1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yawasilisha pendekezo kuhusu amani ya Syria

11 Novemba 2015

Urusi imeandaa mpango wa amani kuhusu Syria, ambamo inapendekeza serikali ya nchi hiyo na wapinzani wakubaliane kuanzisha mchakato wa mabadiliko ya katiba ambao utamaliza miezi 18, na kufuatiwa na uchaguzi wa Rais.

https://p.dw.com/p/1H3m2
Mazungumzo ya kimataifa kuhusu Syria mjini Vienna mwishoni mwa Oktoba, 2015
Mazungumzo ya kimataifa kuhusu Syria mjini Vienna mwishoni mwa Oktoba, 2015Picha: picture-alliance/AA/C. Oguz Gumrukcu

Rasimu ya mpango huo utakaosambazwa na Urusi katika Umoja wa Mataifa, na ambayo nakala yake imeonwa na Shirika la Habari la Reuters imeletwa siku chache kabla ya mazungumzo ya pande mbali mbali kuhusu Syria, ambayo yatafanyika mjini Vienna mwishoni mwa wiki hii. Mpango huo wenye vipengele vinane hauondoi uwezekani wa kuhusika kwa rais Bashar al-Assad katika mchakato huo, hali ambayo wapinzani wa kiongozi huyo wanasema haiwezekani katika kuitafutia amani Syria.

Kulingana na rasimu hiyo, rais atakayechaguliwa kwa kura za umma atakuwa amiri mkuu wa majeshi, na atakuwa na udhibiti katika masuala kijasusi na kuhusu sera ya nje ya nchi.

Mapendekezo ya Urusi katika mpango huo yanazitaka pande zote katika mzozo wa Syria kuafiki mapendekezo hayo katika mkutano utakaofanyika siku zijazo chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa. Aidha, inabainisha kwamba mchakato wa mabadiliko hautaongozwa na rais Bashar al-Assad, bali mtu atakayekubaliwa na pande zote.

Mwanadiplomasia mmoja wa nchi ya magharibi ameiambia Reuters kwamba anaamini watu wengi hawatavutiwa na rasimu hiyo ya Urusi, na kuongeza kuwa wale watakaoipinga watahakikisha mpango huo hauchukuliwi kama msingi wa mazungumzo.

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa atoa wito

Wakati huo huo mjumbe wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria Staffan de Mistura amezitaka nchi zenye nguvu dunia, kujengea kwenye msukumo wa mazungumzo ya kimataifa yanayoendelea, kupata jibu la kisiasa kwa mzozo wa Syria ambao umedumu kwa miaka minne sasa.

Staffan de Mistura, mjumbe wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria
Staffan de Mistura, mjumbe wa Umoja wa Mataifa kuhusu SyriaPicha: Reuters

''Ujumbe wangu nimeutoa kwa neno moja, msukumo. Msukumo wa mazungumzo ya Vienna haupaswi kupotea. Fikiria miezi michache iliyopita, hatukufikiria ingewezekana kuzileta pamoja Marekani, Urusi, Saudi Arabia Iran na nchi nyingine. Msukumo huo tunapaswa kuunga mkono.''

Wito wake huo umeungwa mkono na balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Samantha Power, ambaye kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Twitter, amesema mazungumzo ya Vienna yanapaswa kufikia usitishaji mapigano, na kuanzisha njia kuelekea suluhisho la kisiasa kwa Syria.

Hata hivyo, pande zote katika mzozo huo zinasema hatima ya rais Bashar al-Assad ndio kikwanzo kikubwa katika mchakato mzima.

Jeshi la serikali laikomboa kambi ya kimkakati

Haya yanajiri wakati nchini Syria kwenyewe jeshi la serikali limeuvunja mzingiro kwenye kambi ya jeshi lake la anga, ambao umewekwa na kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS.

Kundi la wanajeshi limejipenyeza katika ngome ya IS na kuingia katika kambi hiyo ya Kweyris, na kushangiria ushindi huo kwa kufyatua risasi hewani. Wachambuzi wanaamini kambi hiyo ambayo inao uwanja wa ndege, itatumiwa na Urusi katika operesheni zake za kumuunga mkono rais Assad.

Mwandishi: Daniel Gakuba/rtre/afpe

Mhariri:Josephat Charo