1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Urusi yailenga miundombinu ya bandari nchini Ukraine

26 Septemba 2023

Urusi imehujumu miundombinu ya bandari na hifadhi za nafaka nchini Ukraine katika mfululizo wa mashambulizi usiku wa kuammkia leo yaliyoilenga wilaya ya Izmail yenye shughuli nyingi za usafirishaji mazao ya Ukraine.

https://p.dw.com/p/4WorK
Vita vya Ukraine mkoani Odessa
Hujuma za Urusi zimeharibu mali huko Odessa, UkrainePicha: Odesa Regional Prosecutor's Office/REUTERS

Kwa mujibu wa maafisa wa Ukraine, ndege za kijeshi na makombora ya Urusi yamefanya uharibifu mkubwa kwa miundombinu ya bandari na maeneo ya kuhifadhi nafaka hususani kwenye mkoa wa kusini mwa Odesa.

Gavana wa mkoa huo, Oleh Kiper, amesema miongoni mwa bandari zilizolengwa ni zile za Izmail na Reni zinazopatikana kwenye kingo za mto Danube.

Amesema kwa jumla, kituo cha upekuzi wa bandarini, maghala kadhaa ya kuhifadhi mazao na zaidi ya malori na magari madogo 30 vimeharibiwa.

Watu wawili pia wamejeruhiwa kwenye kampeni hiyo ya kijeshi ya Urusi iliyodumu kwa muda wa saa mbili usiku wa kuamkia leo.

Jeshi la Ukraine limearifu kuwa mashambulizi hayo yamelazimisha kufungwa kwa muda kwa kituo cha upekuzi wa mpakani kilichotambulishwa baadaye na walinzi wa mipaka wa nchi hiyo kuwa ni kile cha Orlivka kinachoitenganisha Ukraine na Romania.

Miji na majimbo mingine ya Ukraine yashambuliwa 

Hujuma hizo za Urusi ni za hivi karibuni kabisa dhidi ya miundombinu ya bandari ya Ukraine na maeneo ya kuhifadhi nafaka tangu mwezi Julai, pale Moscow ilipojitoa kutoka mkataba wa kimataifa wa kusafirisha nafaka za Ukraine kupitia bandari za Bahari Nyeusi.

Odessa, Ukraine
Lori la mizigo likiteketea kwa moto baada ya shambulio la Urusi mkoani Odessa nchini UkrainePicha: Odesa Regional Prosecutor's Office/REUTERS

Tangu wakati huo, Ukraine iliyo mzalishaji na msafirishaji mkubwa wa nafaka na mazao mengine ya chakula, iliongeza kasi ya kutumia bandari za mto Danube kupeleka mazao hayo kwenye soko la kimataifa.

Mbali ya mkoa wa Odesa, majimbo mengine ya Ukraine ya Mykolaiv, Kherson na Kirovohrad yamelengwa na hujuma za kijeshi za Moscow. Hapajatolewa ripoti zozote za vifo kwenye mashambulizi hayo.

Jeshi la Ukraine limesema kwa jumla Urusi ilirusha ndege 38 zisizo na rubani usiku wa kuamkia leo na kati ya hizo 26 zilidunguliwa na mifumo ya ulinzi wa anga ya Ukraine.

Duru za kijeshi ndani ya Ukraine zimefahamisha ndege zote hizo zilirushwa kutokea rasi ya Crimea, eneo ambalo Urusi ililitwaa kwa mabavu kutoka Ukraine mnamo mwaka 2014.

Ukraine yafanya hujuma ndani ya ardhi ya Urusi, Pistorius aendelea na ziara ya Baltiki

Katika kile kilichotafsiriwa kuwa na hatua ya kujibu mapigo, vikosi vya Ukraine navyo vimefanya mashambulizi kadhaa ndani ya ardhi ya Urusi na eneo la rasi ya Crimea.

Gavana wa jimbo la Kursk la nchini Urusi amesema nyumba kadhaa zilipoteza huduma ya nishati ya umeme baada ya kutokea shambulizi.

Wizara ya Ulinzi ya Urusi imesema ndege moja isiyo na rubani inayoaminika kuwa ya Ukraine ilidunguliwa kwenye anga ya jimbo la Kursk mnamo majira ya alfajiri.

Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius
Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius akiwasilia Riga, Latvia Picha: Kay Nietfeld/dpa/picture-alliance

Katika hatua nyingine, Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius amezihakikishia nchi za kanda ya Baltiki kwamba ziko salama dhidi ya kitisho cha ulinzi kinachoongezeka tangu Urusi ilipoivamia Ukraine kijeshi.

Pistorious anayeyatambelea mataifa yote matatu ya kanda hiyo ambayo ni Latvia, Estonia na Lithuania ametoa ahadi kuwa Ujerumani itaendelea kuwa bega kwa bega na kuonesha mshikamano kwenye kuikabili Urusi.

Mapema hii leo Pistorius aliitembelea kambi ya kijeshi ya Amari nchini Estonia baada ya hapo jana kufanya mazungumzo na maafisa wa serikali ya Latvia kwenye  mji mkuu, Riga.