1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yaidhinisha usitishwaji mapigano Syria

Sekione Kitojo
25 Februari 2018

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa  kauli  moja limeunga mkono kusitishwa mapigano nchini Syria kwa siku 30, wakati mashambulio mapya dhidi ya Ghouta mashariki yakifikisha idadi ya vifo vya raia 500.

https://p.dw.com/p/2tIHx
UN Sicherheitsrat Abstimmung über Waffenruhe in Syrien
Picha: Getty Images/AFP/D. Emmert

Kwa uungwaji  mkono  wa  Urusi , Baraza  la  Usalama  la Umoja  wa  Mataifa  liliidhinisha azimio kuhusu kusitisha mapigano  ili  kuruhusu upelekaji  wa  misaada  ya  kiutu pamoja  na  kuwaondoa  wagonjwa  na  waliojeruhiwa, "bila kuchelewa".

Baada  ya  kura  hiyo  katika  Baraza  la  Usalama, ndege za  kivita  za  Syria zikisaidiwa  na  ndege  za  kivita  za Urusi  zilifanya  mashambulio  mapya  katika  mji huo wa Ghouta mashariki, limesema  shirika   linaloangalia  haki  za binadamu  nchini  Syria.

USA UN Sicherheitsrat Nikki Haley
Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Nikki HaleyPicha: picture-alliance/newscom/J. Angelillo

Kiasi  watoto 127 ni  miongoni  mwa  watu 519  waliouwawa katika  kampeni  hiyo  ya  mashambulio ambayo  utawala wa  Syria  ulianzisha Jumapili  iliyopita dhidi  ya  eneo  hilo la  waasi, nje  kidogo  ya  mji  mkuu  Damascus, shirika hilo  la  kuangalia  haki  za  binadamu  lenye  makao  yake mjini  London  lilisema.

Kiasi ya raia 41 waliuwawa katika  mashambulizi  ya  jana Jumamosi(24.02.2018), ikiwa  ni  pamoja  na  watoto wanane. Urusi ilikana  kushiriki  katika  mashambulizi  hayo.

Russischer UN-Botschafter Vasily Nebenzya
Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa Vassily NebenzyaPicha: AFP/Getty Images/K. Betancur

Macron na Merkel kuzungumza na Putin

Haraka  kufuatia  kura  hiyo , Rais  wa  Ufaransa Emmanuel Macron na  Kansela  wa  Ujerumani Angela Merkel wamesema  watazungumza  leo  Jumapili (25.02.2018) na  Rais  wa  Urusi Vladimir Putin  kuhakikisha kwamba  makubaliano  hayo  ya  kusitisha  mapigano yanatekelezwa "katika siku zinazokuja," Ikulu  ya  Ufaransa imesema  katika  taarifa.

Ufaransa na  Ujerumani  zilipambana  kupata  uungwaji mkono  wa  Urusi  kwa  makubaliano  hayo  ya  kusitisha mapigano  nchini  Syria , ambayo kwa  kiasi  kikubwa  ni kuruhusu misaada  kufika  katika  eneo  hilo  lililozingirwa na  kuruhusu  kuondolewa  kwa  watu.

EU Gipfel Macron Merkel
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron(kushoto) na kansela Angela Merkel wa UjerumaniPicha: picture-alliance/abaca/D. Aydemir

Kura  hiyo  katika  Umoja  wa  Mataifa  awali  ilitarajiwa kufanyika  siku  ya  Alhamis, lakini  ilicheleweshwa  mara kwa  mara  wakati  wanadiplomasia  wakivutana  katika majadiliano  makali  kuepuka kura  ya  veto  ya  Urusi , ambayo kijeshi  inaiunga  mkono  serikali  ya  Rais Bashar al-Assad.

"Kila dakika  ambayo  baraza liliisubiria  Urusi, madhila  ya binadamu  yaliongezeka," amesema  balozi  wa  Marekani katika  Umoja  wa  mataifa  Nikki Haley baada  ya  kura hiyo, akiishutumu Urusi kwa  kuzuwia.

Balozi  wa  Urusi  Vassily Nebenzia  alipuuzia shutuma hizo za  kuburuza  miguu, akisema  kwamba  majadiliano yalihitajika  ili  kufikia  madai  ya   kusitisha  mapigano ambayo  "yatawezekana."

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe

Mhariri: Caro Robi