UN kushinikiza mazungumzo Burundi | Matukio ya Afrika | DW | 19.01.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

UN kushinikiza mazungumzo Burundi

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wataishinikiza serikali ya Burundi kukubali kufanya mazungumzo na upande wa upinzani chini ya mpatanishi mpya watakapofanya ziara mjini Bujumbura wiki hii.

Hayo yamesemwa na mwanadiplomasia wa Umoja wa Mataifa, Jamal Benomar, ambaye amesisitiza kuwa mazungumzo hayo lazima yaongozwe bila kuupendelea upande wowote na yawe na muda makhsusi, baada ya kushindwa kwa jaribio la Uganda kuzipatanisha pande hizo mbili ili kukomesha vurugu za miezi kadhaa nchini Burundi.

Wajumbe 15 wa Baraza la Usalama watafanya ziara yao ya pili nchini Burundi siku ya Alhamisi katika muda wa chini ya mwaka mmoja, wakiwa na matumaini ya kuepusha kile wengine wanachohofia kuwa ni kurudi katika vita vikubwa vya wenyewe kwa wenyewe. Benomar aliwambia waandishi wa habari kuwa "Warundi wanayo nafasi ya kuja pamoja na kujadili namna wanavyoweza kusonga mbele."

Marais wa zamani wa Burundi Pierre Buyoya (kushoto) na Sylvester Ntibantunganya wakiteta na wajumbe wa Marekani wakati wa mazungumzo yaliofanyika Entebbe Uganda.

Marais wa zamani wa Burundi Pierre Buyoya (kushoto) na Sylvester Ntibantunganya wakiteta na wajumbe wa Marekani wakati wa mazungumzo yaliofanyika Entebbe Uganda.

Lakini alisema ili waweza kulifanya hilo, watahitaji kuwa na mchakato shirikishi unaoongozwa pasipo na upendeleo wowote, wenye muda maalum, bayana, ajenda, makubaliano juu ya nani atashiriki, mambo ambayo alisema yanakosekana hadi wakati huu.

UN yaimarisha uwepo wake Burundi

Mjumbe huyo hakusema iwapo Umoja wa Mataifa unapaswa kubeba jukumu hilo, lakini chombo hicho cha kimataifa kinaimarisha uwepo wake nchini Burundi kwa kutuma ujumbe wa watu 20 wiki hii.

Burundi ilitumbukia katika umwagaji damu mwezi Aprili 2015, baada ya Rais Pierre Nkurunziza kutangaza nia yake ya kuwania muhula wa tatu, na hatimaye kushinda mwezi Julai. Tangu hapo, mamia ya watu wameshauawa katika vurugu hizo na zaidi ya 100,000 kukimbilia mataifa jirani.

Mkuu wa Shirika la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa, Zaid Ra'ad al-Hussein, alisema wiki iliyopita kwamba ishara za hatari, zikiwemo mwelekeo unaoongezeka wa kikabila wa mgogoro huo, vinatia hofu na akatoa wito wa kufanyika uchunguzi wa haraka. Zeid alitolea mfano wa madai kwamba vikosi vya usalama vya Burundi viliwabaka wanawake kimakundi, kuzizika maiti katika makaburi ya halaiki, na vilikuwa vinazidi kutumia mateso.

Wanajeshi wa Burundi wametuhumiwa kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binaadamu, ubakaji na mauaji ya watu wengi.

Wanajeshi wa Burundi wametuhumiwa kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binaadamu, ubakaji na mauaji ya watu wengi.

Mgogoro mgumu

Akiuelezea mgogoro wa Burundi kuwa ni mgumu, Benomar alisema ukiukaji wa haki ulikuwa unatendeka kwa kiasi kikubwa, katika muktadha wa uasi na kupambana dhidi ya uasi. Wajumbe wa Baraza la Usalama watawasili mjini Bujumura siku ya Alhamisi kwa mkutano wa siku mbili na wapinzani, mashirika ya kiraia na pia Rais Nkurunziza.

Wanadiplomasia hao wanapanga pia kupitia mjini Addis Ababa kufanya mazungumzo na Umoja wa Afrika, kuhusu pendekezo lake la kutuma kikosi cha kulinda amani nchini Burundi, baada serikali kulikataa pendekezo hilo.

Siku ya Jumatatu, polisi ilisema watu watatu waliuawa baada ya watu wenye silaha waliokuwa kwenye pikipiki, kufyatua risasi katika baa moja, ambapo msemaji wa polisi Pierre Nkurikiye aliwataja waliouwa kuwa ni afisa wa polisi, afisa mwandamizi wa wizara ya elimu pamoja na wakili.

Mauaji hayo yalifanyika katika kitongoji cha Bwiza na wauaji walitoroka baada ya shambulizi hilo.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/dpae,rtre,afpe

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

IJUE DW

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com