UN yaonya kuhusu hali Sudan Kusini | Matukio ya Afrika | DW | 14.07.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

UN yaonya kuhusu hali Sudan Kusini

Umoja wa Mataifa umeonya kuhusu kuzuka upya mapigano Sudan Kusini, baada ya siku kadhaa za makabiliano baina ya wanajeshi pinzani hali iliyosababisha maelfu ya raia kukimbia na raia wa kigeni kuondolewa nchini humo

Hofu ya mgogoro wa kibinaadamu inaendelea kuongezeka wakati mashirika ya misaada, - ambayo mengi yamelazimika kuipunguza kazi yao kwa sababu ya hali ya kiusalama – yanasema kuna uhaba wa chakula na maji.

Mpango tete wa kusitisha mapigano hata hivyo umeonekana kutekelezwa katika mji mkuu Juba kwa siku ya tatu mfululizo baada ya mapigano kuzuka kwa ghafla wiki iliyopita ambayo yalitishia kulitumbukiza tena taifa hilo change kabisa duniani katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Südsudan Evakuierung der Helfer aus Juba

Raia kigeni wanaondolewa mjini Juba

Rais Salva Kiir ametangaza msamaha, kuanzia leo, kwa waasi wa zamani wanaomtii hasimu wake wa muda mrefu kisiasa Riek Machar ambao walipambana na majeshi ya serikali mjini Juba kwa siku nne. Rais Barack Obama jana alitangaza kutumwa wanajeshi 47 nchini Sudan Kusini kwenda kuulinda ubalozi wa Marekani na wafanyakazi wake. Alisema wanajeshi 130 zaidi wako nchini Djibouti na tayari kwenda Juba ikiwa watahitajika.

Wakati huo huo, Ujerumani na Italia zinawahamisha raia wao na wa mataifa mengine, ijapokuwa safari za abiria zilitarajiwa kuanza kufanya kazi leo. Karibu watu 200, wakiwemo Wajerumani karibu 100 wanaoishi Sudan Kusini, walipelekwa Uganda na jeshi la angani la Ujerumani. Raia wa Uingereza, Ufaransa, Australia, Marekani, Poland na kwingineko pia walikuwa kwenye ndege hizo za Ujerumani pamoja na wachina watatu wa jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa. Nao maafisa wa India na ndege mbili za kijeshi zilianza kuwahamisha karibu raia 600 wa Kihindi waliokwama nchini humo.

Umoja wa Mataifa umesema karibu watu 36,000 wamekimbia makwao na kutafuta hifadhi katika kambi za Umoja wa Mataifa, makanisa na ofisi za mashirika za misaada tangu machafuko hayo yalianza Ijumaa iliyopita.

Südsudan Opposition Soldaten

Wanajeshi wa upinzani walipambana na wa serikali

Shirika la hisani la Save the Children limesema kuna miili iliyotapakaa barabarani, maduka yameporwa, amsoko yamefungwa, watu wanapanga mistari ya kupewa chakula na familia zinajaribu kuukimbia mji huo. Maafisa wa shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwashughulikia Wakimbizi wanasema karibu watu 20,000 wamekusanyika katika eneo la Nimule, wakitafuta namna ya kuvuka mpaka na kuingia nchini Uganda.

Wale walioweza kuvuka wanasema wanajeshi wa Sudan Kusini wanawazuia watu kuvuka, au kuwapokonya mali zao kabla ya kuwaruhusu kupita. Hii leo msafara wa malori 50 yakisindikizwa na magari ya kivita umevuka mpaka katika eneo hilo la Nimule ili kuwaokoa Waganda waliokwama katika mji mkuu Juba karibu kilomita 200 kaskazini ya eneo hilo, na kufungua barabara salama kwa raia wanaokimbia ambao wameshambuliwa na wapiganaji na wanajeshi waasi.

Jumla ya idadi ya vifo haijulikani lakini karibu watu 300 waliuawa katika saa chache tu siku ya Ijumaa, wakiwemo walinda amani wawili wa China. Adama Dieng, Mshauri Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Uzuiaji wa Mauaji ya Halaiki anasema baadhi ya raia “walidaiwa kulengwa kwa misingi ya kabila lao".

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/Reuters

Mhariri: Mohammed Khelef