1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani na serikali kuunda kamati Misri

Thelma Mwadzaya7 Februari 2011

Wawakilishi wa wanasiasa wa upizani na Makamu wa rais mpya wa Misri wamekutana na kuafikiana kuunda kamati maalum itakayozidurusu upya sheria za nchi na katiba.

https://p.dw.com/p/10BsS
Viongozi wa upinzani na serikali kwenye kikao,CairoPicha: dapd

Kwa mujibu wa msemaji wa serikali ya Misri Magdi Radi,kamati hiyo itawaleta pamoja wanasheria wa ngazi za juu na wanasiasa watakaokuwa na wajibu wa kutoa mapendekezo ya mageuzi ya katiba na taratibu bungeni ifikapo mwanzoni mwa mwezi ujao wa Machi.

Kamati nyengine ya pembeni itakuwa na wajibu wa kuundoa mkwamo wa kisiasa uliopo kadhalika kuzipa msukumo harakati za kuwa na uhuru zaidi wa kupata maelezo kwenye mtandao.  

Ägypten Proteste Chaos Flash-Galerie
Waandamanaji wanaompinga Rais Hosni Mubarak wakiwa uwanja wa Tahrir,tarehe 6 FebruariPicha: dapd

Wapinzani wa serikali wamekuwa wakiandamana tangu wiki mbili zilizopita wakiwa na lengo la kumshinikiza Rais Hosni Mubarak ajiuzulu baada ya kuwa madarakani kwa kipindi cha miaka 30.Kwa upande wake Rais Mubarak aliye na umri wa miaka 82 anashikilia kuwa kamwe hatojiuzulu mpaka uchaguzi utakapofanyika ifikapo mwezi wa Septemba kama ilivyopangwa.