1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Urusi na China zatangaza kuimarisha zaidi uhusiano wao

Zainab Aziz
30 Desemba 2022

Marais wa Urusi Vladimir Putin na Xi Jinping wa China wamefanya mazungumzo ambapo wameahidi kuimarisha uhusiano wa nchi zao mbili. Mazungumzo hayo yamefanyika wakati ambapo Urusi ikiendelea kuishambulia Ukraine.

https://p.dw.com/p/4LaBo
Videokonferenz | Wladimir Putin und Xi Jinping
Picha: Sputnik/Mikhail Kuravlev/Kremlin/REUTERS

Viongozi hao wameahidi kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizo mbili pamoja na kudumisha uhusiano wao wa kijeshi huku uvamizi wa Urusi nchini Ukraine ukiwa umeingia katika mwezi wa kumi sasa. Usiku wa kuamkia Ijumaa Ukraine ilikabiliwa na mashambulizi ya ndege zisizo na rubani na ya makombora.

Putin na Xi kwenye mazungumzo yao yaliyofanyika kwa njia ya video walijikita katika kupongeza kuimarika kwa uhusiano wa nchi zao katika kile walichokitaja kuwa kinatokana na siasa za kikanda na hali ngumu inayoikumba dunia.

Rais wa China Xi Jinping
Rais wa China Xi Jinping Picha: CCTV/AP/picture alliance

Viongozi hao wamesisitiza kwamba China na Urusi daima zibaki kwenye msimamo wao wa kushirikiana na kwamba nchi hizo zinahitaji kuongeza ushirikiano huo na kudumisha maamuzi ya kimkakati kwa pamoja.

Rais wa China akizungumzia juu ya mgogoro wa Ukraine amesema mazungumzo ya amani hayatakuwa rahisi kati ya Urusi na Ukraine lakini daima yatakuwepo matarajio ya kupatikana amani kati ya pande hizo mbili. Vilevile Xi amesema China na Urusi zitaendeleza ushirikiano wa kimataifa katika biashara, nishati, fedha na katika sekta ya kilimo. Juu ya kuongezeka mivutano ya kikanda rais wa Urusi Vladimir Putin amesema:

"Katika muktadha wa kuongezeka kwa mivutano ya  kikanda, umuhimu wa ushirika wa mikakati baina ya  Urusi na China nao pia unaongezeka kuwa msingi wa  uimara. Uhusiano wetu unahimili kwa taadhima mitihani yote. Unaonesha ukomavu na uthabiti na unaendelea kupanuka. Na kama tulivyobainisha hapo awali mahusiano haya ni madhubuti kuliko yote katika historia. Yanaonesha muundo wa ushirikiano kati ya mataifa muhimu duniani mnamo karne hii ya 21."  Mwisho wa kumnukuu.

Rais wa Urusi Vladimir Putin
Rais wa Urusi Vladimir Putin Picha: Mikhail Klimentyev/Sputnik/Kremlin/AP Photo/picture alliance

Putin pia amemwalika rais wa China Xi Jinping kuitembelea Moscow katika msimu wa mapukutiko. China, ambayo imeapa kwamba urafiki wake na Urusi hauna kikomo, imekataa kabisa kukosoa uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, na badala yake imeilaumu Marekani na jumuiya ya kujihami ya NATO kwa kuichokoza Urusi na pia imelaani vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Urusi.

Vyanzo:AFP/RTRE/AP