1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UNDP: Maendeleo ya watu duniani yameshuka

Grace Kabogo
8 Septemba 2022

Umoja wa Mataifa umesema kwamba hali ya ubora wa maisha imezidi kuwa mbaya na kurudisha nyuma maendeleo ya wanadamu kwa asilimia 90 ya nchi zote duniani, huku mizozo mingi ikiwemo janga la COVID-19 ikiwa sababu kuu.

https://p.dw.com/p/4GZOX
Pakistan | Krise durch Überschwemmungen
Picha: Akram Shahid/AFP

Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa, UNDP kwa mara ya kwanza limetangaza kuwa tangu lilipoanzishwa miaka 30 iliyopita, Faharasa ya Maendeleo ya Mwanadamu ambayo inapima matarajio ya viwango vya ubora wa maisha ya nchi zote ulimwenguni, viwango vya afya, elimu, na viwango vya umri wa kuishi, imeshuka kwa miaka miwili mfululizo ya mwaka 2020 na 2021.

Mkurugenzi mkuu wa shirika la UNDP, Achim Steiner amesema hali hiyo inamaanisha kwamba binadamu watakufa mapema, hawatopata elimu nzuri, na mishahara yao itapungua. ''Chini ya vigezo hivyo vitatu, unaweza kupata hisia ya kwa nini watu wengi wanaanza kuhisi kukata tamaa, kuchanganyikiwa, na kupata wasiwasi kuhusu siku zijazo,'' alifafanua Steiner.

Kiwango kilianza kushuka 2020

Ripoti hiyo iliyopewa jina "Nyakati zisizo na uhakika, maisha yasiyo na utulivu," imesema kielelezo cha maendeleo ya mwanadamu kiliongezeka kwa miongo kadhaa, lakini kilianza kushuka mwaka 2020 na kimeendelea hadi mwaka 2021, na hivyo kuondoa mafanikio yaliyopatikana miaka mitano iliyopita.

Ripoti hiyo ya UNDP iliyochapishwa Alhamisi imelitaja janga la COVID-19 kuwa sababu kuu ya mabadiliko hayo ya kushuka kwa viwango vya ubora wa maisha ya mwanadamu, lakini imesema pia idadi kubwa ya migogoro ya kisiasa, kifedha na inayohusiana na hali ya hewa haijatoa muda kwa watu kupona.

Achim Steiner UNDP
Mkurugenzi mkuu wa shirika la UNDP, Achim SteinerPicha: Kyodo/IMAGO

Steiner amesema dunia imeshakumbwa na majanga hapo awali, pamekuwepo na migogoro hapo awali, lakini muunganiko wa kile kinachotokea duniani kwa sasa ni kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya binadamu.

Kwa mujibu wa ripoti ya UNDP, kikwazo hicho ni cha kimataifa, ambacho kimeathiri zaidi ya asilimia 90 ya nchi zote ulimwenguni. Kwenye faharasa hiyo nchi ya Uswisi ndiyo imetajwa kuwa imeendelea zaidi katika ustawi wa jamii ikifuatiwa na Norway na Iceland huku mataifa matatu kutoka barani Afrika ya Chad, Niger na Sudan Kusini yakiwa yameshika nafasi ya mwisho.

Na huku baadhi ya nchi zikiwa zimeanza kujikwamua kutokana na janga la virusi vya corona, mataifa mengine mengi katika eneo la Amerika ya Kusini, Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, Asia na Caribbean bado hata hayajaanza kujinasua na tayari kuna mzozo mpya umeibuka, ambao ni vita vya Ukraine.

Umri wa kuishi umechangia kushuka kwa maendeleo ya binadamu

Kitu kikubwa kilichochangia kushuka hivi karibuni kwa Faharasa ya Maendeleo ya Mwanadamu ni kupungua kwa umri wa kuishi ulimwenguni kutoka wastani wa miaka 73 mwaka 2019 hadi miaka 71.4 mwaka 2021. Mtafiti kiongozi wa ripoti hiyo, Pedro Conceicao, ameelezea kushuka huko kama ''mshtuko usio wa kawaida'', akigusia kwamba baadhi ya nchi ikiwemo Marekani zimepungua kwa miaka miwili au zaidi.

Ripoti hiyo pia imeangazia nguvu za mabadiliko ya tabia nchi, utandawazi na mgawanyiko wa kisiasa, ambavyo vimechangia kuongezeka kwa hisia za ukosefu wa usalama. Steiner anasema watu hawaaminiani tena.

Hata hivyo, ripoti hiyo ya UNDP pia imegusia maendeleo mazuri kama vile fursa za maendeleo ikiwemo teknolojia mpya ya kompyuta, sayansi na aina mpya za nafaka. Kwa mfano nchini Kenya asilimia 90 ya mahitaji ya umeme sasa yanaweza kutimizwa kwa kutumia nishati endelevu.

(AFP, DPA)