Uruguay na Uholanzi kupambana katika nusu fainali ya kwanza kombe la dunia | Michezo | DW | 06.07.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Michezo

Uruguay na Uholanzi kupambana katika nusu fainali ya kwanza kombe la dunia

Saa na dakika zinaendelea kuyoyoma kuelekea nusu fainali ya kwanza ya kombe la dunia mwaka huu 2010 baina ya Uruguay na Uholanzi.

default

Mchezaji wa Uruguay Luis Suarez, kushoto ambaye ana kadi nyekundi na hawezi kucheza leo baada ya kuukamata mpira ambao ulikuwa unaelekea wavuni katika pambano lao dhidi ya Ghana.

Saa  na  dakika  zinaendelea  kuyoyoma  kuelekea  nusu fainali  ya  kwanza  ya  kombe  la  dunia   mwaka  huu 2010 nchini  Afrika  kusini. Uruguay  na  Uholanzi  zinakaribia kuingia  dimbani  kuamua  nani  ataingia  katika  fainali  ya mwaka  huu  ya  kombe  la  dunia.

Uruguay   haipewi  nafasi  kubwa  mbele  ya  Uholanzi  leo kuingia  katika  fainali  baada  ya  kuiondoa  Ghana  katika mchezo  wa  robo  fainali  uliozusha  maswali  kadha,  lakini Ghana  ilipokelewa  kama  mashujaa   waliporejea nyumbani, na  kila  mpenda  soka  katika  bara  la  Afrika aliridhika  kuona  kuwa  Ghana  haikutolewa  kama  timu nyingine  za  bara  hilo.

Uruguay, ambayo  imo  katika  nusu  fainali  yake  ya kwanza  katika  muda  wa  miaka  40  iliyopita,  inaangalia miaka  yake   ya  nyuma  ambapo  ilipata  mafanikio  wakati waliponyakua  kombe  hilo  katika  mwaka  1930  na  1950.

Wadachi, Uholanzi, timu  timu  bora  ambayo  haijawahi kushinda  kombe  la  dunia  licha  ya  aina  ya  mchezo wao  wa  wazi  ambao  ni  maarufu  duniani  kote  ,  hii  leo ndio  wanaopewa  nafasi  ya  juu  kuweza  kuibuka  na ushindi, wakiongozwa  na  wachezaji   hatari  wa  kiungo Arjen  Robben, Wesley Sneijder  na  Dirk Kuyt.

Uruguay  huenda  ikawakosa  wachezaji  wake  watatu muhimu, na  mzigo  mkubwa  utamuangukia  mshambuliaji nyota  Diego  Forlan, ambaye  alipachika  bao  la kusawazisha  dhidi  ya  Ghana  katika  robo  fainali.

Kocha  wa  Uholanzi Bert van Marwijk amesisitiza  kuwa timu  yake  haitaonyesha  ishara  zozote  za  dharau  kama ilivyofanya  siku  za  nyuma.

Huu  ni  wakati  ambao  nimeuzungumzia  miaka  miwili iliyopita, kwamba  iwapo tunashinda  dhidi  ya  timu  kama Brazil  na  tuko  juu  ya  dunia, na  kisha  unakuwa  na mchezo  mwingine, na  mchezo  huo  ni  dhidi  ya Uruguay, hawa  ni  wapiganaji, si  rahisi  kusalim  amri ,  na kwa  hiyo  inatubidi  kuwa   makini  sana.

Wakati  vikosi  hivyo  viwili  vinaota  ndoto  ya  mafanikio, Black Star  wa  Ghana  walikuwa  wakielea  katika  wimbi  la mapenzi  makubwa  ya  taifa  lao  ambapo  walilakiwa kama  mashujaa  licha   ya  kutolewa  katika  kinyang'anyiro hicho  kwa  hali  ya  kusikitisha   dhidi  ya  Uruguay.

Maelfu  ya  watu  walifika  katika  uwanja  wa  ndege kuwalaki, Black  Stars  jana  Jumatatu  wakiimiminia  maji ndege  iliyowachukua  na  kuwapokea  kwa  heshima  ya zulia  jekundu. Kundi  kubwa  la  watu  lilifurika  katika uwanja  huo  wa  ndege  mjini  Accra  wakipuliza matarumbeta  ya  vuvuzela, wakiimba  na  kupiga  ngoma.

Ghana  ilikuwa  timu  pekee  kutoka  idadi  ya  timu  sita katika  bara  la  Afrika  ambayo imefikia  hatua  ya  robo fainali, na  kujiunga  na  timu  nyingine   mbili  za  bara  la Afrika  ambazo  zimeweza  kufikia  hatua  hiyo, Cameroon mwaka  1990  na  Senegal  mwaka  2002.

Wakati  huo  huo  shirikisho  la  soka  duniani FIFA linasaka  hoteli  ya   kuiweka  timu  ya  Uholanzi  baada  ya maafisa  wa  timu  hiyo kushindwa  kujiwekea  vyumba hadi  mwisho  wa  mashindano  hayo. Shirikisho  la  soka la  Uholanzi  liliomba  kubaki  katika  hoteli  waliyoko  hivi sasa  mjini  Johannesburg  ya  Sandton Hilton  hadi  Julai 5  na  hoteli  hiyo  sasa  imejaa.

Wakati  shirikisho  la  FIFA  huziweka  timu zote  usiku mmoja   kabla  na  baada  ya  mchezo, timu  hulazimika kufanya  utaratibu  wao  kwa  ajili  ya   siku  nyinginezo. Shirikisho  la  kandanda  la  Uholanzi  limethibitisha  kuwa timu  yao  inapaswa  kuondoka  katika  hoteli  hiyo  kwa kuwa  imekwisha  jaa  kwa  kipindi  chote  cha  mashindano hayo.

Nahodha  wa  zamani  wa  Uholanzi  Ruud  Gullit amesisitiza  kuwa   mchezaji  wa   pembeni Arjen Robben atakuwa  muhimu  katika  kuishinda  Uruguay  katika mchezo  wao  wa  nusu  fainali  hii  leo. Gullit  ni  nahodha pekee  wa  Uholanzi  ambaye  ameweza  kubeba  kombe katika  mashindano  makubwa   akiwa  na  timu  ya  taifa ya  Uholanzi  baada  ya  kushinda  ubingwa  wa  bara  la Ulaya  mwaka  1988.

Ameongeza  kuwa  kikosi  cha  kocha  Bert van Marwijk kinaweza  kuondoa  machungu  ya  kufungwa  mara  kwa mara  katika  fainali, kama  ilivyotokea  mwaka  1974  na 1978  katika  kombe  la  dunia.

Mwandishi:  Sekione Kitojo/RTRE/AFPE

Mwandishi:  Abdul-Rahman

 • Tarehe 06.07.2010
 • Mwandishi Sekione Kitojo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/OByY
 • Tarehe 06.07.2010
 • Mwandishi Sekione Kitojo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/OByY
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com