1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Ubaguzi wa rangi dhidi ya waafrika ni wa kimfumo duniani

Sylvia Mwehozi
28 Juni 2021

Mkuu wa Ofisi ya Haki za Haki za Binaadamu wa Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet, amesema kuwa ubaguzi wa rangi dhidi ya watu wenye asili ya Kiafrika bado ni wa kimfumo katika sehemu nyingi ulimwenguni

https://p.dw.com/p/3vgCv
Proteste zum ersten Jahrestag von George Floyd
Picha: STRF/STAR MAX/IP/picture alliance

Katika ripoti ya dunia iliyochangiwa na mauaji ya Mmarekani Mweusi, George Floyd, yaliyofanywa na afisa polisi wa kizungu huko Minneapolis, Marekani, mnamo Mei mwaka 2020, Bachelet amesema hatua ya polisi kuwakamata watu kwa kuwabagua kwa rangi zao na matumizi ya nguvu kupitiliza bado yameshuhudiwa katika maeneo mengi ya Amerika ya Kaskazini, Ulaya na Amerika ya Kusini.

Bachelet ameongeza kuwa ubaguzi wa kimfumo unatengeneza vizingiti kwa jamii za wachache kushindwa kupata ajira, huduma za afya, makaazi, elimu na haki.

"Tunahitaji kubadili mwelekeo katika kushughulikia maeneo ambayo husababisha ubaguzi wa rangi na majanga ya kujirudia yanayoweza kuepukika kama kifo cha George Floyd. Natoa wito kwa mataifa yote kuacha kukana na kuanza kuondoa ubaguzi wa rangi, kuondoa kinga ya kutoadhibiwa na kujenga uaminifu, kusikiliza sauti za watu wa asili ya Kiafrika, na kukabiliana na historia ya zamani na kutoa suluhisho."

Kamishna huyo mkuu wa haki za binaadamu amekaribisha "hatua zenye kutia moyo" za rais wa Marekani, Joe Biden, kwa kusaini amri mnamo mwezi Januari kuelezea ubaguzi wa rangi kote nchini Marekani. Ripoti yake hiyo aliyoitoa kwa Baraza la Haki za Binaadamu, imeorodhesha vifo 190 vya Waafrika na watu wenye asili ya Kiafrika kote duniani waliopoteza maisha mikononi mwa maafisa wanaotekeleza sheria ambao ni "nadra kuwajibishwa".

Maandamano ya kupinga ubaguzi wa rangi Minnesota
Maandamano ya kupinga ubaguzi wa rangi MinnesotaPicha: Brandon Bell/Getty Images

Ripoti hiyo ilichagua kesi saba za mfano, ikiwemo kesi ya mauaji ya Floyd. Afisa wa polisi wa Kizungu, Derek Chauvin, alihukumiwa kifungo cha miaka 22 na nusu siku ya Ijumaa kwa mauaji ya Floyd. Vidio ya mauaji yake ilizusha hasira na maandamano ya kitaifa kuhusu maisha ya mtu mweusi kuwa yana umuhimu.

Wahanga wengine ni mvulana wa Kiafrika mwenye asili ya Brazil mwenye umri wa miaka 14 aliyepigwa risasi katika operesheni ya polisi dhidi ya wauza unga huko Sao Paulo, Mei mwaka 2020, pamoja na Mfaransa mwenye asili ya Mali aliyefariki akiwa kizuizini Julai mwaka 2016.

"Ubaguzi wa rangi dhidi ya Waafrika na watu wenye asili ya Afrika, mara nyingi umejikita katika sera na mazoea ya kushusha hadhi ya watu binafsi katika jamii", ilisema ripoti hiyo.

Vitendo hivyo vimekuwa vikionekana zaidi katika nchi zenye historia ya utumwa, au ukoloni na kuathiri jamii kubwa za watu wenye asili ya Kiafrika. Kulingana na Bachelet, "ubaguzi wa kimfumo unahitaji mfumo wa kukabiliana nao" na kwamba hivi sasa kuna fursa ya kufanya mabadiliko na kuondoa ubaguzi wa rangi na kusimamisha haki.