1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Uhuru wa vyombo vya habariKimataifa

UN: Waandishi habari wakimbia nchi zao kutokana na vitisho

23 Mei 2024

Maelfu ya waandishi habari wamekimbia nchi zao kuepuka ukandamizaji wa kisiasa na kuepuka migogoro, lakini wakiwa uhamishoni mara nyingi wako katika hatari ya vitisho vya kimwili, kidijitali na kisheria.

https://p.dw.com/p/4gC3x
Visuelle Journalisten in Nahost & Afrika | Kameramann beim NY-Forum Africa
Picha: Godong/picture alliance

Maelfu ya waandishi wa habari wamekimbia nchi zao katika miaka ya hivi karibuni kuepuka ukandamizaji wa kisiasa, kuokoa maisha yao na kuepuka migogoro, lakini wakiwa uhamishoni mara nyingi wako katika hatari ya vitisho vya kimwili, kidijitali na kisheria.

Haya yameelezwa jana na mchunguzi wa Umoja wa Mataifa Irene Khan.

Katika ripoti kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Khan amesema idadi ya waandishi habari walioko uhamishoni imeongezeka kwa sababu nafasi ya vyombo huru vya habari imekuwa ikipungua katika mataifa ya kidemokrasia ambapo mienendo ya kimabavu inazidi kushika kasi.

Soma pia: Juhudi za kukuza uhuru wa habari zapungua duniani

Khan amesema kwa sasa, vyombo huru vya habari vinavyounga mkono demokrasia na kuwawajibisha wenye mamlaka aidha havipo ama vimebanwa katika zaidi ya mataifa theluthi moja duniani ambapo zaidi ya theluthi mbili ya watu duniani wanaishi.

Mchunguzi huyo huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu ukuzaji na ulinzi wa haki ya uhuru wa maoni na kujieleza, amesema baadhi ya vyombo huru vya habari pamoja na waandishi wengi wa habari, wameziacha nchi zao ili waweze kuripoti na kuchunguza kwa uhuru na bila hofu au upendeleo.