Upinzani Syria kususia mazungumzo ? | Matukio ya Kisiasa | DW | 11.02.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Upinzani Syria kususia mazungumzo ?

Ujumbe wa upinzani wa Syria ulioko Geneva kwa duru ya pili ya mazungumzo ya amani umeonya kwamba haitoshiriki duru ya tatu ya mazungumzo hayo iwapo hakuna hatua yoyote ya maendeleo itakayofikiwa.

Msemaji wa upinzani wa Syria Louay Safi akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva. (10.02.2014).

Msemaji wa upinzani wa Syria Louay Safi akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva. (10.02.2014).

Ujumbe wa upinzani wa Syria ulioko Geneva kwa duru ya pili ya mazungumzo ya amani umeonya kwamba haitoshiriki duru ya tatu ya mazungumzo hayo iwapo hakuna hatua yoyote ya maendeleo itakayofikiwa.Onyo hilo linakuja wakati Urusi ikikwamisha juhudi za mataifa ya magharibi kuidhinisha azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo lingeliwekea vikwazo Syria venginevyo serikali ya nchi hiyo inaruhusu kupelekwa kwa misaada ya kibinaadamu kwa watu walioko kwenye maeneo yaliyozingirwa n mapigano.

Msemaji wa upinzani wa Syria Loay Safi amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva hapo jana kwamba iwapo kutakuwa hakuna maendeleo yoyote yatakayofikiwa itakuwa ni kupoteza wakati kufikiria juu ya duru ya tatu ya mazungumzo.

Amesema ujumbe wake umelizungumzia suala hilo na mjumbe wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Waarabu Lakhdar Brahimi hapo jana asubuhi wakati duru ya pili ya mazungumzo ilipoanza mjini Geneva.Hata hivyo amesema kwa kadri kutakavyokuwa na matumaini kwamba mazungumzo hayo yanaweza kupiga hatua hawatoyatekeleza.

Naibu waziri wa mambo ya nje wa Syria Faisal Maqdad akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva. (10.02.2014).

Naibu waziri wa mambo ya nje wa Syria Faisal Maqdad akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva. (10.02.2014).

Kauli yake hiyo inakuja baada ya siku ya kwanza ya mazungumzo hayo kuanza kwa mvutano ambapo Brahimi alikutana kwa nyakati tafauti na wawakilishi wa serikali na upinzani kwa matarajio kwamba kuwatenganisha pengine kungelisaidia kufanikisha mambo mengi kuliko ilivyokuwa katika mazungumzo ya duru ya kwanza ambayo yametajwa kuwa yameshindwa kabisa kuleta tija.

Pande hizo mbili zinazopingana leo zinatarajiwa kukutana katika mazungumzo ya pamoja. Wakati kuzikutanisha pande hizo mbili kunaweza kukaonekana kama ni hatua kwenye mwelekeo sahihi hakuna dalili kwamba duru hii ya sasa ambayo inatarajiwa kuendelea hadi Ijumaa itapiga hatua yoyote ya maendeleo kukomesha umwagaji damu nchini humo.

Mamilioni wahitaji misaaada

Kwa upande mwengine Urusi inakwamisha juhudi za mataifa ya maghairibi kutaka kuidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa azimio litalaloiwekea vikwazo Syria venginevyo serikali ya nchi hiyo inafunguwa njia za kufikisha misaada ya kibinaadamu kwa watu waliozingirwa na mapigano.

Raia wakihamishwa kutoka mji wa Homs uliozingirwa. (09.02.2014).

Raia wakihamishwa kutoka mji wa Homs uliozingirwa. (09.02.2014).

Kuna takriban watu robo milioni nchini Syria wanaoishi kwenye maeneo yaliyozingirwa ikimaanisha kwamba hawapati kabisa misaada ya kibinadaamu na hawawezi kuondoka katika maeneo hayo.

Jens Learke ni msemaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoratibu Misadaa ya Kibinaadam amesema ni muhimu sana kuwafikia watu milioni 9.3 wanaohitaji misaada nchini Syria.

Ameongeza kusema "Tumeweza kuwafikia baadhi yao lakini tunahitaji kuwafikia watu hao wote kwani zaidi ya milioni 3 wako katika maeneo ambayo ni vigumu kuyafikia."

Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa Vitaly Churkin ameahidi kulipigia kura ya turufu iwapo ikibidi azimio la kuilazimisha serikali ya Syria kufunguwa njia za kufikisha misaada ya kibinaadamu kwa watu waliozingirwa na mapigano.Balozi huyo na mwenzake wa China wote wawili wameususia mkutano wa jana kujadili azimio hilo linaloungwa mkono na mataifa ya magharibi ya yale ya Kiarabu.

Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP/AP

Mhariri: Mohammed Khelef

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com