Urusi na Marekani zakubaliana kupunguza silaha za nyuklia duniani | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 06.07.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Urusi na Marekani zakubaliana kupunguza silaha za nyuklia duniani

Marekani kutumia anga ya Urusi kupeleka mahitaji kwa wanajeshi wake Afghanistan

default

Rais wa Marekani Barack Obama (kushoto) mke wake Michelle na wasichana wao Sasha (katikati) na Melia

Rais wa Marekani Barack Obama ameanza ziara yake ya siku mbili nchini Urusi hii leo yenye lengo la kuboresha uhusiano kati ya nchi hizo mbili ambao umekuwa ukilegalega. Marekani na Urusi zimesaini makubaliano yatakayosaidia kuundwa mkataba mpya wa kupunguza silaha za nyuklia.

Rais Obama na mwenzake wa Urusi Dmitry Medvedev wametia saini makubaliano ya pamoja kuahidi kufikia mkataba mpya wa kupunguza silaha za nyuklia duniani kuchukua nafasi ya mkataba uliopo hivi sasa unaojulikana kama START ambao ulianza kutekelezwa mnamo mwaka 1991. Waziri wa mashauri ya kigeni wa Urusi, Sergei Lavrov, amenukuliwa na vyombo vya habari vya Urusi akisema makubaliano hayo ya pamoja hata hivyo hayatakuwa na vipengee vya mkataba mpya utakaoundwa.

Rais Obama na mwenzake wa Urusi, Dmitry Medvedev wamefanya mazungumzo mjini Moscow kuanza ukurasa mpya wa uhusino kati ya nchi zao ulioharibiwa na mivutano mbalimbali kati ya mahasimu hao wa wakati wa vita baridi. "Tuna matumaini mazungumzo yetu yatafunga kurasa kadhaa ngumu katika historia baina ya Marekani na Urusi na kufungua ukurasa mpya," amesema rais Medvedev wakati alipoanza mazungumzo na rais Obama.

Akiueleza uhusiano kati ya Urusi na Marekani rais Obama amesema, "Mtazamo wa uhusiano kati ya Marekani na Urusi wa wakati wa vita baridi umepitwa na wakati. Huu ni wakati wa kusonga mbele kuelekea mkondo mwingine. Nadhani rais Medvedev analielewa hilo. Nadhani Putin ana mguu mmoja uliosimama katika njia ya kufanya mambo kama zamani na mguu mwingine uliosimama katika njia mpya."

Rais Obama amesema, "Iwapo tutafanya kazi kwa bidii katika siku hizi mbili basi tutafaulu kupiga hatua kubwa mbele zitakazowanufaisha raia wa nchi zetu. Tuna hakika katika maswala yote yatakayojadiliwa Marekani na Urusi zinafanana zaidi kuliko kutofautiana."

Russland Dmitri Medwedew Anerkennung von Abchasien und Südossetien Fernsehansprache

Rais wa Urusi Dmitry Medvedev

Marekani na Urusi zimefikia makubaliano yatakayoruhusu safari 4,500 za ndege za Marekani kila mwaka kupitia anga ya Urusi bila malipo yoyote ili kuwapelekea mahitaji wanajeshi wa Marekani walio nchini Afghanistan. Kufikia leo usafiri wa reli wa bidhaa zisizo hatari ndio uliokuwa ukiruhusiwa. Marekani imesema hatua hiyo ya Urusi inadhihirisha serikali ya Moscow inashirikiana kuiimarisha Afghanistan.

Mada nyengine zitakazojadiliwa ni vita vinavyoendelea huko Afghanistan na mahusiano na Iran na Korea Kaskazini kuhusiana na mipango yao ya silaha za nyuklia.

Urusi na Marekani pia zimekubaliana kufufua tume ya pamoja inayochunguza hatima ya wafungwa wa vita na wanajeshi waliopotea vitani. Tume hiyo inachunguza taarifa ya wanajeshi wa Marekani waliozuiliwa katika mfumo wa zamani wa jela ya Gulag ya muungano wa zamani wa Soviet.

Taarifa iliyotolewa leo na ikulu ya Marekani mjini Washington kabla rais Obama kuwasili mjini Moscow inasema tume hiyo inaanzisha tena kazi muhimu inayodhihirisha kujitolea kwa dhati kwa nchi hizo mbili kwa wanajeshi wao. Hata hivyo haikubainika wazi kwa nini tume hiyo iliyoundwa mnamo mwaka 1992 ilihitaji kuanzishwa tena kikamilifu.

Rais Barack Obama akiandamana na mkewe Michelle na wasichana wake wawili, Sasha na Melia, waliwasili katika uwanja wa ndege wa Vnukovo mjini Moscow wakiwa katika ndege ya Air Force One wakati kukiwa na baridi na mawingu yakitanda angani, hali ya hewa ambayo inasemekena si ya kawaida msimu kama huu.

Kuwasili kwa rais Obama hakukuonyeshwa moja kwa moja kwenye televisheni ya Urusi na kwa ujumla kulikuwa na dalili ndogo mno mjini Moscow ya hamasa ya Obama miongoni mwa wakaazi wa mji huo, ikilinganishwa ziara za kiongozi huyo katika nchi nyingine za kigeni.

Msafara wa rais Obama umeelekea kwenye kaburi la mwanajeshi asiyejulikana ambako ameweka shada la maua. Katika vitongoji vya mji wa Moscow makundi madogo ya Warusi walitabasamu na kumpungia mikono rais Obama huku wengine wakimtazama bila kuonyesha hisia zozote.

Ziara ya rais Obama nchini Urusi haitarajiwi kutokuwa na matatizo kwa kuwa atakutana na viongozi mashuhuri wa upinzani nchini humo na kutoa hotuba muhimu katika chuo kikuu cha uchumi mjini Moscow.

Hapo kesho rais Obama anatarajiwa kukutana na waziri mkuu wa Urusi Vladimir Putin na wajumbe wa makundi ya kutetea wa haki za binadamu.

 • Tarehe 06.07.2009
 • Mwandishi Charo Josephat
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/IiJZ
 • Tarehe 06.07.2009
 • Mwandishi Charo Josephat
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/IiJZ
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com