1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani Congo wagawanyika

Lilian Mtono
13 Novemba 2018

Wafuasi wa chama cha UDPS nchini Kongo wamesifu hatua ya kiongozi wao Felix Tshisekedi kujiondoa kwenye mkataba wa viongozi wa upinzani wa kusimamisha mgombea mmoja wa kupeperusha bendera ya upinzani.

https://p.dw.com/p/388p0
Demokratische Republik Kongo Felix Tshisekedi
Picha: picture-alliance/AA/P. Mulegwa

Wafuasi wa chama cha UDPS nchini Kongo wamesifu hatua ya kiongozi wao Felix Tshisekedi kujiondoa kwenye mkataba wa viongozi wa upinzani uliofikiwa mjini Geneva Uswisi ambapo walimteuwa Martin Fayulu kupeperusha bendera ya upinzani. Hatua hiyo imefuatia maandamano ya hasira yaliofanyika jana kwenye makao makuu ya chama hicho. Mpizani mwengine,Vital Kamerhe pia amejiondoa kwenye mkataba huo hatua iliyozusha maswali kuhusu uwezekano wa upinzani kunyakuwa ushindi kwenye uchaguzi ujao.

Nyimbo na vigelegele vilitawala kwenye makao makuu ya UDPS baada ya Felix Tshisekedi kutangaza kwamba amejiondoa kwenye mkataba wa Geneva na atashiriki mwenyewe kuwa mgombea wa kiti cha urais.

Mchana kutwa wa Jumatatu, mamia ya wafuasi wa chama hicho waliandamana na kuchoma matairi na picha za kiongozi wao ili kupinga, uteuzi wa mgombea mmoja atakayesimama kwa niaba ya upinzani ambaye hata hivyo hakuwa Felix Tsisekedi. Rubens Mikindo, naibu katibu mkuu wa chama cha UDPS amesema kwamba kiongozi wa chama hana budi kufuata matakwa ya wafuasi wa chama chake.

DR Kongo Trauer um Etienne Tshisekedi
Felix Tshisekedi akiwa na baadhi ya wafuasi wake katika makao makuu ya chama chake cha UDPSPicha: Reuters/R. Carrubba

Mkataba wa Geneva uliotiwa saini Jumapili na viongozi saba wa upinzani na kumteua Martin Fayulu kuwa mgombea mmoja, ulidumu masaa 24 tu. Mkataba huo haukudhaminiwa na vigogo pamoja na wafuasi wa vyama vya UDPS na UNC. Vital Kamerhe pia alijiondoa kwenye mkataba huo masaa machache baada ya Felix Tshisekedi kutangaza hatua hiyo. Rubens Mikindo amelezea kwamba Kwenye chama cha UDPS, hawana haja ya kuwa na mgombea mmoja hivi sasa.

Kwenye mitandao ya kijamii,maoni mengi yametolewa na raia wa kongo,wengi wakieleza kukasirishwa na kile wanachokiita tabia ya utoto ya wapinzani wa Kongo ambao hawaja fanikiwa kuungana pamoja toka uhuru wa nchi hii.

Kwa upande wake Martin Fayulu ameeleza kukerwa na hatua hiyo ya Felix Tshisekedi na Vital Kamerhe na kusema hakuna tofauti yeyote baina ya Kabila na baadhi ya wale wanaompinga. Hayo yote yametokea huku zikisalia siku 10 kabla ya kuanza kwa kampeni ya uchaguzi.

Mwandishi: Saleh Mwanamilongo,DW Kinshasa.

Mhariri: Iddi Ssessanga