1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiAsia

UN: Vita vya Yemen vitagharimu maisha ya watu 377,000

24 Novemba 2021

Shirika la Umoja wa Mataifa la mipango ya Maendeleo UNDP limesema vita vya Yemen vilivyodumu kwa miaka saba vitakuwa vimegharimu maisha ya watu 377,000 ifikapo mwisho wa mwaka huu.

https://p.dw.com/p/43OPz
Jemen Sanaa | Unterernährung
Picha: Mohammed Hamoud/AA/picture alliance

Katika ripoti yake iliyochapishwa Jumanne, shirika la Umoja wa Mataifa la mipango ya Maendeleo UNDP limesema takriban asilimia 60 ya vifo vitakuwa vimesababishwa na athari zisizo za moja kwa moja na vita kama vile ukosefu wa maji safi, baa la njaa na magonjwa ilhali vita vyenyewe vitagharimu maisha ya watu wapatao 150,000.

Ripoti hiyo ya UNDP imeongeza kuwa, wengi waliokufa mwaka huu ni watoto wadogo wanaokabiliwa na utapia mlo.

Ripoti hiyo imeongeza, "Mwaka 2021, mtoto wa Yemen chini ya umri wa miaka mitano hufariki kila baada ya dakika tisa kutokana na vita."

Vita vya Yemen vinaelezwa kusababisha mgogoro mkubwa zaidi wa kibinadamu duniani kote. Shirika hilo la Umoja wa Mataifa la mipango ya maendeleo pia limesema katika ripoti yake kuwa vita vimerudisha nyuma maendeleo ya taifa hilo la Magharibi mwa Asia.

Soma pia: Hali ya Kiutu yazidi kuwa mbaya nchini Yemen

Zaidi ya asilimia 80 ya wakaazi nchini humo wanahitaji msaada wa kibinadamu, wakati uchumi wa nchi hiyo ukiwa ukingoni mwa kuporomoka, ripoti hiyo imeendelea kueleza.

UNDP inakadiria kuwa, iwapo vita hivyo vitaendelea basi watu wapatao milioni 1.3 watakuwa wamekufa ifikapo mwaka 2030.

Hata hivyo katika hatua ya kutia moyo UNDP imesema ikiwa vita vya Yemen vitakwisha sasa, angalau yapo matumaini siku za usoni kwa nchi hiyo ya Magharibi mwa Asia kufikia hadhi ya kipato cha kati ifikapo mwaka 2050.

UNDP inakadiria watu wapatao milioni 1.3 watakuwa wamekufa ifikapo mwaka 2030

Jemen Marib Provinz | Angriff von Huthi-Rebellen
Wapiganaji watiifu kwa serikali ya YemenPicha: AFP

Ama kwa upande mwengine, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limeonyesha wasiwasi wake juu ya usalama wa raia katika mkoa wa Marib, wakiwemo zaidi ya watu milioni moja wanaoripotiwa kupoteza makaazi yao.

Msemaji wa UNHCR Shabia Mantoo akiwa Geneva, amesema watu wapatao 40,000 wamelazimika kutoroka Marib tangu mnamo mwezi Septemba.

"Shirika la UNHCR lina wasiwasi kuhusu usalama wa raia katika mkoa wa Marib, wakiwemo watu wapatao milioni moja waliokimbia makaazi yao. Wakati vita vikiendelea, maisha yao yanakuwa hatarini na inakuwa vigumu kwa misaada ya kiutu kuwafikia."

Soma pia: Waasi 40 wa Houthi wauwawa kwenye mapigano Yemen

Muungano wa jeshi unaoongozwa na Saudi Arabia uliivamia Yemen mnamo mwaka 2011 ili kuisaidia serikali baada ya wanamgambo wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran kuuteka mji mkuu wa Sanaa.

Juhudi zinazoongozwa na Umoja wa Mataifa za kujaribu kusitisha vita hivyo vya mawakala kati ya Saudi Arabia na Iran zinaonekana kugonga mwamba. Wanamgambo wa Houthi wanasema wanapambana na mfumo wa ufisadi na uvamizi wa kigeni.