UN yarefusha muda wa UNAMID kubakia Darfur | Matukio ya Kisiasa | DW | 31.07.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

UN yarefusha muda wa UNAMID kubakia Darfur

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limerefusha muda wa mwaka mmoja kwa majeshi hayo kuwepo katika jimbo hilo la Sudan lenye mapigano.

default

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeongeza muda wa mwaka mmoja kwa majeshi ya kulinda amani ya umoja huo kuwepo katika jimbo la Sudan lenye mapigano la Darfur kwa muda wa mwaka mmoja zaidi. Hatua hiyo inamaanisha kuwa UNAMID, muungano wa vikosi vya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika, vitaendelea na operesheni kwenye jimbo la Darfur hadi Julai 2010.

Uamuzi huo uliofikiwa na baraza hilo lenye maamuzi ya juu katika Umoja wa Mataifa umesisitiza kuwa vikosi hivyo vitakuwa na kazi ya kuwalinda raia na kuhakikisha shughuli za mashirika ya misaada zinapewa kipaumbele zaidi ili wafanyakazi wa mashirika hayo waweze kufanya kazi zao kwa uhuru.

Vikosi vya Umoja wa Mataifa viliungana na vile vya Umoja wa Afrika mwishoni mwa mwaka 2007 na mwanzoni mwa 2008 kuongeza nguvu katika jitihada za kumaliza mapigano katika jimbo hilo la Magharibi mwa Sudan, ambako Marekani na mataifa mengine duniani yameyaita kuwa ni mapigano wa kimbari.

Kwa mujibu wa ripoti ya hivi karibuni iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, idadi ya vikosi hivyo bado havijafikia malengo yake, kutokana na kwamba wanajeshi wanaohitajika ni 20,000. Lakini wanajeshi waliopo Darfur kwa sasa ni 14,000 ambayo ni sawa na asilimia 68. Hata hivyo, Baraza hilo la Usalama la Umoja wa Mataifa limeomba kupatiwa taarifa kila baada ya miezi mitatu kuhusu maendeleo ya vikosi hivyo.

Mzozo baina ya waasi wenye asili ya Afrika na wapiganaji wenye asili ya Kiarabu wanaoungwa mkono na serikali ya Sudan, umesababisha vifo vya zaidi ya watu laki 3 tangu mwaka 2003. Na inakadiriwa kuwa watu wengine milioni 2.6 hawana makaazi huku wananchi milioni 4.7 wa Darfur wanategemea msaada ya kibinaadamu.

Wakati huo huo, Mjumbe maalum wa Marekani nchini Sudan, Jenerali mstaafu Scott Gration, amesema hakuna ushahidi wa kutosha kwa Marekani kuendelea kuiweka Sudan katika orodha yake ya nchi za kigaidi, na hivyo kuiadhibu nchi hiyo bila sababu kwa kuiwekea vikwazo vya kiuchumi. Akizungumza na Kamati ya Bunge ya Uhusiano wa Kigeni, Jenerali Scott amesema hatua hiyo inadidimiza maendeleo ya Sudan, nchi inayohitaji kuwa na amani na utulivu.

Mjumbe huyo maalum wa Marekani nchini Sudan ametolea mfano wa vikwazo hivyo kuwa ni pamoja kutopelekwa kwa vifaa vya ujenzi wa barabara na kompyuta kwa ajili ya sekta ya elimu. Kauli hiyo ya Jenerali Scott ameitoa akitetea hatua ya utawala wa Rais Barack Obama wa kutaka kusaidia kufikiwa kwa makubaliano ya amani ya mwaka 2005 ambayo bado yanalegalega yaliyomaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe baina ya Sudan Kusini na Sudan Kaskazini, vilivyodumu kwa miongo miwili.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (DPAE/AFPE)

Mhariri: M. Abdul-Rahman

 • Tarehe 31.07.2009
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/J0lt
 • Tarehe 31.07.2009
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/J0lt
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com