1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi na Marekani zabadilishana majasusi

Abdu Said Mtullya9 Julai 2010

Ngede inayowarudisha majasusi wa Urusi imeshatua Vienna ikielekea Mosko.

https://p.dw.com/p/OEwc
Marais Barack Obama wa Marekani na Dmitry Medvedev wa Urusi. Nchi zao zimebadilishana majasusi.Picha: AP

Katika sakata la ujasusi baina ya Urusi na Marekani nchi hizo zimeanza kubadilishana wapelelezi waliokuwa wanashikiliwa katika kila upande.Watu 10 waliokiri kuwa majasusi wa Urusi wamefukuzwa Marekani.

Wizara ya sheria ya Marekani imethibitisha kwamba watu hao wameshaondoka Marekani.Ndege ya watu hao,wanaume watano na wanawake watano, iliondoka New York baada ya hakimu kuamua watu hao waondoke Marekani.Watu hao walikiri kuwa walikuwa wanafanya shughuli za upelelezi kwa niaba ya nchi ya kigeni. Watu hao walifukuzwa muda mfupi baada ya kufikishwa mahakamani na kutiwa katika ndege iliyokodishwa na serikali ya Marekani kupelekwa Mosko kwa kupitia Vienna.

Na mjini Mosko, rais Dmitry Medvedev wa Urusi amewasamehe watu wanne waliokuwa wanafanya shughuli za upelelezi kwa ajili ya nchi za magharibi.Habari zinasema watu hao walikuwa wanapeleka siri za hali ya juu kwa nchi za magharibi.Walikiri kuendesha shughuli za kijasusi katika barua walizoziandika kwa rais Medvedev kuomba msamaha.

Muhimu kati ya majasusi hao wanne ni Igor Sutyagin, mtafiti wa mambo ya nyuklia, ambae mnamo mwaka wa 2004 alihukumiwa kifungo cha miaka 15 jela, kwa kosa la usaliti . Wakili wake, Anna Stavizkaya, amesema kuwa mteja wake Sutyagin anakabiliwa na matatizo ya kinafsi. Ingawa Marekani haikutaja jina la jasusi huyo, maafisa wa nchi hiyo wamesema wanatambua kwamba wote waliowekwa ndani nchini Urusi wamo katika hali mbaya ya afya.

Wengine waliosamehewa na rais Medvedev wa Urusi ni majasusi wa pande mbili, Alexander Zaporozhsky, na Sergei Skripal, waliokuwa wanatumikia kifungo cha miaka 13 jela nchini Urusi.Mwengine ni Gennadi Vasilenko.

Maafisa wa Urusi na Marekani wamesema mapatano ya kubadilishana majasusi yametokana hasa na uhusiano mzuri uliopo sasa baina ya Urusi na Marekani

Zoezi hilo la kubadilishana majasusi baina ya Urusi na Marekani ndilo kubwa kuwahi kufanyika tokea kumalizika enzi za vita baridi mnamo mwisho wa miaka ya 1980 baina ya kambi za mashariki na magharibi.

Mwandishi Mtullya, Abdu

Mhariri: Miraji Othman