UN wahimiza mbinu za kuzuia kuharibika kwa hali ya hewa | Masuala ya Jamii | DW | 28.11.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

UN wahimiza mbinu za kuzuia kuharibika kwa hali ya hewa

Ripoti ya Umoja wa Mataifa inaeleza kuwa jukumu la kuilisha dunia yenye njaa inaendelea kuwa ngumu kwani mabadiliko ya hali ya hewa na kupungua kwa ardhi na rasilimali nyingine kunadhoofisha mifumo ya chakula.

Ripoti hiyo ya Shirika la Chakula na Kilimo na Umoja wa Mataifa, FAO, iliyotolewa leo inaeleza kuwa kuongezeka kwa idadi ya watu kunahitaji upatikanaji mkubwa zaidi wa chakula bora kwa bei nafuu. Lakini kuongeza uzalishaji mashambani ni vigumu ikizingatiwa hali mbaya ya raslimali, kwani binadamu wamezidisha viwango vya kile ambacho ardhi inaweza kubeba kwa suala la ardhi, maji na mabadiliko ya hali ya hewa.

Upatikanaji chakula pia unahatarishwa na ugomvi wa kiraia pamoja na migogoro mingine. Nchini Yemen, ambapo maelefu ya raia wameuawa kutokana na mashambulizi ya angani yanayofanywa na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia, shirika la kimataifa la kuwasaidia watoto, Save the Children, limesema watoto elfu 85 chini ya umri wa miaka mitano huenda walifariki dunia kutokana na njaa au magonjwa kufuatia vita hivyo.

Kadhalika, Shirika la Mipango ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa imesema kwamba uzalishaji wa hewa chafu duniani uliongezeka tena mwaka 2017 baada ya miaka mitatu ya kusimamishwa, ikiashiria kwamba ni muhimu kwa mataifa kutekeleza Mkataba wa Kihistoria wa Paris wa kuiweka ongezeko la joto duniani chini ya nyuzi joto 2.

Mkuu wa shirika hilo, Satya Tripathi, amesema kuna ushahidi wa kutosha kwamba mataifa hayachukui hatua za kutosha kubadili hali hiyo.Satya amesema, "Kwa sasa tunaelekea nyuzi joto 3.2. Iwapo tunahitaji kuteremka hadi nyuzi joto mbili, tunafaa kuweka juhudi mara tatu. Iwapo tunataka kufikia nyuzi joto 1.5 tunafaa kuweka juhudi mara tano zaidi ya tunachokifanya kwa sasa. Kuna ushahidi wa kutosha wa kuaminika kuwa tunafaa kufanya vizuri kuafikia malengo yetu."Hayo yakijiri, Tume ya Ulaya leo inazindua ripoti ya Muungano wa Ulaya ambayo inaeleza kuwa itapunguza uzalishaji wa hewa chafu hadi sufuri ifikapo mwaka 2050, ishara ya kuwepo kwa ajenda kuu ya hali ya hewa. Pendekezo hilo linajiri siku kadhaa kabla ya mkutano wa mataifa wanachama wa Mpango wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, utakaoanza Jumapili tarehe 2 Desemba, mjini Katowice, Poland.

Ripoti hiyo aidha imetoa mfululizo wa mapendekezo ikiwemo kuboresha hisa za makaazi, kupanua sekta ya nishati mbadala, kuimarisha umeme wa nishati mbadala ili kujitenga na mafuta yanayochafua mazingira na kubuni mtandao mzuri wa usafiri.

Mwandishi: Sophia Chinyezi/APE/AFPE
Mhariri: Mohammed Khelef

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com