1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi na Uturuki kuendelea kujadili Syria

Lilian Mtono
17 Septemba 2018

Rais wa Urusi Vladimir Putin anatarajiwa kumkaribisha mwenzake wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, hii leo mjini Sochi katika mkutano wa kujadiliana juhudi za amani katika jimbo la Idlib nchini Syria.

https://p.dw.com/p/34z4c
Iran Teheran Syrien Gipfel - Putin trifft Erdogan
Picha: Getty Images/AFP/K. Kudryavtsev

Rais wa Urusi Vladimir Putin anatarajiwa kumkaribisha mwenzake wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, hii leo mjini Sochi katika mkutano wa kujadiliana juhudi za amani katika jimbo la Idlib nchini Syria, ambalo hivi karibuni litalengwa na mashambulizi makubwa kutoka kwa vikosi vya serikali vinavyotaka kulirejesha eneo hilo ambalo ni ngome ya mwisho ya waasi. 

Mkutano huo unaofanyika mjini Sochi unakuja katika wakati ambapo vikosi vya Syria vinavyoungwa mkono na Urusi na Iran vikijiandaa kufanya mashambulizi dhidi ya ngome hiyo ya mwisho ya waasi ya Idlib, ingawa Uturuki na Marekani mara kadhaa zimeonya dhidi ya operesheni ya aina yoyote kwenye eneo hilo. 

Mkutano huu unatarajiwa kuwa mwendelezo wa mazungumzo yaliyoanzia kwenye mkutano wa kilele uliowakutanisha marais watatu ulioandaliwa na Iran wiki iliyopita, ambapo pamoja na mambo mengine Rais Putin na mwenzake wa Iran, Hassan Rouhani, walipuuzilia mbali pendekezo la Rais Erdogan lililohusu usitishwaji kamili wa mapigano nchini Syria.

Iran Teheran Putin, Rohani und Erdogan Beratungen zu Syrien
Rais Putin wa Urusi na Rouhani wa Syria walipuuza hoja ya Uturuki ya kusitisha mapigano Syria.Picha: Getty Images/AFP/M. Klimentyev

Mchambuzi aliyeko nchini Syria Mazen Bilal amesema tofauti na majadiliano mapana kuhusu mzozo wa Syria kwenye mkutano huo wa kilele wa Tehran, mkutano huu wa Sochi huenda ukaanzia zaidi suala la Idlib, na hususan kuhusu namna ya kulishambulia kundi la kigaidi Jabhat Fateh al-Sham, lakini pia matatizo mapya, yanayosababishwa na Uturuki ambayo mara kadhaa hupeleka wanajeshi nchini Syria.

Ameongeza kuwa, pamoja na majadiliano hayo yanayoweza kufikiwa, lakini kuna dalili kwamba huenda mkutano huo pia ukakabiliwa na ushawishi wa mataifa ya magharibi, hivyo kutokuwa na mafanikio.

Urusi na Uturuki hazikufikia maafikiano na pia zilishindwa kupitisha mapendekezo ya operesheni za kijeshi, na hususan kuhusu shughuli za jeshi la Uturuki pamoja na makundi inayoyaunga mkono.

Syrien Ärzte ohne Grenzen Bombardierung Krankenhaus
Baadhi ya hospitali za Idlib zimeshambuliwa vibaya na kushindwa kabisa kuendelea kutoa hudumaPicha: picture-alliance/dpa/S.Taylor

Wakati viongozi hao wakijiandaa na mkutano huo, huko nchini Syria, zaidi ya madaktari na wauguzi 300 wameandamana hapo jana katika eneo hilo la Idlib wakiitaka Jumuiya ya Kimataifa kuwalinda dhidi ya mashambulizi yanayotarajiwa kufanywa na vikosi vya rais Bashar Al-Assad.

Kulingana na mwandishi wa shirika la habari la AFP, waandamanaji hao walikusanyika mbele ya hospitali ya Atme, karibu na mpaka na Uturuki, wakiwa na mabango yaliyokuwa na ujumbe wa kwa Umoja wa Mataifa unaosema ni jukumu lake kuwalinda, huku ujumbe mwingine ukimlenga moja kwa moja mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Syria, Staffan De Mistura, ukisema "ulinzi kwa watumishi wa afya ni sehemu ya majukumu ya ujumbe wako".

Mmoja wa wauguzi Fadi al-Amur alinukuliwa akisema wanataka kuhitimishwa kwa mashambulizi dhidi ya hospitali, na kuongeza kuwa wauguzi hawaegemei upande wowote, na jukumu lao ni kuwatibu waathirika kwa mashambulizi yanayofanywa na Urusi na Syria.

Mashambulizi yaliyofanywa hivi karibuni na utawala wa Syria na Urusi, mara kadhaa yalishambulia hospitali na vituo vya uokozi katika eneo hilo la Idlib. Umoja wa Mataifa ulisema shambulizi lililofanywa Septemba 6, liliharibu hospitali ya Kafr Zita na kushindwa kuendelea kutoa huduma.

Jimbo la Idlib lililoko karibu na mpaka na Uturuki, kaskazini magharibi mwa Syria, ndilo ngome pekee ya waasi iliyosalia baada ya miaka saba ya vita kali nchini humo.

Mwandishi: Lilian Mtono/DPAE/AFPE

Mhariri: Mohammed Khelef