1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Walinzi waliwaua wahamiaji

Angela Mdungu
4 Julai 2019

Umoja wa Mataifa umesema wakimbizi na wahamiaji waliokuwa wakijaribu kukimbia shambulizi la ndege lililoua takribani watu 53 wakiwemo watoto sita walipigwa risasi na walinzi

https://p.dw.com/p/3LZNq
Libyen: Kämpfer der LNA
Picha: Getty Images/AFP/A. Doma

Umoja wa Mataifa umesema umepokea taarifa za kupigwa risasi wakimbizi na wahamiaji waliokuwa wakijaribu kukimbia shambulizi la ndege lililoua takribani watu 53 wakiwemo watoto sita katika kituo kinachowashikilia wahamiaji hapo jana.

Kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa watu wanaodaiwa kuwaua wakimbizi katika kituo wanamokuwa wakishikiliwa ni walinzi wa Libya na kwamba kulikuwa na mashambulizi mawili ya ndege, moja likilenga gereji iliyokuwa tupu na shambulizi jingine ni lile lililolenga kituo kilichokuwa na wakimbizi na wahamiaji 120.

Muda mfupi baada ya kushambuliwa kwa kituo hicho na vikosi vinavyodaiwa kuwa ni vya Jenerali muasi Khalifa Haftar, Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan mapema hii leo 04.07.2019 amemtaja Jenerali huyo muasi kuwa haramia.

Rais Erdogan ametoa kauli hiyo ikiwa pia ni siku chache baada ya mabaharia sita raia wa Uturuki kushikiliwa kwa muda mfupi na vikosi vya Jenerali Haftar wakati alipoilaumu uturuki kwa kuchangia vikosi vyake kushindwa kuudhibiti moja ya mji muhimu wa Libya.

Türkei Präsident Erdogan
Raisi wa Uturuki Recep Tayyip ErdoganPicha: Getty Images/AFP/A. Weiss

Hayo yanajiri huku Erdogan akithibitisha kuwa Uturuki iliipatia silaha serikali ya Libya kwa madai kuwa ni muhimu katika vita dhidi ya Haftar ambaye anasaidiwa na mahasimu wa Uturuki, Misri pamoja na nchi za falme za kiarabu.

Erdogan asema yuko tayari kuzipatanisha Iran, Marekani

Wakati huo huo, Rais  Erdogan, amesema yuko tayari kuwa mpatanishi kati ya Marekani na Iran zilizo kwenye mvutano juu ya mpango wa nyuklia wa Iran. Sehemu ya mazungumzo ya Erdogan, yaliyochapishwa leo imesema amezungumza na Waziri mkuu wa Japan, Shinzo Abe juu ya uwezekano wa upatanishi wakati walipokuwa katika mkutano wa mataifa yenye nguvu G-20 yaliyofanyika mwishoni mwa mwezi uliopita.

Hata hivyo, pamoja na Erdogan kuwa tayari kuipatanisha Marekani na Iran, nchi yake inakabiliwa na kitisho cha kuwekewa vikwazo vya kiuchumi na Marekani baada ya Serikali ya Trump kusema inapanga kufanya hivyo na huenda wakaiondoa kwenye mpango wa ndege za kivita iwapo itapata mfumo wa ulinzi wa anga kutoka kwa Urusi.

Hayo yanajiri muda mfupi baada ya Trump kukutana ba Erdogan nchini Japan mwishoni mwa Juma lililopita na Erdogan kusema kuwa nchi yake itasamehewa kuwekewa vikwazo na Marekanii iwapo mfumo wa Urusi wa kujilinda S400 utawasili Urusi katika siku zijazo.