Upinzani waiondoa madarakani serikali ya Ureno | Matukio ya Kisiasa | DW | 11.11.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Upinzani waiondoa madarakani serikali ya Ureno

Muungano wa upinzani unaoegemea siasa za mrengo wa kushoto nchini Ureno umeiondoa madarakani serikali inayoongozwa na wachache kutoka chama cha wahafidhina.

Waziri mkuu Pedro Passos Coelho

Waziri mkuu Pedro Passos Coelho

Kuondolewa madarakani kwa serikali hiyo kumefuatia kura bungeni iliyopigwa jana ikiwa ni karibu wiki mbili baada ya serikali hiyo kuapishwa kuingia madarakani.

Muungano huo mpya wa upinzani unajumuisha chama cha wasosholisti cha PS, wakomunnisti pamoja na washirika wao walipiga kura ya kutokuwa na imani na mipango ya serikali katika hatua ambayo huenda ikawatia khofu wawekezaji pamoja na masoko katika wakati ambapo nchi hiyo bado inajikwamua kutokana na mgogoro wa kiuchumi.

Hatua hiyo imesababisha moja kwa moja kuifikisha mwisho serikali ya waziri mkuu Pedro Passos Coelho ambaye chama chake cha muungano wa siasa za wastani unaoegemea mrengo wa kulia ulishinda kura nyingi katika chaguzi za mwezi uliopita lakini ukapoteza wingi wa viti bungeni ambao muungano huo umekuwa ukipata tangu mwaka 2011.

Bunge la Portugal likishiriki mchakato wa kupiga kura ya kutokuwa na Imani na serikali

Bunge la Portugal likishiriki mchakato wa kupiga kura ya kutokuwa na Imani na serikali

Serikali hiyo yake ya pili ndiyo iliyowahi kukaa kwa muda mfupi zaidi madarakani tangu Ureno ilipokuwa nchi ya kidemokrasia mnamo mwaka 1974.Antonio Costa kiongozi wa chama cha kisosholisti anasema inawezekana nchi hiyo kufungua ukurasa mpya wa kubana matumizi katika kanda ya yuro. Muswaada wa kutokuwa na imani na mipango ya serikali ya waziri mkuu Coelho uliungwa mkono kwa kura 123 dhidi ya 107 za walioupinga.

Kwa pamoja chama cha kisosholisti na kile cha kikomunisti na wanaofuata siasa za mrengo wa kushoto ambao wanamafungamano ya karibu na chama tawala cha Ugiriki cha Syriza wanashikilia wingi wa viti bungeni wakiwa na viti 122 katika bunge lenye idadi ya viti jumla 230. Muungano huo ni wa kwanza wa aina yake tangu nchi hiyo ya Ureno ilipoingia katika mfumo wa Demokrasia pamoja na kwamba muungano huo ulielekea kutowezekana kufanikiwa kubakia pamoja wiki kadhaa zilizopita kutokana na tafauti zilizokuwa zikishuhudiwa ndani ya makundi kadhaa ya upande wa mrengo wa kushoto.

Ni kwa mara ya kwanza kwamba vyama vitatu vinakuja pamoja na kuweka kando tafauti zao na kukubaliana kushirikiana kwa pamoja na kuunda serikali nchini Ureno.Vyama hivyo vinataka kudurusu upya baadhi ya mageuzi yanayohusu kubana matumizi yaliyopendekezwa na wakopeshaji baada ya nchi hiyo ya Ureno kupata mkopo wa kujikwamua kiuchumi wa dola Bilioni 87.

Majengo ya Bunge la Portugal

Majengo ya Bunge la Portugal

Hata hivyo hadi sasa makubaliano kati ya vyama vya mrengo wa kushoto bado hayajawekwa hadharani ingawa mipango yao ikiwemo ule wa kuwalipa wafanyakazi wa serikali malipo yao yaliyokatwa pamona na kurudisha siku nne za mapumziko ambazo ziliondolewa kwa lengo la kuimarisha ukuaji wa kiuchumi.

Waziri mkuu Coelho mwenye umri wa miaka 51 ameutuhumu muungano mpya kabla ya mchakato wa kura ya kutaka kutia msukumo wa kufanyika kile kinachoitwa mpango wa muda mfupi na unaoeleweka ambao utaonekana kama ni kitisho kwa uchumi wa taifa hilo linalojikwamua kutokana na hali ngumu ya kiuchumi.

Mwandishi Saumu Mwasimba/afp

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com