Upinzani Tanzania wawachuja wanaotaka kuwania urais | Matukio ya Afrika | DW | 03.08.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Upinzani Tanzania wawachuja wanaotaka kuwania urais

Vyama vya upinzani nchini Tanzania vimeanza vikao vya kuwajadili na kuwachuja wagombea wa nafasi za urais wa Jamhuri ya Muungano na Zanzibar katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi Oktoba.

Hata hivyo, wakati vyama hivyo vikianza vikao vyao, swali moja linaloendelea kugonga vichwa vya habari ni iwapo safari hii vitafanikiwa kumsimamisha mgombea mmoja atakayeungwa mkono na vyama vyote vya upinzani au la.

Vyama vya Chadema na ACT Wazalendo vimeanza kujifungia katika vikao vyao vya ndani vikiwachambua wagombea wake ambao hawajafahamika rasmi kwa umma. Chadema imesema wagombea wake wa urais wanatarajiwa kufahamika kesho wakati wajumbe wa mkutano mkuu watakapokutana na kwa chama cha ACT Wazalendo, wagombea wake watafahamika siku ya Jumatano.

Leo vyama hivyo vimekuwa na vikao vyao vya ndani, wakati baraza kuu la chadema linakutana na kisha litatoa mapendekezo yake juu ya wagombea wanaofaa kupigiwa kura katika mkutano mkuu wa kesho.

Tundu Lissu (kwenye picha) ni miongoni mwa wanaotaka kuwania urais Tanzania

Tundu Lissu (kwenye picha) ni miongoni mwa wanaotaka kuwania urais Tanzania

Jumla ya wagombea 7 walichukua na kurejesha fomu huku majina yanayotajwa sana ikiwa pamoja na ya makamu mwenyekiti wa chama hicho, Tanzania bara Tundu Lissu na mwenyekiti wa chama hicho kanda ya kati, Lazaro Nyalandu.

Chama cha ACT Wazalendo ni mgombea mmoja tu anayepewa nafasi ya kupitishwa na mkutano wake wa hapo kesho kutwa, Bernard Membe waziri wa zamani wa mashauri ya kigeni aliyejiunga na chama hicho katika siku za hivi karibuni.

Je upinzani utaweza kuwa na mgombea mmoja kuwania urais Zanzibar?

Ingawa vyama vyote havijaondoa uwezekano wa kuwa na ushirikiano wa pamoja kwenye uchaguzi wa mwaka huu, wafuatiliaji wa masuala ya siasa wanatilia shaka namna vyama hivyo vitakavyoweza kulifanikisha jambo hilo hasa wakati huu ambako tarehe ya kuanza kwa kampeni ikizidi kukaribia.

Swali kuu ni ikiwa upinzani utamteua mgombea mmoja kuwania urais

Swali kuu ni ikiwa upinzani utamteua mgombea mmoja kuwania urais

Wakilizungumzia suala hilo, chama cha ACT Wazalendo kinasema kuwa viongozi wa pande zote bado wanaendelea kunoa bongo zao kabla ya kufikia makubaliano ya pamoja.

Wengi wanaofuatilia siasa wanasema njia pekee ambayo wapinzani wanaweza kuwapa wakati mgumu wagombea wa chama tawala CCM ni kwa kuunda umoja kama ulioshuhudiwa wakati wa uchaguzi uliopita wa 2015.

Mbali ya vyama hivyo kuanza kuwachambua wagombea wake wa urais, kadhalika mtihani mwingine unavyovikabili ni namna ya kupitisha majina ya wagombea wa nafasi za ubunge na udiwani, mtihani ambao pia unakikabili chama tawala CCM.

Mhariri: Gakuba, Daniel