UN: Yemen inakabiliwa na janga la meli ya mafuta inayovuja | Matukio ya Kisiasa | DW | 16.07.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

UN: Yemen inakabiliwa na janga la meli ya mafuta inayovuja

Umoja wa Mataifa umetahadharisha juu ya uwezekano wa kutokea kwa janga la kibindamu kuhusu meli ya kubeba mafuta “FSO Safer” iliokwama katika pwani ya Yemen kwenye eneo linaodhibitiwa na waasi Wakihouthi.

Öltanker brennt vor der Küste von Jemen Flash-Galerie (AP)

Mkuu wa Shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa Inger Andersen ameliambia baraza la Usalama la Umoja huo kwamba meli hiyo inamwaga nje mafuta kutokana na kukaa kipindi kirefu bila kufanyiwa ukarabati.

Andersen amesema "FSO Safer,” meli ya kubeba mafuta ambayo imekaa kwa zaidi ya miaka mitano bila matengenezo na huenda ikashika moto na kusababisha madhara makubwa ya miaka mirefu sio tu kwa binadamu bali pia mifumo ya ikologia.

Kwa mujibu wa shirika la habari la AP meli hiyo imebeba takribani mapipa milioni 1.1 ya mafuta ghafi na imekuwa katika bahari nyekundu kwenye eneo la Ras Issa kwa zaidi ya miaka mitano, eneo linalodhibitiwa na waasi Wakihouthi.

Soma zidi UNICEF: mamilioni ya watoto kukabiliwa njaa Yemen

Ikumbukwe kuwa mnamo Mei 27, mkuu wa masuala ya kibinadamu katika Umoja wa Mataifa Mark Lowcock pia aliliambia baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa maji yameanza kumeza injini ya meli hiyo na kutishia kuizamisha au kuripuka.

"FSO Safer” meli yenye uwezo wa kubeba takribani mapipa ya mafuta ghafi milioni 3 ilinunuliwa kutoka Japan na serikali ya Yemen mnamo miaka ya 1980. Hata hivyo tangu nchi hiyo kukumbukwa na vita, meli hiyo imekuwa mikononi mwa waasi Wahouthi.

 Inger Andersen (Getty Images/M. Ngan)

Mkuu wa shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa Inger Andersen ameonya juu ya uwezekano wa meli ya mafuta ya FSO Safer kulipuka na kusababisha madhara ya kimazingira.

Hatari ya kulipuka

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa waasi hao wamekataa kuridhia wataalamu wa umoja huo kuifikia meli hiyo kwa ajili ya kuifanyia ukarabati, kuchukua baadhi ya mafuta ghafi na kuipeleka eneo salama.

Hata hivyo Umoja huo umesema kuwa katika siku za hivi karibuni, waasi hao wameashiria kukubaliana na Umoja huo kuhusu meli hiyo.

Katika taarifa yake kwa baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, mnamo Mei Lowcock, mkuu wa masuala ya kibinadamu katika Umoja huo alieleza wasiwasi kuhusu hatari ya uwezekano wa kuripuka na kusababisha madhara makubwa kwa mazingira kibindamu na uchumi sio tu kwa Yemen pekee bali pia kwa majirani zake.

Licha ya waasi Wakihouthi kukubali kikosi cha wataalamu wa Umoja wa Mataifa kuifikia meli hiyo, Lowcock bado anashuku kama waasi hao watafanya hivyo.

Aidha amewalaumu Wahouthi kwa kukataa kukubali kikosi cha wataalamu wa umoja huo kuifikia meli hiyo mnamo Agosti mwaka uliopita licha ya kwamba awali waasi hao walikuwa wameridhia kufanya hivyo.

Wakati hayo yakijiiri, watu 10 wamefariki Alhamisi katika mkoa wa Jawf ulio Kaskazini mwa Yemen kufuatia shambulio la angani lililofanywa na Muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia.

Miongoni mwa wahanga hao ni watoto 6 pamoja na wanawake wawili. Aidha watu watatu pamoja na watoto wanne walijeruhiwa katika shambulizi hilo.

Chanzo: AP

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com