UN yapitisha azimio kupambana na maharamia wa kisomali | Matukio ya Kisiasa | DW | 08.10.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

UN yapitisha azimio kupambana na maharamia wa kisomali

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeidhinisha azimio la kupelekwa kwa meli na ndege za kijeshi kwenye eneo la pwani ya Somalia kupambana na vitendo vya utekaji nyara meli vinavyofanywa na maharamia wa kisomali

Meli ya Ukraine itwayo Faina ambayo inashikiliwa mateka na maharamia wa kisomali

Meli ya Ukraine itwayo Faina ambayo inashikiliwa mateka na maharamia wa kisomali

Azimio hilo nambari 1838 linazitaka nchi zote zenye kuguswa na hali ya usalama wa majini, kushiriki katika mapambano hayo haswa kwa kupeleka meli na ndege za kivita.


Azimio hilo lililotayarishwa na Ufaransa linayataka mataifa yenye meli na ndege za kivita zilizoko kwenye maeneo ya pwani ya Somalia kushiriki katika mapmbano hayo dhidi ya maharamia wa kisomali.


Balozi wa Ufaransa kwenye Umoja wa Mataifa Jean-Maurice Ripert alielezea kufurahishwa kwake na uamuzi wa baraza hilo kupitisha azimio hilo kwa kauli moja, akisema hatua hiyo ni ujumbe kwa maharamia kuwa jumuiya ya kimataifa imechoshwa na vitendo vyao.


´´Azimio hili liko wazi kabisa, kuzitaka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kupambana kwa njia yoyote ile na maharamia, chini ya ibara ya saba.Pia ni jibu kwa serikali ya somalia iliyotuma barua umoja wa mataifa kuomba msaada wa jumuiya ya kimataifa kupambana na maharamia katika pwani ya somalia na kwenye bahari kuu kwenye pwani hiyo hiyo ya somalia.´´


Balozi huyo wa Ufaransa ambayo kwa sasa ndiyo inayoshikilia urais wa Umoja wa Ulaya, pia amesema kuwa umoja huo wa Ulaya unajiandaa kuanzisha harakati kubwa dhidi ya maharamia hao kabla ya mwisho wa mwaka huu.


Lakini kwa upande wake balozi wa Afrika Kusini katika Umoja wa Mataifa, Dumisan Kumalo alisema kuwa pamoja na kwamba alipiga kura kuunga mkono azimio hilo lakini baraza hilo limeshindwa kuona picha halisi ya Somalia, akimaanisha vita vinavyoendelea nchini humo.


Mashirika ya misaada yamesitisha shughuli zao nchini Somalia kutokana na kuongezeka kwa hali tete ya usalama, kunakosababishwa na wanamgambo wa kiislam wanaopigana dhidi ya serikali ya mpito.


Umoja wa Mataifa umesema kuwa umeshindwa kupeleka shehena ya misaada ya kibinaadamu kutokana na hofu ya meli kutekwa na maharamia hao, na hivyo kuwazidishia madhila wananchi wa Somalia.


Ban Ki-moon ni Katibu Mkuu wa Umoja huo wa Mataifa akieleza zaidi alisema

´´Meli za kivita kutoka Uholanzi, Ufaransa, Denmark na Canada zimekuwa zikizisindikiza meli zetu hadi bandarini.Canada itasitisha jukumu lake hilo tarehe 23 mwezi huu.Na mpaka sasa hakuna nchi yoyote iliyojitolea kuchukua nafasi ya Canada.Bila ya kusindikizwa meli hizo za misaada hazitoweza kufika na bila ya misaada watu wengi watakufa´´.


Mwezi June mwaka huu Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio linaloyapa nguvu mataifa yanayotaka kushirikiana na serikali ya mpito, kutuma meli za kivita katika eneo la Somalia kupambana na maharamia hao.Azimio hilo linatoa muda wa miezi sita.


Pwani ya somali ni moja kati ya maeneo hatari kabisa duniani ambapo meli kadhaa zimekuwa zikitekwa kabla ya kuachiwa baada ya maharamia hao kulipwa.


Hapo jana maharamia wanaoishikilia meli ya Ukraine yenye shehena kubwa ya silaha vikiwemo vifaru walisema kuwa wanakaribia kufikia makubaliano na wahusika na huenda wakaichia meli hiyo hii leo.


Maharamia hao wamekuwa wakidai kulipwa dola millioni 20 kabla ya kuiachia meli hiyo waliyoiteka tarehe 25 mwezi uliyopita.


Wakati huo huo wafanyakazi wawili wa shirika la medecins du Monde yaani tiba kwa dunia ambao walitekwa na wanamgambo wa kisomali, katika mpaka na Ethiopea wako katika hali nzuri, na majadiliano yanaendelea kuhusiana na kuachiwa kwao.


Wafanyakazi hao walitekwa nyara mwezi uliyopita walipokuwa katika kazi za misaada ya kibinaadamu kwenye jimbo la Ogaden linalopakana na Somalia, ambapo watekaji hao wanadai kiasi cha fedha ili waachie.Hata hivyo kiasi cha fedha wanachodai na uraia wa mateka hao havijajulikana
 • Tarehe 08.10.2008
 • Mwandishi Liongo, Aboubakary Jumaa
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/FVzU
 • Tarehe 08.10.2008
 • Mwandishi Liongo, Aboubakary Jumaa
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/FVzU
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com