UN: Mashambulizi Syria yalisababisha vifo vya raia wengi | Matukio ya Kisiasa | DW | 06.03.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

UN: Mashambulizi Syria yalisababisha vifo vya raia wengi

Wachunguzi wa Umoja wa Mataifa wamesema mashambulizi ya anga yaliyofanywa na Urusi na muungano wa majeshi unaoongozwa na Marekani yaliwaua raia wa Syria kwa kiasi kikubwa mwaka uliopita.

Wachunguzi wa Umoja wa Mataifa wamesema kuwa mashambulizi ya anga yaliyofanywa na Urusi na muungano wa majeshi unaoongozwa na Marekani yaliwaua raia wa Syria kwa kiasi kikubwa mwaka uliopita, huku serikali ya Assad ikifanya mashambulizi ya kutumia silaha za kemikali katika eneo linalodhibitiwa na waasi la Ghouta Mashariki.

Wachunguzi hao wa uhalifu wa kivita wamesema leo kuwa wapiganaji wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS na makundi mengine ya wanamgambo wanahusika na uhalifu wa kivita ikiwemo mashambulizi yaliyosababisha mauaji ya raia na kuwatumia raia kama ngao ya kujikinga.

Uchunguzi huo uliochukua miezi sita hadi Januari 15 mwaka huu, umeeleza kuwa wakati wa kipindi hicho, waathirika wa mzozo wa Syria wameteseka kwa kiasi kikubwa wakati ambapo ghasia zinazidi kuongezeka nchi nzima. Ripoti ya tume hiyo ya wachunguzi wa Umoja wa Mataifa imebainisha kuwa vikosi vya serikali ya Syria vimeendelea kutumia silaha za kemikali dhidi ya makundi ya wapiganaji wenye silaha Ghouta Mashariki.

Schweiz Paulo Pinheiro auf der Syrien Kommission der UN (REUTERS/D. Balibouse)

Mwenyekiti wa tume ya uchunguzi ya UN, Paulo Pinheiro

Paulo Pinheiro, aliyeongoza tume hiyo ya Umoja wa Mataifa amesema ndege za Urusi zilihusika katika shambulizi la anga lililofanyika Novemba 13 mwaka uliopita katika jimbo la Idlib na kuwaua kiasi ya watu 84 na kuwajeruhi wengine 150 katika soko moja. Amesema shambulizi hilo linaweza kuchukuliwa kama uhalifu wa kivita.

''Tume yetu imethibitisha kuwa ndege za Urusi zilitumia silaha za kutawanyika katika eneo lenye raia. Kulingana na sheria ya kibinaadamu ya kimataifa, mashambulizi ya kutumia silaha na mbinu kama hizo huenda zikachukuliwa kama uhalifu wa kivita,'' alisema Pinheiro.

Watu 150 waliuawa Raqqa

Aidha, mashambulizi matatu ya anga yaliyofanywa na majeshi yanayoongozwa na Marekani katika shule karibu na Raqqa Machi mwaka 2017 yaliwaua watu 150, takriban mara tano zaidi ya idadi iliyothibitishwa na wizara ya ulinzi ya Marekani ambayo ilisema wakati huo kwamba wapiganaji kadhaa ndiyo waliuawa na sio raia.

Wachunguzi hao wamegundua hakuna ushahidi unaoonyesha kwamba wapiganaji wa IS walikuwa katika eneo hilo na kwamba muungano huo wa kijeshi ulikiuka sheria za kimataifa kwa kushindwa kutekeleza jukumu lake la kuwalinda raia.

Ama kwa upande mwingine, Urusi imesema leo kuwa maafisa wake wanajadiliana na mashirika ya misaada ya kibinaadamu kuhusu mpango wa kupeleka msaada mpya siku ya Alhamisi Ghouta Mashariki. Umoja wa Mataifa umesema msafara uliokuwa ukipeleka misada katika mji wa Douma ulilazimika kugeuza hapo jana, kutokana na kuendelea kwa mashambulizi ya makombora.

Syrien Hilfskonvoi (Reuters/B. Khabieh)

Msafara unaopeleka misaada Ghouta Mashariki

Wakati huo huo, jeshi la Urusi leo limewaruhusu waasi wa Syria katika eneo la Ghouta Mashariki kuondoka kwakutumia njia ya kupitisha misaada ya kibinaadamu huku wakiwa na familia zao pamoja na silaha. Afisa wa jeshi la Urusi, Vladmir Zolotukhin amesema njia hiyo haikufunguliwa tu kwa ajili ya raia wa Ghouta Mashariki, bali pia wapiganaji na familia zao.

Wakati hayo yakijiri, vikosi vinavyopigania demokrasia nchini Syria, SDF ambavyo vinaungwa mkono na Marekani vimetangaza leo kuwa vitawaondoa wapiganaji 1,700 kutoka kwenye maeneo ya mapambano dhidi ya IS na kuwapeleka katika eneo la Afrin ambako Uturuki inapambana na wapiganaji wa Kikurdi.

Ufaransa na Uingereza zimetoa ombi la kufanyika mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kujadili hatua ya kushindwa kutekelezwa mpango wa kusitisha mapigano kwa siku 30 nchini Syria. Baraza hilo litakutana kesho Jumatano.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP, AP, Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com