1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani: DRC haiko tayari kwa Uchaguzi

31 Oktoba 2018

Upinzani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo umesema kuwa nchi hiyo haiko tayari kwa uchaguzi wa mwezi Disemba siku moja baada ya jeshi la nchi hiyo kutoa vifaa kwa Tume ya Uchaguzi

https://p.dw.com/p/37SlX
Kongo Präsident Joseph Kabila
Picha: picture-alliance/AP Photo/J. Bompengo

Msemaji wa chama kikuu cha upinzani nchini jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo UDPS; Augustin Kabuya amesema kiwango cha vifaa kilichokabidhiwa kwa tume ya uchaguzi hakitoshi kutokana na ukubwa wa nchi hiyo ambayo vilevile haina miundombinu ya kutosha ya barabara kuwezesha usafirishaji wa vifaa vya kupigia kura.

Siku ya jumatatu Jeshi la nchi hiyo lilikabidhi kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi magari makubwa 150 na ndege kadhaa kwa ajili ya kusaidia shughuli za maandalizi ya uchaguzi uliosubiiwa kwa muda mrefu.

Uchunguzi wa maoni ya umma uliochapishwa leo umeonesha kuwa licha ya changamoto zilizopo wagombea wawili wa upinzani wanaongoza kuelekea uchaguzi huo unaotarajiwa baadae mwezi disemba.

Kiongozi wa Chama Kikuu cha Upinzani UDPS ambaye pia anawania kiti cha urais Felix Tshisekedi ndiye anaongoza kwenye uchunguzi huo wa maoni kwa asilimia 36 akifuatiwa na Vital Kamerhe wa chama cha Union for the Congolese Nation aliyeshika nafasi ya tatu wakati wa uchaguzi wa mwaka 2011 ambaye anaungwa mkono na wapiga kura kwa asilimia 17.

Mgombea wa Chama Tawala na waziri wa wa zamani wa mambo ya ndani Emmanuel Ramazani Shadary, ambaye anaungwa mkono na rais Joseph Kabila ameorodheshwa nafasi ya tatu kwenye uchunguzi huo wa maoni kwa kupata asilimia 16.

Rais kabila aliridhia kuachia madaraka baada ya miongo miwili kutokana na shinikizo kubwa kutoka jumuiya ya kimataifa.

Robo tatu ya raia wanataka uchaguzi kucheleweshwa

Kulingana na kura hiyo hiyo ya uchunguzi wa maoni umma iliyoitishwa na kampuni ya BERCI na kundi la utafiti kuhusu DRC katika Chuo Kikuu cha New York, robo tatu ya wapiga kura wanaunga mkono wito wa kucheleweshwa kwa uchaguzi huo.

Taifa hilo linaloandamwa na mizozo lina ukubwa wa kilomita za mraba zaidi milioni 2.3  zinazoifanya kuwa nchi kubwa kuliko zote kusini mwa Jangwa la Sahara na karibu robo tatu ya ukubwa wa bara zima la Ulaya lakini ina kilometa 27,877 pekee ya barabara za lami.

M23 Rebellen in Goma Kongo
Picha: picture-alliance/dpa

Msemaji wa UDPS Kabuya amesema kutolewa kwa magai, ndege na helikopta kulifanywa kwa lengo tu la kuuonesha ulimwengu kuwa nchi hiyo iko tayari kwa uchaguzi lakini wao wanafahamu kuwa hata tume ya uchaguzi haiko tayari kwa zoezi hilo.

Wakati wa hafla ya kukabidhi vifaa hivyo kusaidia uchaguzi, maafisa wa serikali ya Kongo walisema uchaguzi uliohairishwa mwaka 2016 na baadaye mwaka jana unataendelea kama ulivyopangwa mwezi Disemba bila ya msaada wa Jumuiya ya Kimataifa.

Chaguzi za hapo kabla za mwaka 2006 na 2011 zilifanyika kwa msaada kutoka ujumbe wa amani wa Umoja wa Mataifa nchini humo MUNUSCO.

Hata hivyo uhusiano kati ya serikali mjini Kinshasa na ujumbe huo wa amani umetatizika katika siku za hivi karibuni.

Serikali ya Kabila umetoa wito mara kadhaa ya kutaka kuondolewa kwa ujumbe huo wa amani ulioingia nchini humo mwaka 2000 wakati wa vita vya pili vya Kongo.

MUNUSCO ina vikosi vya wanajeshi wa kulinda amani wanaopindukia 15000, zaidi ya polisi 1000 na wafanyakazi wa kiraia 2500 nchini humo.

DRC imekataa msaada wa kimataifa

USA New York Vereinte Nationen Joseph Kabila
Picha: picture-alliance/Xinhua/Q. Lang

Mzozo bado unaendelea hasa katika jimbo la Kivu kaskazini uliko mpaka wa mashariki ya taifa hilo ambapo kumekuwa kitovu cha umwagikaji damu na ukatili unaofanywa na amakundi yenye silaha, waasi na vikosi vya serikali kwa zaidi ya miaka 20.

Alipohutubia hadhara kuu ya Umoja wa Mataifa mwezi Septemba rais Kabila alitoa ahadi ya kupinga uingiliaji wowote kutoka nje wakati wa uchaguzi mkuu na kusema nchi yake ingegharamia bila kuhitaji msaada uchaguzi huo wa disemba.

Uchaguzi wa rais, wabunge na manispaa za miji uliopangwa tarehe 23 disemba utafanikisha kupatikana mrithi wa Kabila ambaye anazuiwa na utaratibu wa mihula miwili kuwania tena.

Kabila mwenye umri wa miaka 47 aliingia madarakani mwaka 2001 na hivi karibuni alimaliza uvumi wa kuendelea kubakia madarakani alipokubali kuitisha uchaguzi na kukabidhi maradaraka kwa njia ya amani.

Mwandishi: Rashid Chilumba/AFP

Mhariri:Yusuf Saumu