UN yapigia kura azimio kuzuia silaha za nyukilia | Matukio ya Kisiasa | DW | 28.10.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

UN yapigia kura azimio kuzuia silaha za nyukilia

Kamati ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa imepiga kura kuunga mkono azimio  lenye  lengo la kupiga marufuku silaha za nyuklia licha ya azimio hilo kupingwa na mataifa yenye nguvu yaliyo na silaha za aina hiyo.

Nchi 123 zilipiga kura kuunga mkono azimio hilo wakati nchi 38 zililipinga na nchi 16 zikajizuia. Nchi nne miongoni mwa nchi tano wanachama wa kudumu wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa  ambazo ni Marekani, Urusi, Uingereza na Ufaransa zilipinga azimio hilo wakati  China haikupiga kura.

Licha ya kukumbana na upinzani  azimio hilo lililowasilishwa na Austria, Brazil, Ireland, Mexico, Nigeria na Afrika Kusini sasa litapelekwa katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambako linatarajiwa kupigiwa kura Desemba mwaka huu.

Azimio hilo linalenga kuitishwa mkutano utakaofanyika Machi, 2017 ili kujadili juu ya umuhimu wa kupitisha sheria itakayozuia silaha za nyukilia na hivyo kuelekea kupigwa marufuku kabisa utengenezaji  wa silaha hizo.

Azimio hilo limeungwa mkono na Mkurugenzi mtendaji wa mtandao wa kimataifa unaoendesha kampeni ya kupiga marufuku silaha za nyukilia (ICAN ) Beatriz Fihn, ambaye amesema kura hiyo inaashiria wazi kuwa mataifa mengi duniani yanafikiria suala la kupigwa marufuku silaha za nyukilia ni la lazima na linalopaswa kuchukuliwa kama suala la dharura.  Mkurugenzi huyo alisema kuwa kura hiyo inalenga kuzishawishi nchi zenye nguvu ya nyuklia kuachana na shuguli zake hizo kama ambavyo imefanyika katika suala la mabomu ya kutegwa ardhini na mabomu  ya mtawanyiko.

Japan yapiga kura kuunga mkono azimio

Japan ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikipiga kampeni dhidi ya matumizi ya silaha za nyuklia  hata hivyo ilipiga kura kupinga azimio hilo kama ilivyofanya Korea Kusini ambayo imekuwa ikikabiliwa na kitisho kutoka kwa Korea Kaskazini. 

Mwaka 2009  Rais wa Marekani Barack Obama alitoa mwito wa kupigwa marufuku silaha za nyukilia ingawa Marekani haitarajiwi kuunga mkono jitihada hizo katika Umoja wa Mataifa.

Wapinzani wamekuwa wakitoa hoja kuwa suala la kuzuia silaha hizo lazima lifanyike kupitia majadiliano kuhusu mkataba wa kuzuia kuenea kwa silaha hizo(NTP)

Tangu mwaka 2013 mikutano mitatu ya kimataifa imeitishwa kujadili madhara ya kibinadamu yasababishwayo na matumizi ya silaha za nyukilia na mapema mwaka huu mkutano mwingine uliokuwa na lengo la kuzuia silaha hizo pia uliitishwa.

Mwandishi: Isaac Gamba/dw

Mhariri: Gakuba Daniel

 

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com