mtengenezaji muhimu wa injini tangu enzi za kisovieti.

Majengo yake yamekuwa yakilengwa mara kwa mara na mashambulizi ya Urusi wakati wa vita.