1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yafuatilia majaribio ya kuzuia mchakato wa uchaguzi Libya

Bruce Amani | Zainab Aziz
30 Novemba 2021

Umoja wa Mataifa umeelezea wasiwasi kuhusu kulazimika kufungwa kwa mahakama ya rufaa ya Libya.

https://p.dw.com/p/43eKE
Lybien Saif al-Islam Gaddafi, Sohn des libyschen Führers Muammar Gaddafi
Picha: Mast Irham/dpa/picture alliance

Mahakama hiyo inahitajika kuamua kama mtoto wa aliyekuwa rais wa nchi hiyo marehemu Muammar Gaddafi anaweza kugombea urais.

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya umesema katika taarifa kuwa unafuatilia ripoti kuwa kundi lenye silaha lilizuia kimabavu utenda kazi wa mahakama hiyo katika mji wa Sabha kusini magharibi mwa nchi.

Majaji wa mahakama hiyo wana jukumu la kuamua kama Seif al-Islam Gaddafi, ambaye wakati mmoja alitarajiwa kuwa mrithi wa baba yake, ataweza kugombea urais, baada ya kuwasilisha mahakamani pingamizi dhidi ya uamuzi wa wiki iliyopita uliomzuia kushiriki uchaguzi huo.

Tume ya uchaguzi ilitoa orodha ya wagombea ambao hawakutimiza vigezo vya kuwania, miongoni mwao Seif al-Islam.

Uchaguzi huo unaokaribia kufanyika ni matokeo ya miaka mingi ya mazungumzo yaliyoongozwa na Umoja wa Mataifa kati ya pande zinazopingana nchini Libya.

Seif al-Islam alizuiwa kwa sababu ya hukumu zilizopita dhidi yake.
Seif al-Islam alizuiwa kwa sababu ya hukumu zilizopita dhidi yake.Picha: Libyan High National Elections Commission via AP/picture alliance

Tume ya uchaguzi nchini Libya wiki iliyopita lilitoa orodha ya wagombea 25 kati ya wagombea 98, ambao hawakutimiza masharti ya kugombea nafasi hiyo ya juu na miongoni mwao alikuwepo Seif al-Islam ambaye alizuiliwa kwa sababu ya hukumu kadhaa za awali  zinazomkabili ikiwemo ile ya mwaka 2015 ambapo alihukumiwa kifo na mahakama ya mjini Tripoli kwa makosa ya kuamuru kuwashambuliwa waandamanaji mnamo mwaka 2011. Maandamano hayo yalikuwa ya kuupinga utawala wa baba yake Muammar Ghadafi.  

Hata hivyo uamuzi huo umetiliwa shaka na wapinzani nchini Libya. Sababu nyingine iliyofanya Saif al. Ghadaffi ashindwe kukidhi vigezo ni kwamba anatafutwa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai kwa tuhuma za kutenda uhalifu dhidi ya ubinadamu kuhusiana na kuhusiana na makundi yalifanya uasi dhidi yanutawala wa baba yake.

Uchaguzi wa Libya unaosubiriwa kwa muda mrefu sasa unakabiliwa na changamoto nyingine, ambazo hazijatatuliwa kama vile maswala ya sheria zinazosimamia uchaguzi, na migogoro ya hapa na pale miongoni mwa makundi yenye kumiliki silaha. 

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya UNSMIL umesema una wasi wasi mkubwa kutokana na kuendelea kufungwa kwa Mahakama ya Rufaa ya Sebha.
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya UNSMIL umesema una wasi wasi mkubwa kutokana na kuendelea kufungwa kwa Mahakama ya Rufaa ya Sebha.Picha: AFP/F. Belaid

Vikwazo vingine ni pamoja na mgawanyiko mkubwa ambao umebakia kati ya upande wa mashariki na magharibi ya nchi na uwepo wa maelfu ya mamluki na askari kutoka nchi za kigeni.

Kuongezea wasiwasi unaotanda kwenye uchaguzi huo wa urais nchini Libya, ni kutokana na hatua ya kutangaza kujiuzulu nafasi yake aliyekuwa Mjumbe wa Umoja wa Matafa nchini humo Jan Kubis aliyewasilisha barua yake ya kujiuzulu wiki iliyopita.

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya UNSMIL umesema una wasi wasi mkubwa kutokana na kuendelea kufungwa kwa Mahakama ya Rufaa ya Sebha ambapo majaji wanazuiwa kufanya kazi zao walizopewa kisheria, hali ambayo inazuia moja kwa moja mchakato wa uchaguzi.