Upinzani Venezuela utashiriki uchaguzi wa mikoa | Matukio ya Kisiasa | DW | 01.09.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Upinzani Venezuela utashiriki uchaguzi wa mikoa

Vyama vya upinzani nchini Venezuela vimetangaza kuwa vitashiriki katika chaguzi za mikoa na manispaa zilizopangwa kufanyika Novemba. Uamuzi huo ni tofauti na msimamo wao wa awali wa kususia upigaji kura wa hivi karibuni.

Vyama hivyo vya upinzani vimetoa tangazo hilo siku chache kabla ya upande wa upinzani na serikali kukutana Mexico kwa lengo la kuendeleza mazungumzo ya kutafuta njia ya kumaliza mkwamo wa kisiasa uliotawala Venezuela.

Pande zote mbili zilikubaliana kujadili masuala ya uchaguzi kama sehemu ya mazungumzo, yaliyoanza rasmi mapema mwezi huu.

Soma zaidi: Guaido aliomba jeshi kususia uchaguzi Venezuela

Juan Guaido, kiongozi wa muungano huo wa vyama vya upinzani wa United Platform alliance amesema wamefanya uamuzi huo baada ya majadiliano ya kina yaliyoshirikisha viongozi wa mikoa na kitaifa.

Siku chache zijazo, serikali ya Venezuela na upinzani wanapanga kuanza mazungumzo yao huko Mexico wakisaka suluhisho la mzozo wa kisasa ulioikwamisha nchi yao. Mazungumzo yalizinduliwa katika Jiji la Mexico mwezi uliopita.

Upinzani unadai kufanyike uchaguzi ulio huru pamoja na kuachiliwa kwa wafungwa wa kisiasa. Huku serikali ya kisoshalisti ya Rais Nicolas Maduro ikitaka kulegezewa vikwazo vya kimataifa ilivyowekewa.

Upinzani ulisusia uchaguzi 2018

Upinzani haukushiriki uchaguzi wa mwaka 2018 kwa madai kwamba haukuwa huru na wa haki. Rais Maduro anayeiongoza nchi hiyo kwa mkono wa chuma alishinda kwenye uchaguzi huo. Bunge lilikataa kumtambua kama rais halali wa nchi hiyo, kwa madai kwamba kulifanyika wizi wa kura wakati wa uchaguzi, vitisho pamoja na watu wachache kujitokeza katika vituo vya kupigia kura.

Kolumbien Cúcuta | Migranten Grenze | Soldaten

Raia wa Venezuela wakikimbilia Colombia

Kufuatia hali hiyo, Guaido, ambaye ni spika wa bunge la Venezuela alijitangaza kama rais wa mpito. Na tangu wakati huo, pande hizo mbili zimekuwa zikivutana kisiasa huku Maduro akigoma kuachia madaraka.

Soma zaidi:Maduro asema Venezuela haitasalimu kutokana na vitisho 

Licha ya kuwa na hifadhi kubwa ya mafuta duniani, uzalishaji wa mafuta umepungua na kufika katika viwango vya chini kabisa kuwahi kushuhudiwa kwa miaka 80 nchini humo.

Na hivyo raia wa Venezuela wanakabiliwa na matatizo mengi ya kiuchumi huku watu wapatao milioni 5.6 wakiwa wameshaikimbia nchi hiyo.

Mamilioni ya watu wa Venezuela wanaishi katika umaskini kutokana na mishahara midogo na bei za juu za chakula zinazotokana na mfumuko wa bei mbaya zaidi kuwahi kutokea duniani.

Shirika la msaada wa chakula la Umoja wa Mataifa limekadiria kwamba mtu mmoja kati ya kila raia watatu wa Venezuela anashindwa kupata chakula cha kutosha cha kila siku.

Uchaguzi wa mikoa na manispaa umepangwa kufanyika Novemba 21.

Vyanzo: ap, dpa