UN yasita kuidhisha hatua za kijeshi nchini Mali | Matukio ya Afrika | DW | 06.07.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

UN yasita kuidhisha hatua za kijeshi nchini Mali

Baraza la Usalama la Umoja Mataifa limeunga mkono juhudi za mataifa ya Afrika Magharibi kukomesha vurugu nchini Mali, lakini limekataa kuunga mkono uingiliaji wa kijeshi katika taifa hilo.

Moja ya turaathi za mji wa Timbuktu.

Moja ya turaathi za mji wa Timbuktu.

Wanamgambo wa Kiislamu wa Ansar Dine na washirika wao wametumia fursa ya uasi uliyofanywa na Watuareg kaskazini mwa Mali, na hivi sasa wanadhibiti mbili ya tatu ya eneo hilo la jangwa, lililo na miji ya kihistoria ya Gao, Kidal na Timbuktu, ambako turaathi muhimu za dini ya kiislam zimeharibiwa katika siku chache zilizopita.

Wanamgambo wa Ansar Dine, wanaodhibiti sehemu kubwa ya Mali Kaskazini.

Wanamgambo wa Ansar Dine, wanaodhibiti sehemu kubwa ya Mali Kaskazini.

Uharibifu wa turaathi hizo umekosolewa na jumuiya ya kimataifa na pia kusababisha maandamano mjini Bamako, ambayo yalioongozwa na viongozi wa dini ya Kiislam. Kiongozi wa Baraza kuu la waislam nchini Mali, Mahmoud Dicko, aliwaomba waandamanaji wapatao 1000, kuwa watulivu na kuwaeleza kuwa uharibu huo ulifanywa kutokana na ujinga, na kutaka kuamsha hasira za wananchi.

Majirani wa Mali walikuwa wanataka Umoja wa Mataifa uidhinishe hatua za kijeshi ili kurejesha utulivu katika taifa hilo, na kurejesha sehemu ya kaskazini chini ya utawala wa Bamako. Mwezi uliyopita wa Juni, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliutaka Umoja wa Afrika na Jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika magharibi, ECOWAS, kuelezea kinagaubaga, azimio la namna gani walitaka lipitishwe.

Taarifa zaidi zahitajika
Lakini Azimio lililopitishwa jana halikuwapa msaada waliyoutafuta, lakini liliwapa matumaini ya kupata msaada huo kama utahitajika huko mbele. Azimio hilo pia lilielezea kuunga mkono juhudi za upatanishi za ECOWAS na Umoja wa Afrika nchini Mali.

Muswada wa azimio hilo uliyowasilishwa kwa Baraza na Ufaransa, ulieleza utayari wa Baraza hilo la Usalama kuangalia upya maombi ya ECOWAS kama taarifa zaidi zitatolewa, kuhusiana na malengo, uwezo na namna ya kupeleka vikosi vya kimataifa nchini Mali.

Waandamanaji mjini Bamako wakipinga kuvunjwa kwa turaathi za Mali zilizoko mjini Timbuktu.

Waandamanaji mjini Bamako wakipinga kuvunjwa kwa turaathi za Mali zilizoko mjini Timbuktu.

Ufaransa na Morocco zilikuwa mstari wa mbele kushinikiza Baraza la Usalama kuunga mkono uingiliaji kijeshi wa ECOWAS nchini Mali, ingawa idadi kubwa ya wanachama wengine wa baraza hilo wamekuwa wakisita kuunga mkono hatua hizo. Jumuiya hiyo kwa kushirikiana na Umoja wa Afrika, ilikuwa imepanga kupeleka vikosi 3,200 nchini Mali.

Ufaransa yataka washirika wa al-qaeda waorodheshwe
Waziri wa Mambo ya nje wa Ufaransa Laurent Fabius alisema jumuiya ya kimataifa laazima ifanye kila linalowezekana kupambana na ugaidi nchini Mali na kanda ya Sahel, ambao unatishia kuvuruga utulivu wa kanda hiyo. Alisema Ufaransa imezitaka nchi za kanda hiyo kuungana katika vita dhidi ya al-qaeda.

Baraza la Usalama lilionya dhidi ya hali mbaya ya kibinaadamu na vitendo vya utekaji vinavyofanywa na magaidi nchini Mali. Liliyataka mataifa ya kanda hiyo kusaidi kuwatambua na kuwaripoti watu wote waliyo na uhusiano na al-qaeda.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga\APE\RTRE
Mhariri: Josephat Charo