1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Sudani Kusini iko katika hatari kubwa

17 Novemba 2016

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameonya kuwa Sudan Kusini iko katika hatari ya kuingia katika matatizo makubwa kufuatia ongezeko la hotuba za chuki zinazohamasisha ghasia za kikabila.

https://p.dw.com/p/2Sogc
Sudanesische Flüchtlinge in Äthopien Flüchtlingslager
Picha: DW/Coletta Wanjoyi

Katika ripoti iliyotolewa jana katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, Ban alisema kuwa vikosi vya kulinda amani nchini Sudan Kusini vinapungukiwa nguvu na uwezo wa kuzuia uhalifu huo ikiwa utatokea, pamoja na kuwa taasisi anayoiongoza inaendelea kufanya juhudi za utekelezaji wa majukumu yake katika kuwalinda raia,  kwa kutumia njia uwezo wote ilionao. Hata hivyo ametahadharisha kuwa Umoja wa Mataifa hauna uwezo wa kufika mahali pote, wala uwezo  wa kuzuia uhalifu wa kiwango kikubwa.

Ban amerejelea wito wake kwa baraza hilo wa kuiwekea vikwazo Sudan Kusini, nchi ambayo inaitaja kuwa imejaa silaha, na aliongeza pia kitendo cha serikali kuzuia harakati za vikosi cha vya kulinda amani kimesababisha kuzorota kwa juhudi  za oparesheni za kulinda raia katika taifa hilo changa duniani.

Mkurugenzi wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya misaada ya kibinadamu, John  Gink, ambaye pia hivi karibuni ametembelea nchi za Haiti, Sudan na Sudan Kusini ameunga mkono hoja ya katibu mkuu Moon wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika Jumatano.(16.11.2016)

Südsudan Rebellenführer Riek Machar in Juba
Viongozi wa Sudan Kusini Riek Machar na Salva KiirPicha: Reuters/Stringer

"Katika nchi hizi tatu ambazo nimezitembelea Sudan Kusini ni moja ya nchi ambayo iko katika njia ya hatari, katika kila kitu ambacho kinafanya kazi katika nchi kuna hali ya kuzorota" alisema Gink.

Hatari ya kutokea mauaji ya halaiki

 Adama  Dieng mshauri maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu kuzuia mauaji ya halaiki ambaye aliambatana na Gink katika kuzitembelea nchi hizo wiki iliyopita pia alionya kuwa Sudan Kusini iko katika hatari kubwa ya kuelekea katika mauaji ya halaiki

Sudan Kusini  iligawanywa na mapigano ya kikabila muda mfupi baada ya kujipatia uhuru wake kutoka Sudan mwaka 2011, mwaka 2013 nchi hiyo ilitumbukia  katika vita vya wenyewe kwa wenyewe wakati ambao vikosi vya serikali ambavyo ni tiifu kwa Rais Salva Kiir na kabila la Dinka walikabiliana na kikundi cha waasi kilicho chini ya  Rais Machar ambaye ni kutoka kabila la Nuer.

Makubaliano ya amani yalisainiwa mwaka 2015 lakini hata hivo mapigano yaliendelea, maelefu ya watu wameuwawa na wengine milioni mbili wameyakimbia makaazi yao. Katika ripoti hiyo Ban amependekeza kuwa mamlaka ya vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa  vilivyopelekwa mara ya kwanza mwaka 2011 viongezewe mwaka zaidi.

Mwandishi: Celina Mwakabwale/AP

Mhariri:Gakuba Daniel