1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Wasudan wanahitaji amani, utulivu na demokrasia

4 Juni 2021

Baraza la usalama la Umoja wa mataifa limeihimiza serikali ya Sudan kuunda haraka baraza la Bunge la mpito na pia kutekeleza hatua za usalama na vipau mbele vingine katika makubaliano ya amani ya mwezi Oktoba.

https://p.dw.com/p/3uQiY
UN-Sicherheitsrat
Picha: picture-alliance/Photoshot/Li Muzi

Baraza la usalama la umoja wa mataifa limesema raia wa Sudan wanahitaji utekelezwaji wa hatua za usalama katika makubaliano ya amani na kuundwa kwa bunge la mpito ili kuwepo na amani, utulivu, demokrasia na mustakabali mzuri nchini humo.

Azimio lililopitishwa kwa sauti moja na baraza hilo pia limesisitiza kutiwa saini kwa makubaliano ya amani ili kushughulikia chanzo kikuu cha mizozo katika eneo pana la Magharibi mwa jimbo la Darfur, eneo la Blue Nile na Kusini mwa Kordofan.

Mzozo wa Darfur ulianza mnamo mwaka 2003

Baraza hilo la Usalama la Umoja wa mataifa pia limetoa mwito kwa makundi ya waasi katika jimbo la Darfur, yaliyo na vikosi katika nchi jirani kuweka chini silaha zao.

Sudan Rebellen in Nuba Mountains
Waasi nchini Sudan katika milima ya NubaPicha: picture-alliance/AP Photo/N. El-Mofty

Mzozo wa Darfur ulianza mnamo mwaka 2003 wakati Wasudan weusi walipoanzisha harakati za uasi na kuituhumu serikali ya Sudan iliyotawaliwa na Wasudan wenye asili ya kiarabu kwa ubaguzi.

Aidha serikali ya Khartoum ilituhumiwa pia kwa kulipiza kisasi dhidi ya Wasudan weusi kwa kuwapa silaha watu wa makabila ya Kiarabu, madai ambayo serikali inakanusha.

Soma zaidi: Kesi ya uhalifu wa kivita Darfur yaanza kusikilizwa ICC

Kikosi cha pamoja cha Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika katika jimbo la Darfur kilianzishwa mwaka 2007 lakini kikavunjwa na baraza la usalama mnamo Disemba 31. Na badala yake, kikosi hicho kilibadilishwa na nafasi yake kuchukuliwa na ujumbe mdogo ulioegemea zaidi kisiasa.

Jeshi la Sudan lilimuondoa madarakani Rais wa muda mrefu Omar Al-Bashir mnamo Aprili, 2019 kufuatia maandamano makubwa ya kudai demokrasia, na tangu wakati huo serikali ya mpito inayojumuisha jeshi na raia wamekuwa madarakani.

Nchi hiyo inatetereka kidemokrasia na mnamo Februari 10, baraza jipya la mawaziri liliapishwa linalojumuisha mawaziri waasi, mpango huo ukiwa kama sehemu ya kugawana madaraka kufuatia makubaliano ya amani yaliyotiwa saini mjini Juba Oktoba 3.

Waziri Mkuu Sudan asema hakuna atakaekwepa mkono wa sheria

Vile vile, baraza hilo la usalama la Umoja wa Mataifa limekaribisha makubaliano yaliotiwa saini mwezi Machi 28 kati ya serikali na kundi kubwa la waasi nchini humo, la Sudan Liberation Movement-North, makubaliano yanayoweka wazi njia za mazungumzo. Baraza hilo limeitolea wito pande zote mbili kushughulikia kwa haraka makubaliano ya amani yanayohusisha pande zote. Duru mpya ya mazungumzo ilianza mwezi Mei, 26.

Hata hivyo kundi moja la waasi, Sudan Liberation Movement linaloendesha harakati zake katika jimbo la Darfur linaipingia serikali iliyoko sasa ya mpito na pia limekataa kushiriki katika mazungumzo hayo.